Uamuzi wa Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, kutangaza rasmi kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, umezidi kunogesha mchuano wa kuwania nafasi hiyo ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kwa muda mrefu sasa, Waziri huyo amekuwa akitajwa kuwa miongoni mwa wana CCM wenye nia ya kuomba ridhaa ya chama hicho kwa ajili ya kupeperusha bendera yake kwenye Uchaguzi Mkuu utakaoshirikisha vyama vingi vya siasa.
Duru za uchunguzi zinaonyesha kuwa tayari kambi zenye nguvu, kama ile ya Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, zimeanza kujipanga vilivyo kukabiliana na Dk. Magufuli.
Anatajwa kuwa na sifa zinazokaribiana na za Lowassa, hasa kwenye uchapaji kazi.


Hata hivyo, tofauti na Lowassa, Dk. Magufuli anatajwa kutokuwa na mizizi imara ndani ya CCM kwa vile hajawahi kuwa mjumbe katika vikao vya juu vya chama hicho, isipokuwa Mkutano Mkuu wa Taifa anaoingia kwa nafasi yake ya ubunge.
Kuingia kwake kwenye mpambano huo kunatajwa kuongeza chachu ya ushindani, hasa kutoka kwa makada wenzake wenye majina makubwa kama Bernard Membe, Lowassa, Profesa Mark Mwandosya, Stephen Wasira, Mizengo Pinda, Makongoro Nyerere, Profesa Sospter Muhongo; na wengine ambao hawajatangaza rasmi, akiwamo Dk. Emmanuel Nchimbi.


Dk. Magufuli, anasema anaingia kwenye mchuano huo akiwa na sifa zote stahiki za kupiga na kupigiwa kura.
Alitangaza azma yake hiyo muda mfupi nje ya ukumbi wa Bunge mjini Dodoma baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu, wiki iliyopita.
Baada ya kuulizwa kama ana mpango huo, mara moja alisema: “Swali hili nimeulizwa mara nyingi. Mara zote nimekataa kulijibu kwa sababu chama chetu (CCM) kuna utaratibu wake wa namna ya kuomba nafasi ya uongozi. Muda ulikuwa haujawadia.
“Lakini utakumbuka wiki hii hapa hapa Dodoma vikao vya juu vya chama chetu vimetoa ratiba kwa wanaotaka kuwania nafasi mbalimbali kujitokeza.


“Kwa maana hiyo sasa niko huru kujibu swali lako kwa kusema rasmi ‘nitagombea urais’. Nafanya hivyo kwa sababu naamini ninazo sifa za kuchagua na kuchaguliwa kama mwanachama wa CCM kwa nafasi yoyote inayojitokeza kulingana na na Katiba ya chama chetu na pia Katiba ya nchi.”
Tofauti na wagombea wengine walioamua kutangaza nia zao kwa mbwembwe, Dk. Magufuli ameliambia JAMHURI kwamba atakachofanya ni kwenda kuchukua fomu na kuanza kutafuta wadhamini mikoani.
Dk. Magufuli amekuwa mbunge tangu mwaka 1995. Baada ya kushinda ubunge mwaka huo alichaguliwa kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi; Wizara iliyokuwa ikiongozwa na Anna Abdallah.
Anajulikana kama kipenzi cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya Nne, Benjamin Mkapa, ambaye mara kadhaa hakusita kumsifu hadharani, akimtaja kama mmoja wa ‘askari wa miavuli’ katika Baraza lake la Mawaziri.


Aidha, uhusiano wake na Mkapa umejidhihirisha hadi kwenye masuala ya kifamilia ambako mara kadhaa Rais huyo mstaafu ameweza kuhudhuria hafla na misiba mbalimbali nyumbani kwa Dk. Magufuli.
Wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 Dk. Magufuli alipewa fursa mwenye Mkutano Mkuu wa CCM kusoma mafanikio ya chama hicho kwenye utekelezaji wa Ilani yake upande wa barabara.
Uwezo wake wa kukariri takwimu mbalimbali ulikuwa kivutio kwenye mkutano huo na sehemu nyingine kama bungeni ambako hutakiwa kueleza mafanikio ya wizara yake.


Hivi karibuni, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Ali Hassan Mwinyi, alimsifu kwa kumtaja kama ‘simba wa kazi’ kutokana na uchapaji kazi wake katika wizara mbalimbali ambazo ameziongoza.
Kwa upande wa wananchi, wengi wanamuona Dk. Magufuli kama mmoja wa mawaziri wachapakazi waliowahi kutokea katika historia ya taifa letu.

Wasifu
Dk. John Pombe Joseph Magufuli, alizaliwa Oktoba 29, 1959 Chato (sasa Mkoa wa Geita).
Ana Shahada ya Uzamivu ya Kemia (2006 – 2009) kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Mwaka 1991 – 1994 alisoma shahada ya uzamili (Kemia) katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na baadaye Chuo Kikuu cha Salford nchini Uingereza.
Mwaka 1985 – 1988 alisoma Shahada ya Kwanza ya Elimu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akichukua masomo ya Kemiua na Hisabati.
Mwaka 1981 – 1982: alisoma diploma katika Chuo cha Mkwawa akichukua masomo ya Kemia na Hisabati.
Mwaka 1979 – 1981 alipata elimu ya juu ya sekondari katika Shule ya Juu ya Sekondari Mkwawa, Iringa.
Mwaka 1977 – 1978 alisoma elimu ya sekondari katika Shule ya Sekondari Lake, Mwanza.
Mwaka 1975 – 1977 alisema Shule ya Msingi Katoke, Biharamulo mkoani Kagera.
Mwaka 1967 – 1974 alisoma Shule ya Msingi, Chato.

Mafunzo
Machi 1984 – Juni 1984 alihudhuria mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Mpwapwa mkoani Dodoma.
Januari 1984 – Machi 1984 alikuwa JKT Makuyuni, Arusha.
Julai 1983 – Desemba 1983 alikuwa JKT Makutupora, Dodoma.

Uzoefu wa kazi
Mwaka 2010 – hadi sasa Waziri wa Ujenzi na Mbunge wa Chato.
Mwaka 2008 – 2010: Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Samaki; Mbunge wa Biharamulo Mashariki (Chato).
Mwaka 2005 – 2008: Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; na Mbunge wa Biharamulo Mashariki (Chato)
Mwaka 2000 – 2005: Waziri wa Ujenzi, na Mbunge wa Biharamulo Mashariki.
Mwaka 1995 – 2000: Naibu Waziri wa Ujenzi; na Mbunge wa Biharamulo Mashariki.
Mwaka 1989 – 1995: Mkemia Chama cha Ushirika cha Nyanza Cooperative Union (Ltd.) Mwanza.
Mwaka 1982 – 1983: Mwalimu Shule ya Sekondari Sengerema (akifundisha masomo ya Kemia na Hisabati).
Amepata tuzo mbalimbali za ndani na nje ya nchi. Ameshiriki na kuongoza mikutano mingi ya kitaifa na kimataifa. Tofauti na wanasiasa wengine wengi, Dk. Magufuli ameandika vitabu na majarida mbalimbali ya kitaaluma. Ameoa na ana watoto kadhaa.