Kuna kila dalili kuwa Waziri wa Ujenzi, Dk. John Pombe Magufuli, amekataa au kushindwa kutekeleza maagizo ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kutokana na kilichoelezwa kuwa kuyatekeleza ni kuvunja sheria ya usalama barabarani na kanuni zake, hivyo yeye hayuko tayari kufanya hivyo.

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa tangu Waziri Mkuu Pinda atoe agizo la kuunda kamati ya kushughulikia mgogoro wa wasafirishaji wenye malori na mabasi waliotangaza mgomo Oktoba 4, 2013, baada ya Magufuli kuwatangazia faini wanaozidisha uzito, hadi leo hakuna kilichofanyika.

“Kimsingi Waziri Magufuli ameona akae kimya. Anajiuliza kuwa yeye ndiye mtuhumiwa katika kesi hii, sasa inakuwaje apewe kazi ya kuunda kamati au tume itakayochunguza uamuzi alioufanya yeye. Kwa kufuata utawala wa sheria Magufuli ni mlalamikiwa, hivyo akiunda tume au kamati, ni wazi atakuwa ana mgongano wa kimaslahi,” kilisema chanzo chetu kutoka Wizara ya Ujenzi.

Chanzo hicho kilisema hadi sasa Ofisi ya Waziri Mkuu haijawapelekea hadidu rejea za kamati hiyo ikiundwa ifanye kazi zipi na kwa mwelekeo upi, kama taratibu za uendeshaji wa shughuli za Serikali zinavyotakiwa.

“Serikali haiendeshwi kwa matamko, bali sheria na maandishi,” kilisema chanzo chetu na kuongeza: “Leo upo ofisini kesho haupo, kama kuna maandishi anayeingia anaendeleza kazi.”

Hata hivyo, chanzo kingine kilisema Ofisi ya Waziri Mkuu ilipeleka barua Wizara ya Ujenzi iliyokuwa ikisema “Mkutane na wadau wa usafirishaji kuangalia jinsi ya kumaliza tatizo hili.” Pamoja na barua hiyo, Ujenzi hawajakutana na wasafirishaji au Mwanasheria Mkuu, ambaye naye aliagizwa ashiriki katika kuunda kamati iliyopaswa kufanya kazi ndani ya mwezi mmoja kuanzia Oktoba 10, kwa kusema:

“Kwa kuwa bado kuna kutokuelewana baina ya Wizara ya Ujenzi na wasafirishaji wa malori na mabasi kuhusu utelekezaji wa kanuni 7 (3) kwamba haitekelezeki kirahisi, ninaiagiza Wizara ya Ujenzi ikutane na wadau wa usafirishaji kujadiliana kuhusu namna bora ya kutekeleza kanuni hiyo.

“Kwa hiyo, Wizara ya Ujenzi na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wanatakiwa kuunda timu ya wataalamu ambao watakutana na wawakilishi wachache wa wamiliki wa malori na mabasi (TATOA na TABOA) ili kupitia kanuni hizo kwa lengo la kupata mwafaka.

“Natoa kipindi cha mwezi mmoja kwa Wizara husika na wadau hao kukamilisha kazi hiyo. Katika kipindi hicho cha mpito, utaratibu uliokuwapo awali kabla ya tangazo la tarehe 1 Oktoba 2013 lililotolewa na Wizara ya Ujenzi, utaendelea kutumika.” Pinda aliyasema maneno haya kwenye mkutano na wahariri na hivyo Wizara inasema haikupelekewa maagizo ya kimaandishi kuhusu haya.

Chanzo cha mgogoro

Mgogoro uliibuka Oktoba 4, 2013 baada ya Wizara ya Ujenzi kuchapisha tangazo Oktoba 1, likisema kuwa msamaha wa asilimia 5 ya uzito uliozidi uliokuwa unatolewa na Serikali kwenye mizani, sasa unafutwa rasmi kwani ulitolewa kinyume cha sheria na kanuni za Usalama Barabarani mwaka 2006.

Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa msamaha huo ulitolewa na aliyekuwa Waziri wa Miundombinu wakati huo, Basil Pesambili Mramba, aliyeandika barua yenye Kumb. CKA/16/419/01 ya Julai 19, 2006.

Barua hiyo ya Mramba iliyochukuliwa kama mwongozo, ilisitisha matumizi ya Kanuni Na. 7(3) iliyokuwa inawataka wasafirishaji kutozwa faini mara nne ya mzigo uliozidi, iwapo ingeshindikana kuupanga upya au kuushusha katika gari husika.

Nia ya msingi ya kanuni hii ni kulinda barabara zinazoharibika kwa kiasi kikubwa, kutokana na magari kuzidisha uzito kwa nia ya matajiri kupata faida ya haraka.      Hata Waziri Mkuu Pinda alisisitiza hili katika taarifa yake kwa vyombo vya habari Oktoba 10, 2013.

