Maisha bila maadui hayanogi. Maadui katika maisha ni kama viungo kwenye mboga, wanayanogesha maisha. Wanayapamba maisha ili yavutie, maadui wanakufanya umtafute na kumkumbuka Mungu usiku na mchana.

Kama una maadui wewe ni wa kupongezwa na kama hauna maadui jitafakari upya. Kukosa maadui katika maisha ni kukosa changamoto muhimu za maisha.

Watakatifu walioko mbinguni enzi za uhai wao hapa duniani walikuwa na maadui. Mtume Paulo anaeleza namna ambavyo maadui wake walimtesa.

Anashuhudia kwamba: “Mara tano nilichapwa kwa Wayahudi mapigo arobaini kasoro moja, mara tatu nilipigwa fimbo, mara moja nilipigwa kwa mawe.” (2 Wakorintho 11:24). Nilipigwa kupita kiasi (2 Wakorintho 11:23).

Hakuna mahali Mtume Paulo anasema nililipa kisasi kwa watesi wangu. Mtume Paulo anatufundisha kuiacha ile falsafa ya jino kwa jino, usijifunze kulipa kisasi. Unapolipa kisasi wewe unageuka kuwa adui wa mwenzako.

Namna bora ya kuelewana na adui yako ni kumpenda, kumuombea kwa Mwenyezi Mungu. Katika maisha usihangaike kuwachukia maadui zako, hangaika kuwaombea. 

Kuna tofauti kubwa kati ya dhambi na mtenda dhambi. Tofauti ya wazi ni kwamba mtenda dhambi ameumbwa na Mungu kwa namna hiyo. Mtenda dhambi ana asili ya ‘Umungu’ ndani yake hata kama anatenda dhambi.

Dhambi ni neno ‘Tasa’. Kwa msingi huo; mtenda dhambi ni binadamu, lakini dhambi si binadamu.

Adui yako anapokuwa dhaifu msaidie, anapokuwa mjinga mfundishe. Adui yako anapokuwa na majivuno ishi maisha ya unyenyekevu ili ajifunze unyenyekevu kutoka kwako.

Adui yako anapokuonyesha dharau, mwonyeshe heshima, anapovaa sura ya chuki, vaa sura ya upendo. Maadui wanaweza kukusaidia bila kujua. Kwa namna fulani adui yako anaweza akawa mtaji wa mafanikio yako. Goliati aligeuka kuwa mtaji kwa Mfalme Daudi.

Bila adui Goliati, Daudi asingechukua kiti cha kifalme. Mungu alimbariki Daudi kupitia kumshinda Goliati. Kwa namna fulani adui Goliati alisaidia kampeni za Daudi kukitwaa kiti cha kifalme.

Kumsamehe adui yako na kumpenda adui yako kwa uhalisia wake ni jambo gumu. Ni jambo gumu kwa maumbile yetu ya kibinadamu. Ni lazima tukiri kwamba sisi wenyewe kwa uwezo wetu hatuwezi kuwapenda maadui zetu waliotuumiza kimwili, kihisia, kiuchumi, kifamilia, kimaadili na kiroho.

Tunahitaji neema ya Mungu ili tuweze kuwapenda na kuwasamehe maadui zetu. Tumekuwa tukijiuliza: “Tufanyeje ili tuweze kuibuka washindi wa kulipa wema kwa ubaya?” Jibu ni msamaha.

Jizoeze kumpa adui yako zawadi ya msamaha. Kusamehe haimaanishi ni kushindwa vita. Methali ya Brazil inasema: “Msamehe mkosoaji wako, nawe utaibuka mshindi.”

Hatuwezi kuwapenda adui zetu kwa nguvu kama Yesu anavyoagiza sisi tuwapende kwa msaada wa Mungu tu. Hata kama hatutavaa viatu vyao, tunaweza kujifunza njia za kuwa na huruma na kuonyesha huruma kwa wale waliotuumiza sisi hatimaye kuwapenda adui zetu.

Msamaha wa kweli unadumu na unabadilisha maisha, inategemea kule kuhisi tofauti kuhusu mtu aliyekuumiza.

Ukweli ni kwamba unapokuwa umemchukia mtu yeyote yule aliyekuumiza unakuwa bado umo kifungoni. Ili utoke kifungoni ni lazima umfungue yule aliyekupeleka kifungoni.

Maumivu na uchungu hutufanya kuwa wafungwa wa mazingira ya zamani na hutukumbusha daima kile kilichotokea zamani.

Mwaka 2018 nilitoa chapisho langu la kitabu kinachoitwa ‘Usikate tamaa katika maisha’. Hiki ni kitabu ambacho kimegusa maisha ya wasomaji wengi. Wengi waliokisoma kitabu hiki wamekiri kubarikiwa na kubadilisha mienendo yao ya kimaisha.

Mmoja wa wasomaji wa kitabu hiki alinitumia ujumbe mfupi kupitia simu yangu ya kiganjani. Ujumbe huo ulinishtua kidogo, ulikuwa unasomeka hivi:

 “Habari kaka William! Mimi naitwa …, nimeletewa kitabu chako leo na mama yangu nipo nakisoma hapa. Ila nikwambie ukweli, nimeumizwa mno kiasi kwamba moyo wangu umegeuka kuwa jiwe na kamwe sitamsamehe mume wangu, mama mkwe wangu na wifi yangu mpaka wanaiacha hii dunia. Najuta kuolewa, najuta kuzaa naye. Maisha yangu ameyaharibu kiasi kwamba mimi sasa hivi nimekuwa ombaomba. Sitamsamehe milele. Nakutakia kazi njema.”

Tulio wengi tumejiapiza viapo vya kutowasamehe waliotuumiza katika maisha yetu. Viapo hivi vimetufunga, viapo hivi vinatutesa, viapo hivi vinachochea hasira na maumivu makali kila kukicha.

Tuko kifungoni, hatujui tutatoka lini. Ni kweli, umeumizwa lakini leo fungua ukurasa mpya wa maisha yako.

Viachilie leo hivyo viapo vilivyokufunga.  Msamehe mume wako aliyekuumiza, msamehe mke wako aliyekuumiza. Msamehe mtoto wako aliyekuumiza, msamehe kaka yako aliyekuumiza.

Msamehe mama mkwe wako aliyekuumiza, msamehe baba mkwe wako aliyekuumiza, msamehe mzazi wako aliyekuumiza, pia wasamehe wale wote waliokuumiza katika maisha yako. Samehe! Samehe! Samehe!

Msamehe aliyekuumiza ili na wewe usamehewe na Mungu.