Wanasiasa, akiwamo rafiki yangu Zitto Kabwe, wanasema Rais John Magufuli, ameongeza ugumu wa maisha.
Wanahadharisha juu ya idadi ya watu wanaoachishwa kazi katika hoteli, viwanda na sekta mbalimbali kwa miezi michache hii ya uongozi wake.
Zinatolewa sababu za mtikisiko huo, lakini linalotazamwa zaidi ni uamuzi wa Rais wa kubana ‘kila kona’ matumizi ya fedha ambayo wengi wanakubaliana naye kwamba yalikuwa ya anasa mno.
Sitaki kumpinga Zitto na wenzake wanaoamini hivyo, ingawa napata shida kujua utafiti huo wameufanya wapi na kwa kuwahoji kina nani.
Naamini kama tungepata sampuli ya wanaolalamikia ugumu wa maisha uliosababishwa na uongozi wa Rais Magufuli, tungekuwa mahali pazuri zaidi pa kuwajadili.
Walau kwenye kauli hii ya wanasiasa kuna ukweli unaosemwa, ingawa chanzo cha kweli cha hali hii hakisemwi. Kuna kundi kubwa (siyo dogo) la wale waliozoea kuishi kwa ujanja-ujanja ambao sasa wanapata shida.
Kama watu waliishi kwa kukwepa ushuru na kodi mbalimbali, halafu hao hao wakawa na roho nzuri ya kutununulia bia, kutuchangia harusi, kipaimara na hata rambirambi, sidhani kama kukosa kwao fedha kunaweza kusiwe na athari za moja kwa moja kwao na kwetu sisi tuliofaidi fedha hizo.
Nasema haya ya kina Zitto yana chembe ya ukweli kwa sababu siku hizi baa nyingi zinakosa idadi ya wateja iliyozoeleka kutokana na uhaba wa pesa. Ingawa wanasema hivyo, ukweli wenyewe bado wanaendelea kunywa, lakini sasa kwa adabu na kwa siku maalumu! Wale tuliozoea kuanzia na kumalizia siku baa-kwa kutumia fedha tulizopata kwa kupiga simu tu – leo mambo ni tofauti. Tunakunywa kwa kuchagua tunywe siku gani. Wapo waliochagua wanywe Ijumaa, wengine Jumamosi, wengine Jumapili.
Sisi wengine tuliojiandaa, tukaingia baa ilhali tukiwa hatuna chochote mifukoni, isipokuwa maneno yetu matamu na hadithi nyingi za kuvutia tulizotumia kushawishi tununuliwe pombe, leo hatuna namna.
Hatuna namna kwa sababu wale tuliowachekesha nao wakafurahi hata wakaweza kutununulia vinywaji na kutulisha vyakula vya aina kwa aina, leo wamebadilika. Wamekuwa mikono ya birika! Hawamwagi fedha kama zamani kwa sababu wanazipata kwa jasho. Mbwembwe hazijakoma, lakini zimepungua. Sehemu za starehe unaweza kusema ni kama barabarani-ajali zipo, lakini zimepungua!
Anachosema Zitto kinaweza kuwa na ukweli kwa sababu kama kiwanda kilikuwa hakilipi kodi maana yake ni kwamba faida iliyopatikana ilikuwa kubwa mno, na kwa sababu hiyo kila mwenye kiwanda hakusita kuajiri ndugu na hata jamaa za marafiki zake bila kuangalia idadi. Kila aliyemweleza mwajiri wake: “Bosi, nina ndugu yangu hana kazi.” Alijibiwa, “Mlete tu ajishikize. Hakuna shida.” Leo hayo yanapungua.
Baada ya Rais Magufuli, kubana kampuni na viwanda vilipe kodi stahiki, wamiliki wanapunguza idadi ya wafanyakazi ili wabaki na idadi stahiki. Wakati serikalini kulijaa wafanyakazi hewa, sekta binafsi kulitamalaki wafanyakazi sanamu tu-wasiokuwa na kazi ya kufanya, lakini walilipwa.
Kunapotokea watu wakakosa ajira kwa sababu viwanda vimeamua kuajiri watu kulingana na mahitaji halisi, sioni hapo kuna lawama anazostahili kuzipata Rais Magufuli. Vinginevyo tuamue basi nchi hii iwe ya wakwepa kodi ili hizo zinazokwepwa ziwanufaishe wachache kama ilivyokuwa.
Mara kadhaa Watanzania tumesemwa kwamba tuna utamaduni wa kuishi ki-ujanja ujanja. Juzi, kumetolewa takwimu za utafiti zikionesha asilimia 71 ya Watanzania ni ‘kula kulala’. Hili lipo. Tujiulize, katika familia zetu ni wangapi wanafanya kazi ili kuwalisha watu wangapi. Mara nyingi ni mtu mmoja au wawili wanaofanya kazi kwa ajili ya kutunza kaya zenye watu 10 au zaidi.
Maisha yetu ya ujanja ujanja tumeyaendekeza kiasi cha kuamini kuwa ndivyo inavyopaswa kuwa. Bahati mbaya tukajisahau kwa kudhani ujanja-ujanja huu ungedumu kwa miaka yote. Sasa kaja kiongozi anayetaka tuchape kazi ili kila mtu asiyekuwa kilema, mtoto mdogo au mzee; apate stahili ya malipo kulingana na kazi.
Rais Magufuli, anatenda anachomaanisha. Aliposema “Hapa Kazi Tu”, wengi tuliyachukulia maneno hayo kama porojo ya kisiasa. Tukadhani huyu hatakuwa tofauti na mtangulizi wake. Kinyume chake, ameamua kuishi kwa vitendo kwa kauli yake ya kusisitiza uchapaji kazi.
