Mjadala unaohusu mafuta ya kula ya mawese yanayoingizwa nchini kutoka Indonesia na Malaysia, umechusha.

Kila mwaka kelele kwenye biashara hii imekuwa jambo la kawaida-mvutano ukiwa Serikali kwa upande mmoja dhidi ya wafanyabiashara kwa upande mwingine.

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mara kadhaa imesema mafuta ya mawese yanayoletwa kutoka katika mataifa hayo si ghafi, lakini wafanyabiashara wamekuwa na msimamo tofauti.

Yamekuwapo madai ya muda mrefu kwamba wafanyabiashara wanashirikiana na baadhi ya vyombo vya udhibiti wa vyakula nchini kuihadaa Serikali, na hivyo kuikosesha mabilioni ya shilingi.

Kwa upande wetu tunaona kuwa mvutano wa sasa unapaswa kuwa mwanzo wa mwisho wa malumbano kuhusu bidhaa hii.

Tunasema hivyo kwa sababu ni jambo la ajabu kuona kuwa pamoja na umri wetu mkubwa kama taifa bado tunashindwa kupata uwezo wa kubaini mafuta ghafi na yasiyo ghafi.

Tunaamini uwezo wa kupata ukweli tunao, lakini pengine kinachosababisha malumbano haya ni ukosefu wa uadilifu kwa pande zinazohusika.

Si wajibu wetu kuegemea upande wowote kwenye sakata hili, lakini tunashawishika kuamini kuwa biashara hii imezingirwa na mbinu zisizo wazi, na hivyo kusababisha mvutano usiokuwa na tija kwa walaji.

Serikali ina wajibu wa kuwalinda wafanyabiashara ili walipe ushuru na kodi stahiki. Wafanyabiashara nao wana wajibu wa kulipa kile kinachostahili bila kuleta ujanja ujanja.

Pamoja na ukweli huo, tunaamini njia nzuri ya kuondokana na malumbano haya ni kuhakikisha Watanzania tunazalisha mafuta ya kula ya kutosheleza mahitaji na kuuza ziada nje ya nchi. Indonesia na Malaysia walichukua mbegu za michikichi Kigoma, na leo ndio wasafitrishaji wakuu wa mafuta ya mawese duniani.

Hatuoni ni kitu gani kinachotukwaza kulima zao hili kwa wingi na kuwa na viwanda. Tulumbane kuona mbinu za kutufikisha kwenye hali ya kujitosheleza. Ardhi tunayo ya kutosha, tuna hali ya hewa inayofaa. Kinachokosekana ni dhamira na utashi wa kufikia kiwango cha uzalishaji mkubwa. Tujikwamue kwa kuwa na kilimo na viwanda vyetu wenyewe. Tukiamua tunaweza.