Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Nzega
Wakili Edward Malando anayewawakilisha upande mmoja wa ndugu wanaovuna kwenye shauri la mirathi ya Zena Jalakhan ameomba Mahakama impe muda apitie jalada la shauri hilo.
Wakili Malando aliwasilisha maombi hayo jana katika Mahakama ya Mwanzo Nzega, mbele ya Hakimu Mfawidhi Abunas Sonyo.
Shauri hilo lilikuwa mahakamani hapo kwa ajili ya usikilizwaji wa pingamizi lililowasilishwa Februari 13, mwaka huu, lakini halikusikilizwa baada ya mahakama kukubali maombi ya Wakili Malando na kuahirisha shauri hadi Februari 27 mwaka huu.
Shauri hilo lenye mvutano, upande wa pili wanapinga Karim Samji aliyeteuliwa na Mahakama kusimamia mirathi ya Zena kutekeleza amri ya Mahakama ya kukusanya mali za marehemu.
Wakili Malando anamwakilisha Salma Mohammed ambaye alifungua shauri la mirathi ya Zainabu Jalakhan kwa mali ambayo ni nyumba iliyopo pia katika mirathi ya Zena Jalakhan.
Katika pingamizi hilo Salma amewasilisha hoja tatu, akidai kwamba shauri linalomuhusu marehemu lilikwisha sikilizwa na kutolewa uamuzi katika shauri la mirathi namba 24/2023.
Hoja ya pili mali iliyotajwa katika maombi hayo ilikwishaorodheshwa katika mirathi namba 24/2023 mbele ya Hakimu Hilda Kibona.
Na hoja ya mwisho ni kwamba shauri hilo lenye viini hivyo lilishasikilizwa na kuamuliwa na mahakama hiyo hivyo aliomba maombi ya mirathi namba 35 ya mwaka jana ya mali ya Zena Jalakhan ambayo mahakama ilimteua Karim kuwa msimamizi yatupiliwe mbali.
Mahakama hiyo mbele ya Hakimu Sonyo ilimteua Karim kuwa msimamizi wa mirathi ya mali ya marehemu Zena ambayo ni nyumba iliyopo Mtaa wa Ntinginya wilayani Nzega mkoani Tabora yenye namba NTC/NMSH/NTI/81..
Mahakama hiyo pia mbele ya Hakimu Hilda Kibona ilimteua Salma Mohammed kuwa msimamizi wa mirathi ya Zainabu Jalakhan ambayo nyumba iliyopo kwenye mirathi ni hiyo hiyo iliyopo mtaa wa Ntinginya wilayani Nzega yenye namba NTC/NMSH/NTI/81.
Hivi karibuni baada ya Mahakama kufanya Usuluhishi kwa familia hiyo, iliamuru aliyeteuliwa kusimamia mirathi, Karim akusanye mali za marehemu.
Hata hivyo katika nyaraka mbalimbali za nyumba hizo ikiwemo risiti za Kodi ya pango iliyowasilishwa mahakamani zinasomeka kwa jina la Zena Jalakhan na si Zainabu Jalakhan
Karim aliwasilisha kiapo mahakamani akidai marehemu ni mama yake mdogo, amefariki hakuwa na watoto, mume, wazazi wala wajukuu, watoto ni wa dada zake na mwombaji ndiye mtoto pekee.
Alidai marehemu hakuacha wosia na maelezo hayo yaliungwa mkono na wajukuu, Gullam Siager na Haji Seager hivyo mahakama ikamteua kusimamia mirathi hiyo.
Marehemu aliacha nyumba moja iliyopo mtaa wa Ntinginya wilayani Nzega yenye namba NTC/NMSH/NTI/81.
Wanafamilia wanufaika katika mirathi hiyo ni wajukuu, Araf Seager, Azaz Seager, Haji Seager, Asha Seager, Gullam Seager, Fatuma Seager, Kasu Seager na Karim Samji ambaye ni mtoto.