Mahakama ya Katiba nchini Korea Kusini Jumatatu imetupilia mbali uamuzi wa Bunge wa kumuondoa Waziri Mkuu Han Duck-soo, na kumrudisha rasmi katika wadhifa wake kama kaimu rais.
Han alishika nafasi hiyo baada ya Rais Yoon Suk Yeol kuondolewa madarakani kutokana na kutangaza sheria ya kijeshi mwezi Desemba mwaka jana, hatua iliyosababisha mgogoro mkubwa wa kisiasa nchini humo.
Katika hukumu yake, mahakama hiyo ilipiga kura 7-1 kutengua uamuzi wa bunge, ikieleza kuwa matendo ya Han hayakukiuka uaminifu wa umma na hivyo hayakustahili kumuondoa madarakani. Mara baada ya hukumu hiyo, Han alirejea kazini na kutoa ujumbe wa umoja kwa taifa.
Katika hotuba yake kwa taifa, Han alisema: “Nitazingatia maslahi ya taifa lote na watu wetu na kusikiliza kila sauti ili taifa letu lisonge mbele katika zama za busara na mantiki. Ninaomba kwa dhati ushirikiano kutoka pande zote za kisiasa ili taifa letu lishinde mgogoro huu na kusonga mbele kwa maendeleo.”
Aidha, Han aliongeza kuwa kipaumbele chake kikubwa ni kukabiliana na changamoto za kiuchumi, hasa mvutano wa kibiashara duniani, ambao umeongezeka kufuatia kuingia madarakani kwa Rais wa Marekani Donald Trump.
