Kimsingi, bado najadili kujitegemea kwenye makala mbili zilizopita. Nilibadilisha vichwa vya habari kutokana na tukio la Rais Magufuli kuwaalika wanahabari kuelezea mafanikio ya mwaka mmoja tangu aingie madarakani.

Katika kueleza changamoto zinazoukabili utawala wa Rais Magufuli, nilitoa mfano wa Nabii Nehemia alivyoijenga Yerusalemu iliyobomolewa, na kwenye makala iliyopita, nilimsihi Magufuli akunjuke kisiasa yaani awe ‘flexible.’ 

Kwa sababu katika kuijenga upya Tanzania, Rais anahitaji mchango wa kila Mtanzania, hapaswi kumwacha mwananchi yeyote nje ya harakati zake.

Tanzania inaweza kuendelea chini ya mfumo wowote – iwe Ujamaa ama Ubepari – kinachotakiwa ni mipango chanya. Ipo mifano hai kutoka nchi kadhaa za dunia hii ambazo wananchi waliamua na wakajikwamua wakaondokana na mkwamo uliowasumbua hadi wengine wakadhani haiwezekani kujikomboa.

Ukombozi wa nchi huanza na hatua ya watu kujitambua nafasi yao na uwezo wao. Huko nyuma nilitoa mfano wa Ujerumani mara ulipoangushwa utawala wa Adolf Hitler. Nchi ilikuwa na hali mbaya, miundombinu yake iliharibiwa kwa mabomu, viwanda viliteketezwa kwa moto, bakeries zilibomolewa kwa makusudi ili zisitengeneze mikate, Wajerumani walifukua vifusi wakitafuta mizoga ya farasi ili wale. 

Lakini hatimaye wakaambizana ukweli wakasema “dunia nzima inatuchukia hatuwezi kuliendea taifa lolote likatuhurumia likatutatulia matatizo yetu” wakakubaliana kimsingi kwamba jawabu la matatizo ya Ujerumani liko mikononi mwa Wajerumani wenyewe. Chini ya kanuni hiyo, wakaijenga upya Ujerumani yao hadi ikasimama tena kama taifa lenye nguvu.

Leo natumia mfano wa Korea ya Kaskazini ambayo ilijiendeleza chini ya ukomunisti yalipoanza mageuzi yaliyoitikisa dunia. Wakorea walisema wazi ubepari hautawaletea lolote jipya zaidi ya waliyoyafanya.

Utawala wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ulijenga viwanda vingi chini ya mfumo wa Ujamaa, nao jirani zetu Kenya walikuwa na viwanda vingi chini ya ubepari, hiki ni kielelezo cha awali kwamba viwanda vinastawi chini ya mfumo wowote. Kilichoua viwanda vya Tanzania si mfumo wa Ujamaa bali ni wizi, uzembe na uongozi wa juu kukosa umakini.

Mwaka 1997 lilifanyika kongamano waliloliita ‘Ghana/Korea summit’ ambapo wataalamu mbalimbali walikutanika kubadilishana uzoefu (sharing experience). Nchi zote mbili za Ghana na Korea zilipata uhuru mwaka 1957 kwa hiyo zilitimiza miaka 50 na zilifanana na watoto mapacha waliozaliwa siku moja.

Walipoanza kulinganisha maendeleo ya kila nchi yaliyopatikana ndani ya miaka 50, ilibainika wazi Korea ilikuwa imeendelea kuizidi Ghana, Korea imeweza kutengeneza makombora ya nyuklia na inadai ikichokozwa inao uwezo wa kurusha kombora lake likatua Washington (Marekani). Lakini Ghana haina hata kiwanda cha kutengeneza bunduki za kawaida achilia mbali makombora. 

Korea inatengeneza magari yake na inauza nje ya nchi wakati Ghana haitengenezi hata pikipiki, je, kuna nini kilichoizuia Ghana isikue na kipi kilichoipaisha Korea? Katika makala hii sitaeleza yote yaliyojadiliwa kwenye mkutano ule ila nitanukuu mfano mmoja uliotolewa na wataalamu wa Korea.

Mfano huu nimeunukuu mara nyingi kwenye makala zangu huko nyuma, nawasihi wasomaji wasichoke ninaporudia kuutoa, maana ulinisisimua na pia ulinipa simanzi unavyofanana na mashambulizi ya kujitoa mhanga. Wataalamu wa Korea walisema walipoanza kujenga bwawa lao ili kuzalisha umeme teknolojia yao bado ilikuwa ya kiwango cha chini. Kompresa zao walizotengeneza zilikuwa za uwezo mdogo wa kusukuma hewa kwa saa mbili tu.

