Na Suzy Butondo, JamhuriMedia, Shinyanga
Jaji Mfawidhi wa Mahaka Kuu kanda ya Shinyanga Frank Habibu Muhimbali amesema mahakama hiyo imefanikiwa kusikiliza mashauri yote kwa mwaka 2023 yakiwemo mashauri ya migogoro ya ardhi,yakifuatiwa na mashauri ya makosa ya jinai na mauaji .
Aidha amesema sababu ya mashauri hayo ya migogoro ya aridhi yakitajwa kuwa ni elimu ndogo kwa wananchi kuhusiana na sheria zinazosimamia umiliki na utatuzi wa migogoro ya aridhi, ambapo pia wamefanikiwa kwa wakati kusikiliza mashauri yote kwa mwaka 2023.
Jaji Muhimbali akizungumza na waandishi wa habari katika kuelekea kwenye maadhimisho ya wiki ya sheria nchini yanayotarajia kuanza Januari 24 hadi 30 amesema sababu mojawapo inayopelekea kuwepo kwa migogoro ya ardhi ni wananchi kukosa elimu kuhusiana na sheria zinazosimamia umiliki wa ardhi na badala yake humiliki ardhi kiholela .
Pia amesema uzinduzi rasmi wa wiki ya sheria Mkoani Shinyanga unatarajiwa kufanyika Januari 27 katika viwanja vya Zimamoto nguzo nane ukiongozwa na kauli mbiu isemayo ‘Umuhimu wa dhana ya haki kwa ustawi wa Taifa, nafasi ya mahakama na wadau katika kuboresha mfumo wa haki jinai’.
“Kila ifikapo Desemba 15 hadi Januari 31 Mahakama huwa ipo rikizo, na kipindi hicho huwa tunatumia kujitathimini na kubaini changamoto na kuzitatua, pamoja na kuadhimisha wiki ya sheria na kuanza mwaka mpya wa Kimahakama, ambapo hua tuna huanza mwanzoni mwa mwezi Februari.
“Katika maadhimisho ya wiki ya sheria tunawaomba wananchi wajitokeze kwa wingi kuja kupata elimu ya sheria bure katika viwanja vya Zimamoto pale nguzo nane, kutakuwa na utoaji wa elimu juu ya masuala ya mirathi, ndoa na talaka, makosa ya Jinai na migogoro ya ardhi,”ameongeza.
Pia amesema watakuwa na wadau kutoka Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), ambao ni wadau Muhimu katika upatikanaji wa vitambulisho hivyo, ambavyo kwa sasa ndiyo vinatumika katika ufunguaji wa Mashauri Mahakamani, pamoja na Rita kwa ajili ya kusajili vizazi ili kuwapatia utambuzi wao.
Amesema kwa upande wa Mkoa wa Simiyu wananchi wataipata elimu hiyo ya kisheria katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Mahakama ya wilaya Itilima, Busega, Meatu, Maswa, ambapo pia watatembelea Magereza na baadhi ya Shule.