Na Mwandishi Wetu
Magonjwa yasiyoambukiza (NCDs) yanachangia takribani asilimia 33 ya vifo vyote nchini huku takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), kwa mwaka 2020 zinaonesha kuwa magonjwa hayo yalichangia zaidi ya vifo milioni 41 sawa na asilimia 71 ya vifo vyote Duniani ukilinganisha na vifo milioni 57 kwa mwaka 2016 duniani.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Afya kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Ally Mazrui wakati wa Uzinduzi wa Utafiti wa Kitaifa wa Viashiria vya Magonjwa Yasiyoambukiza (STEPS SURVEY 2023) uliofanyika kwenye ukumbi wa Tawimu Jijini Dodoma.
Mazrui amesema takwimu zinaonesha kuwa magonjwa hayo yameongezeka mara tano hadi tisa zaidi kati ya miaka ya 80 ambapo asimilia moja tu ya watanzania walikuwa na tatizo la kisukari na asilimia tano walikuwa na tatizo la shinikizo la juu la damu wakati kwa sasa tatizo la kisukari limefikia asilimia tisa na tatizo la shinikizo la juu la damu limeongezeka na kufikia asilimia 25.
“Takwimu hizo zote kutoka katika vituo vyetu vya kutolea huduma za afya nchini zinaonesha ongezeko kubwa sana la magonjwa hayo ambapo katika kipindi cha Julai 2022 hadi Machi 2023, magonjwa yasiyoambukiza ambayo yalisababisha wagonjwa wengi kuhudhuria vituo vya huduma za afya ni pamoja na shinikizo la juu la damu wagonjwa 1,456,881 sawa na asilimia 49 ukilinganisha na asilimia 34 kipindi kama hicho mwaka 2021/2022, kisukari wagonjwa 713,057 sawa na asilimia 24, magonjwa ya mfumo wa hewa wagonjwa 386,018 sawa na asilimia 13 ikilinganishwa na asilimia 10 kwa kipindi kama hicho mwaka 2021/2022.
Amesema katika kukabiliana na ongezeko la magonjwa hayo, Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Afya imeendelea kutekeleza mkakati wa Kitaifa wa kukabiliana na magonjwa hayo nchini kwa kutoa elimu kwa jamii kuhusu namna bora ya kujikinga na magonjwa hayo pamoja na kuimarisha mifumo ya utoaji huduma za afya nchini kwa kufikisha huduma za uchunguzi wa awali na matibabu kuanzia ngazi ya afya ya msingi.
“Kufuatia mwenendo na hali ya magonjwa haya nchini, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na WHO inakwenda kufanya utafiti wa Kitaifa utakaobaini hali halisi ya mwenendo wa viashiria hatarishi na magonjwa yasiyoambukiza. Utafiti huu utakuwa ni wa pili baada ya ule wa kwanza uliofanyika mwaka 2011 upande wa Zanzibar na mwaka 2012 kwa upande wa Tanzania Bara”. Aliongeza.
Amesema utafiti huo unatarajiwa kuanza tarehe 14 Agosti,2023 na unatarajia kuifikia mikoa yote Tanzania bara na Zanzibar ukihusisha watu wenye umri kati ya miaka 18 hadi 69 na utafiti huo unapaswa kufanyika kila baada ya miaka minne hadi mitano.
“Utafiti huu ni muhimu sana hasa katika kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza na takwimu hizo za kisayansi zitaonesha juu ya ukubwa wa viashiria vya magonjwa hayo nchini ambavyo vinaweza kutumika katika kuandaa mikakati ya kudhibiti magonjwa hayo nchini” amsisitiza.
Hata hivyo amewakumbusha watafiti wote watakaoshiriki katika zoezi hilo kuhakikisha ubora wa takwimu zitakazokusanywa na kuzingatia maadili wakati wote wa utekelezaji wa utafiti huo.
Naye, Mwakilishi wa Katibu Mkuu ambaye pia ni Mganga Mkuu wa Serikali Prof.Tumaini Nagu amesema nchi inakabiliwa na majanga mawili ya magonjwa ya kuambukiza ikiwemo TB, UKIMWI, Malaria lakini na magonjwa yasiyoambukiza ambapo kwa sasa yamekuwa yakiongezeka kwa kasi na kuongezea mzigo mkubwa wa bajeti ya Serikali hususani Wizara ya Afya na gharama kwa familia.
Amesema,kumekua na vifo vya kabla ya wakati vikitokea ambavyo vinasababishwa na magonjwa yasiyoambukiza na hata ubora wa maisha imepungua kwa kiasi kikubwa kwa sababu ya magonjwa hayo licha ya kuwa na dawa za kutibu magonjwa hayo na ndio maana wanajikita katika utafiti.
“Kipaumbele chetu ni kukinga na kwa wale ambao tayari wamegundulika tunawapa matibabu na ndio maana tumeimarisha mifumo ya utoaji huduma za afya nchini kwa kufikisha huduma za uchunguzi wa awali na matibabu kuanzia ngazi ya afya ya msingi ambapo ugatuzi wa huduma za matibabu na uchunguzi wa awali wa magonjwa haya kufanyika kuanzia ngazi ya vituo vya afya na zahanati” amesema.