Kazi ya kufunga mitambo huko chini ilihitaji kufanywa kwa saa zisizopungua sita mfululizo pasipo kusimama. Lakini kwa jinsi walivyodhamiria nchi yao ipate umeme, mtaalamu aliingia na kompresa akijua anakwenda chini kufanya kazi ya kifundi kwa saa mbili mfululizo na baada ya hapo atakosa hewa na kufia shimoni. 

Wataalamu walijitoa mhanga wakijua wanawarithisha watoto wao na wajukuu zao umeme wa uhakika, kwa hiyo mtaalamu mmoja baada ya mwingine waliingia kwa zamu kufanya kazi kila mmoja akianzia pale alipoishia mtaalamu mwenzake aliyemtangulia. Walikufa kwa zamu mmoja baada ya mwingine na maiti zikiopolewa juu na hatimaye kazi ilikamilika. Sasa nchi yao ina umeme wa uhakika uliosukuma mbele maendeleo ya viwanda. Hayo wasingeyapata kama wangekuwa watu wa kuomba na kusaidiwa.

Wazalendo wa aina hii wanaofanana na watoto wanaoshawishiwa kuvaa mabomu na kwenda kujilipua ili kumteketeza adui, hawapatikani kwenye nchi ambayo viongozi wa juu wanaonesha ubinafsi, wanaojipendelea katika kujihudumia. Mashujaa wa aina hii hawazaliwi chini ya uongozi wa wabinafsi wanaojihami na walio tayari kuua wenzao ili tu wabaki madarakani.

Kimsingi, mashujaa hawazaliwi wakiwa mashujaa bali hutengenezwa, tatizo la nchi nyingi za Afrika viongozi wengi huingia madarakani na wengine hupigania kuingia madarakani wakiwa na msukumo wa ubinafsi bila mipango ya kujenga nchi zao. Viongozi wabinafsi hawawezi kuzalisha mashujaa wa kujitoa mhanga kwa ajili ya nchi zao.

Chukulia mfano wa kiongozi anayeona madarakani ndiyo mahala pa kutanua, akiuchukulia uongozi wa juu wa nchi sawa na fungate (honeymoon) ambapo maharusi hutafuta mahali ili waende kufurahia ndoa yao. Kiongozi wa aina hiyo hawezi kuwatengeneza wazalendo wa kiwango cha kufia taifa lao, bali anaweza kuzalisha mamluki watakaoishia kuitafuna na kuididimiza nchi yao. 

Nchi yenye mamluki haitaendelea sawa na nchi yenye wazalendo, wala nchi ambayo ndani yake watu wanawania uongozi kwa kanuni ya kufa au kupona wakiamini madarakani ndiko mahala pekee watakapojipatia pepo ya duniani, haiwezi kujiendeleza wala kuvirithisha chochote chema vizazi vinavyofuata. Katika Tanzania wabinafsi ndiyo walioua viwanda ambavyo utawala wa Nyerere ulivijenga kwa mbinu za hali ya juu ukitumia mtaji utokanao na Watanzania wenyewe.

Kwa ajili hiyo, ili kuifufua Tanzania ya viwanda, inabidi Rais Magufuli awapate watu sahihi wa kufanya naye kazi, akikosea akateua wenye tabia ya ubosi wakafanana na hao waliowahi kuitwa ‘mawaziri mizigo’, ndoto ya Tanzania kuwa na viwanda haitatimia kwa sababu nchi itaendelea kubebeshwa mizigo.

Rais anatakiwa awe na baraza dogo lenye mawaziri wachache wanaopendana na kushirikiana kama ndugu, siyo wanaoshindana kumpendeza bosi wao ili kujibakiza kwenye uwaziri.

Baraza lenye mawaziri wengi wataishia kuhujumiana wao kwa wao ili kuhami maslahi binafsi, Tanzania inahitaji baraza la mawaziri kati ya 15  hadi 20 tu wasizidi hapo. Serikali inatakiwa ibadilishe mbinu za kutekeleza miradi mikubwa ya kitaifa kwani njia inayotumika sasa ya kuijenga Tanzania katika misingi ya kibiashara, inagharimu fedha nyingi wakati hu huo nchi ikiachilia rasilimali nyingi kuchukuliwa wakati kinachojengwa hakilingani na gharama zinazotumika. (Nitaeleza kwa kutoa mifano hai huko mbele).

Katika kuijenga Tanzania, Rais anategemea nguvu ya Watanzania na utaalamu wa Watanzania, suala la ‘expertise’ na vifaa, hapa ndipo inapotakiwa kubadilisha mbinu. Nchini Japan, viwanda vingi vya magari vimeajiri wabunifu (designers) kutoka Italia kutokana na kuaminika kwamba Wataliano ni wazuri kwenye ‘designing’.