Kubwa zaidi lililozua sintofahamu, Waziri Mkuu Pinda siku ya Oktoba 10 alipokutana na wahariri jijini Dar es Salaam, alitangaza rasmi kuwa barua iliyoandikwa na Mramba mwaka 2006 ilikuwa haina nguvu kisheria au kwa maana nyingine ilivunja sheria na kanuni za Usalama Barabarani.

“Lengo la aliyekuwa Waziri wa Miundombinu [Mramba] kwa wakati huo (2006) la kutoa msamaha wa tozo kwa uzito wa magari uliozidi ndani ya asilimia 5 wa uzito unaokubaliwa kisheria, lilikuwa ni kutafuta suluhu ya malalamiko ya wasafirishaji yaliyoletwa kwake ambayo yalisababishwa na ubovu wa barabara, matuta na mapungufu katika mizani za kupima uzito,” alisema Pinda na kuongeza:

“Hata hivyo, kwa kanuni na misingi inayojulikana ya kisheria ni kwamba Sheria au Kanuni haiwezi kufutwa kwa barua hata kama ni kutoka katika mamlaka husika. Pamoja na kwamba Mheshimiwa Waziri [Mramba] alitoa maelekezo kupitia barua, bado Kanuni zilizopo zilikuwa zikiendelea kuwepo na kutakiwa kutumika [ki]sheria.

“Katika mazingira yaliyojitokeza kufuatia barua hiyo, maelekezo yaliyotolewa kupitia barua hiyo yalikandamiza utekelezaji wa Kanuni za Usalama Barabarani za mwaka 2001. Hali hii ndiyo iliyopelekea Wizara ya Ujenzi kwa sasa kuamua kufuta mwongozo huo uliotolewa kwa njia ya barua na kutaka turejee katika kutumia Kanuni na Sheria,” alisema Pinda.

Inadaiwa kuwa maelezo haya ndiyo yanayompa nguvu Magufuli kusema hata Waziri Mkuu anamuunga mkono, hivyo anasubiri Novemba 10 ifike aanze upya kutumia sheria hiyo kwa mujibu wa tangazo lililotolewa na Wizara yake Oktoba 1, 2013.

Mramba ajibu

Aliyekuwa Waziri wa Miundombinu wakati huo, Basil Mramba, alipoulizwa na JAMHURI juu ya maelekezo yake hayo yanayodaiwa kuruhusu uharibifu wa barabara, hali ambayo hakuwapo tangu nchi hii ipate Uhuru, Mramba alisema: “Kwanza siku hizi sisemi, lakini zimepita siku nyingi kiasi sikumbuki kabisa nini kilitokea. Hata Waziri Mkuu alipotoa kauli nilikuwa naumwa na hata nilivyopona sikufuatilia. Mimi siku hizi nafanya kazi ya kushauri watu njia bora ya kufanya biashara, sitaki kujihusisha na siasa tena.”

Wizara zarushiana mpira

Katibu wa Waziri Mkuu, Ndositwe Ahonga, alipoulizwa na JAMHURI kwa nini kamati hiyo haijaundwa na kuwa muda sasa unaisha, na kuna taarifa kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu haijawapelekea barua Ujenzi kuwapa maelekezo jinsi ya kuunda kamati hiyo, alisema yeye hakudhani kama kuna ulazima wa kuwapa barua.

“Yale yalikuwa maelekezo halali ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na yalitolewa kwenye kikao halali. Waziri [Magufuli] alikuwapo na Katibu wa Waziri [Ngusa Samike] alikuwapo. Nilitaraji kuwa alikuwa Katibu anachukua kila kinachoendelea na alipaswa kumwandikia waziri wake kwa ajili ya utekelezaji. Hebu mtafute Katibu wa Waziri anaweza kuwa na majibu,” alisema Ahonga.

Pamoja na Samike kutopatikana ofisini baada ya kuelezwa kuwa alikuwa safarini Kigoma, na baadaye Mwanza wakiwa pamoja na Waziri Magufuli, Msemaji wa Wizara ya Ujenzi, Injinia Martine Ntemo, aliiambia JAMHURI kuwa suala hilo ni zito na kwa kuwa lipo katika ngazi ya Waziri Mkuu, Waziri Mkuu ndiye wa kulizungumzia.

“Hili suala linanizidi kimo, ni ama umuone Mheshimiwa Waziri [Magufuli] mwenyewe au Mheshimiwa Waziri Mkuu [Pinda] ndiyo wenye mamlaka ya kulizungumzia,” alisema Ntemo.

Magufuli kwa upande wake, mara zote hakupokea simu na hata alipotumiwa ujumbe mfupi hakujibu, huku Waziri Mkuu akijibu kupitia kwa Katibu wake Ahonga.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema, ambaye naye alipaswa kushiriki kuunda kamati ambayo hadi sasa haijaundwa aliliambia JAMHURI kwa ufupi “Wizara ya Ujenzi inaratibu jambo hilo. Ungewauliza.”

