Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imesema imefungwa mikono kusikiliza kesi ya kusambaza taarifa za uongo inayomkabili aliyekuwa Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dkt.Wilbroad Slaa kwa kuwa upande wa Serikali umekata rufaa mbili katika Mahakama ya Rufaa.

Hayo yameelezwa leo na Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki wakati mahakama ilipotoa wito wa kuitisha shauri hilo baina ya upande wa Jamhuri na Utetezi, licha ya kwamba shauri hilo lilipangwa kuitishwa February 6, 2025.

Hata hivyo, licha ya mahakama kutoa wito huo mshtakiwa ambaye ni Dkt.Slaa hakuwepo mahakamani hapo kutokana na changamoto ya usafiri wa kutoka gerezani hadi mahakamani.

Hatua ya upande wa Serikali kukata rufaa ni kupinga uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu ya Tanzania, Januari 30, 2025 ambayo ilitoa amri ya kwamba kwamba shauri hilo lirudi Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ili liendelee.

Itakumbukwa kwamba upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Peter Madeleka uliwasilisha hoja Mahakama Kuu ya Tanzania juu ya marejeo ya kesi iliyopo Kisutu kuhusu uhalali wa hati ya mashtaka na dhamana ya Dkt.Slaa.

Hakimu Nyaki amesema “Kwa msingi huo basi nachelea kusema kwamba mikono yangu imefungwa kwa sababu kuba rufani mahakama kuu ambapo kesi itakuwa inasikilizwa huko, ila kwa huku itakuwa inatajwa kama kawaida ili kujua maendeleo ya mshtakiwa,”.

Hadi kufikia leo ni siku 20 Dkt. Slaa anasota korokoroni kutokana na kukosa dhamana ambapo alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza January 10, 2025 akikabiliwa na shtaka moja la kusambaza taarifa za uongo katika mtandao wa X (zamani Twitter) katika kesi ya Jinai namba 993 ya mwaka 2025.