1-mhandisi mkazi(kulia)Dejene na MagufuliKuna maneno yanayosemwa kwamba Rais John Pombe Magufuli anapaswa kuingilia kati sakata la Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar uliovurugika na kutakiwa kurudiwa tena.

Tayari Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imeishatangaza tarehe ya kurudiwa kwa uchaguzi huo. Kwa hapa nataka nilijadili hilo la kumtaka Rais Magufuli kuingilia kati sakata hilo la Zanzibar.

Ndiyo, Magufuli ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini Katiba ya nchi inampa mamlaka ya kufanya mambo kulingana na Katiba yenyewe inavyoelekeza. Siyo kwamba akiwa Rais anapaswa afanye mambo kulingana na matakwa yake.

Ikumbukwe yeye anaapa kuilinda Katiba ya nchi. Nje ya yale anayoelekezwa na Katiba atakuwa ameivunja Katiba hiyo na si kuilinda. Na ni walewale wanaomshauri aende nje ya maelekezo ya Katiba ndiyo watakaokuwa wa kwanza kumshikia bango kuwa kavunja Katiba ya nchi!

Kazi ambazo Rais anatakiwa kuzifanya, kwa mujibu wa Katiba, ni pamoja na kutengeneza Serikali, kuunda Baraza la Mawaziri kwa kuanzia na waziri mkuu, kuteua makatibu wakuu wa wizara, kuteua wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na kadhalika. Watu hao ndiyo walio kwenye mamlaka yake anapoweza kuingilia mara moja na wakati wowote na kufanya mabadiliko ikibidi kadri anavyoona inafaa.

Kwa hiyo, lolote likitokea ndani ya shughuli zinazofanywa na watu hao na kuonekana mambo hayaendi vizuri kiasi cha wananchi kuanza kulalamika, basi Rais anaweza akatakiwa kuingilia kati kwa mamlaka anayopewa na Katiba ya nchi na hivyo kumaliza mzozo wowote unaoweza kuwa umejitokeza. Huo ni wajibu wake.

Lakini linapokuja suala kama hili la Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar mambo yanakuwa tofauti. Ikumbukwe kwamba Rais wa Zanzibar anachaguliwa na wananchi wa Zanzibar kama Rais wa Jamhuri ya Muungano anavyochaguliwa na wananchi wa Tanzania, Bara na Visiwani, siyo kwamba Rais huyo wa Zanzibar anateuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Pale kuna Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kama ilivyo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). Kwa hiyo, suala la uchaguzi wa Zanzibar lipo chini ya tume hiyo. Na ikumbukwe kwamba tume hiyo ndiyo iliyoziona dosari zilizojitokeza kwenye uchaguzi uliopita na kuamua kuufuta.

Katika hali ya aina hiyo, kumbebesha Rais Magufuli lawama za kwamba haingilii kati sakata la uchaguzi huo ni kutaka kumuonea kiukatili. Ni kumbebesha mzigo ambao hahusiki nao kisa eti kwa vile yeye ni mkubwa basi abebe hata kile asichojua ndani yake kuna nini.

Ingekuwa Rais wa Muungano, kikatiba, ndiye anayemteua Rais wa Zanzibar nisingehangaika hata kidogo kumtetea Magufuli. Ningesema kwamba basi na aharakishe kutuondolea kiwingu hiki kilichotanda juu ya Taifa letu. Sasa mambo ni tofauti, kwa nini tumsakame Rais wetu kwa mambo yaliyo nje ya shughuli zake kiutumishi?

 Ingekuwa kwamba Rais wa Muungano ana mamlaka ya kuingilia uamuzi wa Tume za Uchaguzi basi asingehitaji kufanya kampeni wakati wa Uchaguzi Mkuu, angekuwa anajitangaza mara moja kwamba yeye ni Rais. Lakini sote tuliona jinsi Magufuli alivyohangaika mpaka wananchi kumkubali kuwa ndiye anayefaa kuwa kinara wao. Kayafanya yote hayo kwa unyenyekevu mkubwa kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi akielewa kuwa Tume hiyo ndiyo yenye uamuzi wa kukikubali au kukikataa alichokuwa akikifanya.

 Iweje sasa Magufuli atakiwe kubatilisha uamuzi wa Tume ya Uchaguzi ya upande wa pili wa Muungano? Ni lazima tuone kwamba kitu kinachosemwa kuhusu suala hilo kuwa hakiwezekani kabisa. Yeyote anayeleta madai ya kwamba Rais Magufuli anapaswa aingilie suala hilo anapaswa ajiangalie kwanza kama yuko sahihi na makini. Maana mtu aliye makini ndiye anayefanya mambo yaliyo makini, vinginevyo ukosefu wa umakini unaweza kuzaa kitu kisichokuwa makini ambacho wakati mwingine kinaweza kuishia kuisambaratisha jamii kwa ujumla.

 Mbali na suala hilo la kumtaka Magufuli kuingilia kati, nashindwa kuelewa hata kama angekuwa anaweza kuingilia angeingilia kutatua kiti gani? Sababu wahusika wa uchaguzi huo, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, imeishasema kwamba uchaguzi ulivurugika na unatakiwa kurudiwa. Hilo ni jambo lililo wazi. Tatizo liko wapi? Kwa nini mtu wa nje ya utaratibu huo aingilie kati?

Jambo hilo linanipa shida sana. Lakini kwa jinsi ninavyoona wapo wenye mawazo ya kumtaka Magufuli kuchukua majukumu ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar, jambo lililo kama kiinimacho! Pengine wanataka Magufuli atangaze kwamba Maalim Seif ndiye rais wa Zanzibar kama alivyojitangaza mgombea huyo!

 Hivi kweli hilo ni jambo linaloingia akilini, kwamba mtu aliamua kuvunja sheria za nchi na Rais wa Jamhuri ya Muungano amuunge mkono katika uvunjifu huo wa sheria wakati aliapa kuilinda Katiba ya nchi? Kama siyo hilo Magufuli anatakiwa akafanye nini la zaidi kuhusu sakata la Zanzibar?

 Magufuli, kama Rais wa Jamhuri ya Muungano, anachoweza kukifanya ni kuwataka wananchi wa Zanzibar kutulia na kusubiri tarehe ya marudio  ya uchaguzi ili waweze kumpata mtu wanayeona anawafaa kusudi wamkabidhi jukumu la kuwa kinara wao. Zaidi ya hilo yanayosemwa yote ni uchochezi unaolenga kuviingiza matatani visiwa vya marashi ya karafuu. Kwa hiyo, yeyote mwenye wazo hilo chafu anapaswa apingwe kwa nguvu zote.

Tumuache Rais Magufuli achape kazi kwa mwendo mdundo pasipo kumwingiza kwenye kazi ya ziada isiyomhusu. Na anayefanya hivyo ni wazi hamtakii mema Rais Magufuli.

 Nimalizie kwa kuvitakia kila kheri Visiwa vya Zanzibar kwa kaulimbiu ya jadi ya Mapinduzi Daima.