Hapa Tanzania, Serikali inaweza kuanzisha viwanda vyake vya kati kwa kutumia mtaji wa dola tukapata viwanda vya kusindika nyama, kuchakata minofu ya samaki, maziwa na kubangua korosho, lakini vimilikiwe na majeshi yetu matatu Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Magereza na JKT. Serikali inunue mitambo kutoka nchi zenye teknolojia ya wastani, mitambo isitoke kwenye nchi zilizoendelea kiteknolojia itakayokuwa ‘too sophisticated’; mitambo hiyo haitaifaa Tanzania inayoendelea.

Serikali inaweza kutangaza ajira kwa wataalamu na wenye ujuzi, ikaingia nao mikataba kwani mikataba ambayo Serikali itaingia na watu binafsi itakuwa rahisi kuliko ile ambayo Serikali inaingia na taasisi.

Kwa mfano, Jeshi la Wananchi likimiliki kiwanda cha kutengeneza silaha, ama kampuni ya kujenga madaraja na barabara, Serikali itanunua vifaa na kuajiri wataalamu kwa fani zile ambazo itatokea Watanzania hatunao. ‘Approach’ ya namna hii inatofautiana na ile ambapo Serikali inaingia mkataba na kampuni ili kujenga barabara, jengo au daraja ambapo kampuni hulipwa, kwani kuna uwezekano mkubwa wa kampuni kuongeza gharama (to inflate) ili ipate faida.

Majeshi yetu yana uwezo wa kumiliki kampuni za ujenzi na kupewa zabuni kutoka serikalini ama sekta ya umma, kampuni zikipata vifaa na kuajiri wataalamu zitajenga kama wanavyojenga Konoike au Kajima.

Mfano hai; ufisadi wa huyo aliyepewa zabuni ashone sare za polisi naye akapotea na mabilioni ya walipakodi, endapo kazi hiyo wangepewa Gereza la Ukonga lenye kiwanda cha ushonaji ingefanyika vizuri na kwa gharama nafuu, mwisho wake askari magereza wangenufaika, wafungwa wangenufaika na Taifa lingenufaika.

Jeshi la Magereza linaweza kumiliki viwanda vya kutengeneza viatu, kusindika mazao ya kilimo, kubangua korosho kama kile kilichokuwa Vingunguti kilichoitwa TANITA.

JWTZ inaweza kumiliki kiwanda ikatengeneza risasi, silaha kama bastola, bunduki nyepesi (light machine guns) na mabomu badala ya kuendelea kuagiza yote hayo kutoka nje. JWTZ inaweza hata kutengeneza magari yake, kwani chini ya Serikali ya Awamu ya Kwanza hadi mwaka 1979, JWTZ iliweza kutengeneza robo tatu ya vifaa vya magari aina ya nyumbu (mradi huo ulikuwa Kibaha). Ingetokea mradi huo kuendelezwa, leo Tanzania ingekuwa inatengeneza magari yake aina ya nyumbu.

Rais Magufuli asing’ang’anie njia moja tu ya kuvutia wawekezaji, kwani kama ameweza kununua ndege na kuifufua ATCL, anaweza pia kununua mitambo ya viwanda na akaanza na majeshi yetu matatu – JKT, Magereza na JWTZ.

Hakuna ugumu wa kuwaanzishia viwanda vya kutengeneza viatu, kuchakata ngozi, kusindika nyama, kusindika maziwa, kukamua alizeti, kuzalisha sukari kwa matumizi ya ofisi za Serikali, vyuo na shule. Faida yake fedha za Serikali na huenda hata mishahara ya watumishi wake itazunguka kwenye uvuli wa Serikali, huenda ikapunguza mtiririko wa fedha kutoka serikalini kuwaendea watu binafsi hadi Serikali inafikia kukopa kwenye mabenki.

 

Zamani, Tanbond ilitengenezwa kwa ubora wa hali ya juu na kiwanda cha Voil Tanzania, inaweza kujitegemea ikaurudia utukufu wake wa zamani, ikaachana na fedheha ya kuagiza kila kitu kutoka nje.

Mabilioni ya fedha tunazotumia kila mwaka kuagiza bidhaa zitokazo nje, ni kielelezo tosha kwamba kumbe fedha tunazo ila kinachokosekana ni mipango na ubunifu. Ila jambo moja, Rais Magufuli aelewe, Tanzania iliyoendeshwa kijamaa haiwezi ikaachana nao kijumla ndiyo maana nashauri dola iendelee kumiliki viwanda na kampuni ikitumia taasisi kama majeshi yetu matatu.

        

0786311422 na 0767311422