Wasafirishaji waonya

Wasafirishaji waliozungumza na JAMHURI walieleza bayana kuwa siku nne kuanzia leo hawajui nini kitaendelea.

“Waziri Mkuu alisitisha lile tangazo kwa mwezi mmoja. Mwezi huu unaisha Novemba 9, sasa sijui nini kitatokea baada ya hapo maana Mheshimiwa Pinda hakulifuta tangazo la Magufuli, bali alisitisha kwa mwezi mmoja, hivyo litaanza kufanya kazi rasmi,” alisema mmoja wa wasfirishaji aliyedai msamaha huo ukifutwa wataumizwa.

 

Katibu wa Chama cha Wamiliki wa Mbasi Tanzania (TABOA), Enea Mrutu, aliiambia JAMHURI kuwa aliyepaswa kuunda kamati hiyo ni Waziri Mkuu, wao wanasubiri hadi hiyo siku atakapounda kamati.

“Iwapo mwezi huo utaisha wakarejesha hiyo sheria tutagoma,” alisema Mrutu.

 

Msemaji wa Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (TATOA), Elias Lukumai, aliiambia JAMHURI kuwa Waziri Mkuu ndiye aliyetengua tangazo la Magufuli, hivyo wao kama wao hawana cha kusema.

“Tunachosubiri ni kuitwa kwenye hiyo kamati tuweze kutoa dukuduku letu. Kucheleweshwa kwa kamati hii nadhani kumetokana na shughuli za Bunge, hivyo Bunge litakapoisha wanasubiri kuona Serikali itawapa utaratibu upi,” alisema Lukumai.

Uhalisia wa mambo

Mjumbe na Mshauri wa Chama cha Madereva wa Malori Tanzania, Rocket Matogolo, alisema wao kama wao wanamuunga mkono Waziri Magufuli, kwani magari yanaharibu barabara na wao ndiyo wanaopata kadhia barabarani kwa magari kuharibika na kupinduka wakapoteza maisha na si waajiri wao.

“Uamuzi wa Magufuli ni mzuri na unastahili pongezi. Hii ni vita ya matajiri na Waziri sisi haituhusu. Faida wanapata ila hawaridhiki,” alisema Matogolo.

Msimamo wa madereva unatokana na taarifa kwamba matajiri wengi hawataki kuwaajiri madereva na badala yake wanawataka wapakie mizigo ya nyongeza kujipatia fedha za kuendesha maisha yao.

“Kwenye malori, mzigo unaopakiwa kutoka bandarini unakuwa na uzito unaotakiwa, lakini kwa kuwa madereva hawaajiriwi inabidi waongeze mkaa, matenga ya nyanya na mizigo ya kwenda mikoani kuweza kupata fedha ya kula na mshahara wao wa mwezi.

“Unakuta dereva wa basi anaendesha basi kutoka Dar es Salaam hadi Bukoba bila ajira au mshahara, hivyo hiyo asilimia 5 isiyotozwa faini tajiri anamwambia dereva ndiyo ajilipe kwa kupakia mizigo.

 

“Hii ina ubaya wake. Magari yanapakiwa kuliko wezo na kimsingi kinachoharibika si barabara tu, bali hata magari yenyewe yanaharibika na kuisha kabla ya muda wake, kutokana na kupakiwa mizigo kuliko uwezo na mwisho wa siku yanasababisha ajali. Nasema Waziri Magufuli yuko sahihi, hata leo ikibidi malori na mabasi yasiruhusiwe kuzidisha mzigo,” alisema dereva mmoja anayeendesha magari ya kwenda Congo.

Baadhi ya kampuni hazizidishi uzito

Kinachoshangaza wengi ni kuwa baadhi ya kampuni zinazofanya biashara sawa na hawa wanaong’angania asilimia tano, hazizidishi uzito siku zote na Waziri Mkuu Pinda katika mkutano wa Oktoba 10, alizisifia kampuni hizi kwa kusema:

“Wapo wasafirishaji wengine ambao wamekuwa wakizingatia vizuri kanuni hizo na kwa muda mrefu hawazidishi uzito. Napenda kuchukua nafasi hii kutambua na kuyapongeza makampuni yafuatayo ambayo kwa takwimu nilizopatiwa, yanaonekana kuwa hayazidishi uzito unaoruhusiwa. Makampuni hayo ni yafuatayo:

 

“Dar Express (Buses), Cargo Star (Lorries), Hood (Bus), BM (Bus), Coca-Cola (Lorries), Bakhresa (Lorries), TBL (Lorries), Golden Coach (Bus), Kanji Lalji (Lorries), Tawaqal (Lorry/Bus), Consolidated Logistic (Lorry), Ramada Transport (Lorry) na BP-Puma (Lorries).

Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa baadhi ya wafanyabiashara wamechangia kwa kiasi kikubwa kuhujumu mtandao wa reli nchini, kwa kuwa wanapata faida kubwa kusafirisha mizigo kwa malori, ambayo yanaharibu barabara zinazojengwa kwa gharama kubwa.