Ugumu wa upatikanaji wa fedha ulioibua msemo maarufu wa “vyuma vimekeza”, umebadilika kwa serikali kuanza ‘kulegeza’ baadhi ya mambo.

Manung’uniko yameanza kupungua mitaani ambako fedha ziliadimika kwa kiwango kikubwa kuanzia mwaka 2016, lakini Rais John Magufuli akisema waliokuwa wakilalamika ni mafisadi waliozoea kujipatia fedha kwa njia haramu.

Desemba 14, 2017 alipozungumza na walimu, alisema: “Watu wanaosema vyuma vimekaza, kama vimekaza weka grisi. Na hawa wanaosema hivi ni wale waliozoea vitu vya hewa. Walimu hewa, wafanyakazi hewa…hawa vyuma havitakaza tu, vitavunjika kabisa.”

Desemba 20, mwaka huo huo, Rais Magufuli akatoa maagizo kwa wale wanaodai kuwa vyuma vimekaza ilhali takwimu zikionyesha kuwa vyuma havijakaza, wafikishwe mahakamani waeleze wapi vimekaza.

Akasema: “Hata mtu akija na takwimu za kupikwa kwamba vyuma vimekaza, mpelekeni mahakamani akaeleze ametoa wapi hizo takwimu. Ninaomba kurudia tena, Watanzania tujifunze kuheshimu takwimu. 

“Ukikosea kutoa takwimu umeichafua nchi, takwimu ni kitu kibaya sana ndiyo maana kuna watu wamebobea kwenye takwimu, hivyo wananchi tuwasikilize watu wa takwimu – asitokee mtu mwingine akatoa takwimu tofauti na zile walizonazo watu wa takwimu.

“Mtu anasema vyuma vimekaza wakati watu wa takwimu wanasema vyuma vimefunguka, watu hawa wanatakiwa kukamatwa na kuwekwa ndani ili wakajifunze kutoa takwimu huko.”

Kuanza “kulainika kwa vyuma” kunatajwa kusababishwa na mambo kadhaa, miongoni mwa hayo ni hatua ya serikali baada ya kuziba mianya mingi ya rushwa, hasa rushwa kubwa kubwa kulikowezesha serikali kuwa na fedha na kuanza kujenga miradi mingi.

Watu wengi wameajiriwa kwenye ujenzi wa barabara nchini kote, ujenzi wa madaraja, ujenzi wa reli ya kisasa na pia ujenzi wa makao makuu mkoani Dodoma.

Hata hivyo, baadhi ya wananchi wanaamini kuwa mabadiliko haya yenye kuleta faraja ni staili iliyotumiwa na wakubwa serikalini ili kujiwekea mazingira mazuri ya kushinda uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika baadaye mwaka huu; pia ni maandalizi kwa ajili ya kukonga nyoyo za wapigakura kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani mwakani.

Wachambuzi wa masuala ya siasa wanabainisha baadhi ya matukio wanayoyatumia kuhalalisha hoja yao kwamba kulegea kwa vyuma ni maandalizi kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuhakikisha kinashinda uchaguzi huo wote kwa kishindo.

Baadhi ya mambo yanayotajwa ni uamuzi wa Rais Magufuli kukutana na makundi mbalimbali ya kijamii, na kubwa zaidi ni kwa wafanyabiashara.

Alipoingia madarakani mwishoni mwa mwaka 2015, Rais Magufuli alionekana kama kiongozi anayewachukia zaidi wafanyabiashara, lakini kwa miezi ya karibuni hali hiyo imekuwa tofauti.

Januari 22, mwaka huu alikuwa na mkutano mkubwa wa wachimbaji na wafanyabiashara ya madini ya aina mbalimbali jijini Dar es Salaam. Ingawa ratiba ilikuwa hairuhusu, kwa mamlaka yake akawapa muda mrefu ili watoe kero na ushauri wao. Hatua hiyo ilisaidia kuibua mambo mengi ambayo katika hali ya kawaida isingekuwa rahisi kuyafahamu.