Ajira zinatengenezwa na sisi wananchi wenyewe. Serikali na wadau wengine kazi yao kubwa ni kutuwekea mazingira ya uwezeshwaji ili tupate njia nzuri ya kufanya kazi na kutuwezesha kupata tija.
Serikali haiwezi kuweka mazingira mazuri-kwa mfano- katika kilimo kama haina fedha za kujenga miundombinu ya umwagiliaji, pembejeo na kadhalika. Fedha za kufanya mambo hayo hazitoki kwingine isipokuwa kwetu sote kwa kuchapa kazi na kulipa kodi kadri inavyotakiwa.
Juzi juzi kumeibuka mjadala mkubwa wa sisi kunyimwa fedha kutoka Marekani. Mjadala ule umetuwezesha baadhi yetu kutambua ni nani walio na mawazo huru na nani wenye mawazo tegemezi yaliyojiegemeza kwenye ombaomba.
Madhila ya kuwa ombaomba yamezungumzwa vizuri mno na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, mwaka 1967. Maandiko yake yaliyo kwenye vitabu vyake vya Ujamaa ni Imani, yamemaliza kila kitu. Hatuhitaji mawazo mengine mapya ya kutueleza faida za kujitegemea na hasara za kuwa tegemezi. Kilichobaki ni kufanya kazi tu.
Rais Magufuli, anataka Tanzania ijitegemee. Kama hatuwezi kujitegemea kwa asilimia 100 (jambo ambalo si rahisi sana), basi walau tujitegemee kwa asilimia zaidi ya 90. Utegemezi huu wa kutarajia hata vyoo tuvipate kwa “Hisani ya Watu wa Marekani” ni fedheha kubwa.
Lakini hatuwezi kujitegemea kama kuna watu wanaoshangilia wizi, ufisadi na uporaji rasilimali za umma na ukwepaji kodi ambao sasa Rais Magufuli, ameamua kuuvalia njuga.
Lipo tishio kwamba kuna wafanyabiashara wanajipanga kugoma kuagiza bidhaa! Kwa maneno mengine wanachomaanisha ni kuwa Rais Magufuli, aruhusu waendelee kukwepa kodi ili waendelee kuzalisha ‘ajira’ nyingi za aina hii inayolalamikiwa na kina Zitto.
Kuna mamia, kama si maelfu ya watumishi wa umma ambao muda huu wamekosa masurufu kwa safari za nje ya nchi kutokana na agizo la Rais Magufuli. Zipo taarifa za mashirika ya ndege kama Emirates kupunguza safari kutokana na uhaba wa abiria ambao sote tunajua walikuwa ni watumishi na viongozi wa umma.
Watu walilipana fedha bila kujali mamilioni ya makabwela wanaokosa huduma muhimu za kijamii mijini na vijijini. Hao waliolipana hivyo walitumia mapato hayo kwa mambo yao. Mitaani wakaonekana watu wa maana na waliobarikiwa. Hao waliokatiwa mirija hawawezi kuacha kulalama. Hawatasita kupita huku na kule wakimsema vibaya Rais Magufuli. Heshima zao katika maeneo ya starehe na mitaani zimeshuka. Wana chuki iliyopindukia. Hata hivyo, wakati hao wakilalama na kueneza finta mbaya kwa Serikali ya Awamu ya Tano, makabwela wanachekelea. Walau sasa wanauona mwanga.
Wanaendelea kuishi wakiwa na imani kubwa ya kuona Serikali yao ikinyoosha mambo mengi yaliyopinda.
Wakulima wanafarijika kwa imani ya kupata pembejeo sahihi na kwa muda sahihi ili kupitia shughuli halali za kilimo, waweze kupambana na adui umaskini. Wanashuruku kwa kuwa wanaona nuru yenye kuwawezesha kutumia mizani yenye uwiano wa kimaisha.
Zitto ni mbunge. Anajua namna wabunge walivyokuwa wakigawana posho. Anajua zilikuwa zikiandaliwa semina pale Dodoma. Semina tatu-moja ikifanyika bungeni, nyingine St. Gasper Hotel na nyingine Dodoma Hotel. Anajua walichofanya wabunge ni kupita kote huko kuandika mahudhurio na kurejea maskani kusubiri muda wa kufungwa semina. Muda ulipowadia walipita kukusanya posho za vikao vyote vitatu! Mirija hiyo inapofungwa, lazima kuwepo watakaolalamika-wabunge na wapambe wao!
Lakini tunapozungumza kuwa maisha ya sasa ni magumu, lini yalikuwa mepesi? Leo kijana anaweza kupanda daladala kwenda Kariakoo, lakini wakati wa kurudi akatumia usafiri wake wa bodaboda aliyonunua! Je, hilo zamani liliwezekana? Nani alikuwa akimiliki pikipiki kama si padri, bwana/bibi shamba, katibu tarafa na wengine wa aina hiyo?
Hao wanaosema sasa chini ya Rais Magufuli, hali ya maisha imekuwa ngumu, wanataka kutuaminisha kuwa serikali zilizopita maisha yalikuwa mteremko? Tusimkatishe tamaa Rais Magufuli kuijenga nchi hii ambayo kwa miaka 10 ilitapanywa mno.
Sehemu ya Azimio la Arusha ambalo kimsingi ni azimio la utu, inasema hivi: “Tumeonewa kiasi cha kutosha, tumenyonywa kiasi cha kutosha, tumepuuzwa kiasi cha kutosha. Unyonge wetu ndio uliotufanya tuonewe, tunyonywe na kupuuzwa. Sasa tunataka mapinduzi, mapinduzi ya kuondoa unyonge ili tusionewe tena, tusinyonywe tena na tusipuuzwe tena”.
Kila nikimtafakari Rais Magufuli, namuona ndani ya maneno haya.