Rais Magufuli akagusa nyoyo za wadau hao kwa kuagiza kupitiwa kwa tozo za madini ambazo wanazilalamikia mno. Tozo hizo ni Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) inayotozwa kwa asilimia 18, Kodi ya Zuio (asilimia 5), Kodi ya Ukaguzi (asilimia 1), Ushuru wa Huduma (asilimia 0.3), Mrahaba (asilimia 6). Jumla ya tozo zote ni asilimia 30.3. Kiasi hicho hakijumuishi Kodi ya Kampuni kwa mwaka ambayo ni asilimia 30 ya faida.

Katika kuitikia kilio hicho, Rais Magufuli akawaagiza viongozi wa Wizara ya Madini na Wizara ya Fedha kujadiliana na kukubaliana na wadau wa madini kuhusu utaratibu mzuri utakaoondoa kero hizo, lakini utaongeza mapato yatokanayo na madini. Akataka wapendekeze viwango vya tozo za kodi na ushuru vitakavyowavutia wadau kulipa tozo hizo badala ya kukwepa.

Faraja nyingine kubwa kwa wachimbaji hao ilitokana na agizo la Rais Magufuli kuhakikisha kuwa watu waliohodhi leseni za utafiti wa madini kwa muda mrefu bila kuendeleza maeneo husika wanyang’anywe na maeneo hayo wapewe wachimbaji wadogo.

Mwaka 2016 Tanzania ilikuwa na wachimbaji wadogo wa madini takriban 700,000 nchini kote.

Tukio jingine la kulegezwa kwa vyuma lilifanywa na Rais Magufuli Desemba 2, mwaka jana akiwa mkoani Arusha aliikemea Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kuwabambikia kodi wafanyabiashara.

Tamko la rais likawa faraja kubwa kwa wafanyabiashara wengi kuanzia kwa wamachinga hadi wafanyabiashara mabilionea ambao walikwisha kuamini kukamuliwa kwao huenda ni maelekezo ‘kutoka juu’.

Akasema TRA inatakiwa kujitathmini kwanini watu wanakwepa kulipa kodi na kuamua kutumia wamachinga na wafanyabiashara wadogo kuwauzia bidhaa zao.

Akasema wakati mwingine TRA ndio chanzo cha wafanyabiashara kukwepa kodi, kwani badala ya kujenga urafiki na wafanyabiashara wamekuwa maadui.

Alisema wingi na ukubwa wa kodi umewafanya baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wawatumie wamachinga kuuza bidhaa zao ili wasilipe kodi.

“Mnaweka viwango vikubwa ambavyo havilipiki, jambo ambalo linafanya wafanyabiashara kukwepa, hivyo ni bora kuweka viwango vidogo vinavyolipika na wengi kuliko kiwango kikubwa kinacholipwa na watu wachache,” alisema.

Akaenda mbali kwa kusema baadhi ya kodi zinazokusanywa na TRA ni za kuudhi kwani licha ya kuwa aliwaagiza kukusanya kodi kila sehemu, hakuwataka wafanye dhuluma.

“Kuna wengine wamenukuliwa wakisema ‘hapa kazi tu’, mimi nimewatuma hivyo?…Mnawakadiria watu kodi kubwa ili mpate kuomba rushwa,” alisema.

Neema nyingine ya kulainishwa vyuma ikatangazwa na Rais Magufuli pale alipoamuru wamachinga wasibughudhiwe katika maeneo yote wanayoendesha biashara zao.

Akapiga marufuku mgambo na watumishi wengine wa halmashauri zote nchini kutowabughudhi. Uamuzi wa Rais Magufuli ukawa umeua sheria ndogo za miji na majiji zinazozuia au zinazoruhusu kuendeshwa kwa biashara katika maeneo kwa mujibu wa mipango miji.

Akatangaza mpango mpya kwa kuwapa vitambulisho nchini kote kwa gharama ya Sh 20,000 kwa kila kitambulisho.

Uamuzi huo umekonga nyoyo za wachuuzi wengi nchini, ingawa baadhi yao wametumia fursa hiyo kuvamia hadi maeneo ya barabara na ya waenda kwa miguu.

Hatua hiyo ni kete kubwa kwa CCM kushinda uchaguzi kwani sekta ya wamachinga pekee ni mtaji wa kutosha wa kupata kura nyingi.

Januari 15, mwaka huu ikawa siku nyingine ya furaha kwa wavamizi wa maeneo ya hifadhi nchini baada ya Rais Magufuli kutangaza kutengua amri iliyotolewa na wizara zaidi ya nne ya kuwataka wote waliovamia maeneo hayo wawe wametoka wenyewe ndani ya mwezi mmoja.

Rais Magufuli akawaita baadhi ya viongozi, akiwamo Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, na kuwaamuru wawaache wananchi hao pamoja na vijiji na vitongoji 366 nchini kote.

Akaagiza ufanyike uhakiki ili maeneo yaliyopoteza sifa ya uhifadhi yaainishwe na yagawiwe kwa wananchi hao waliovamia hifadhi.

Amri hiyo ya rais ikawa faraja kubwa kwa wakulima, hasa wafugaji ambao wameonekana baadhi yao wakiandamana kumpongeza kwa ‘kuwaruhusu’ kuishi maeneo hayo ambayo yanalindwa kisheria.

Huruma ya Rais Magufuli ikawa imetafsiriwa vibaya na baadhi ya wananchi ambao waliamua kuanza kuvamia maeneo yaliyohifadhiwa. Hatua hiyo ikailazimu Wizara ya Maliasili na Utalii, Januari 27, mwaka huu kutoa tamko kuzuia uvamizi mpya kwenye maeneo yaliyohifadhiwa.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu, akasema: “Agizo la Mheshimiwa Rais John Magufuli halikumaanisha kuwa sasa wananchi wanaruhusiwa kuvamia, kuingiza mifugo na kulima katika maeneo ya hifadhi.”

Msimamo wa Rais Magufuli kutaka waliovamia hifadhi kwa shughuli za kilimo na ufugaji waachwe, unaonekana ni ‘ulegezaji vyuma’, kwani uko tofauti na ule alioutoa mkoani Kagera Novemba 7, 2017.

Rais Magufuli akihutubia wananchi aliwataka waache kuvamia maeneo ya hifadhi, ikiwemo Hifadhi ya Burigi na akaagiza viongozi wa Wilaya ya Muleba kufuatilia madai ya wananchi juu ya kuuzwa kwa ardhi ya kijiji; hatua iliyosababisha wakose maeneo ya kulima na kulisha mifugo yao.

“Na kuna watu waliouziwa ranchi na serikali, watu hao hawajaziendeleza ranchi hizo na badala yake wanawakodisha wananchi, wafuatilieni na mkiona hawajaziendeleza nyang’anyeni muwape wananchi wazitumie kwa ufugaji, lakini pia hakikisheni wananchi hawavamii maeneo ya hifadhi yaliyotengwa,” alisema.

Kabla ya hapo, Julai 19, 2017 Rais Magufuli akiwa mkoani Kagera alisema: “Watu wanafikiri kwamba kila mahali anaweza kwenda akafuga ng’ombe zake, ukitaka kufuga kafuge maeneo yanayopangwa kwa ajili ya kufuga, si kila mahali kwenda kufuga. Ukiona mifugo yako ipo kwenye hifadhi itoe. Hili pori tumeliweka kwa ajili ya wanyamapori ili tupate mvua, mito isikauke, ni kwa ajili ya masilahi ya vizazi vinavyokuja.

“Wewe unataka uwe na ng’ombe mpaka 3,000 ya nini? Halafu hujajenga hata nyumba, huwezi ukazifuga, uza. Simamieni kwa kuzingatia sheria za hifadhi, kama wale ng’ombe ni kutaifisha, taifisha.”

Wakati Rais Magufuli akilainisha vyuma kwa staili hiyo, mawaziri nao wamekuwa hawako nyuma.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, akitambua kuwa Watanzania wengi wamejenga katika maeneo yasiyopimwa, akatangaza urasimishaji wa nyumba zote zilizojengwa katika maeneo hayo.

Hatua hiyo ingawa ni ya huruma zaidi, lakini inalenga kuwapa faraja wananchi wa kada ya chini walioingiwa hofu ya kubomolewa nyumba walizojenga katika makazi holela.