Na Deodatus Balile
Wiki hii nazungumzia tatizo sugu linalolikabili taifa letu katika nishati ya mafuta. Kabla zijaingia undani wa bei za mafuta na suluhisho mujarabu, nizungumzie kwanza kupanda kwa bei za bidhaa na huduma.
Kwa sasa kila mtu anapandisha bei atakavyo kwa kisingizio cha vita ya Urusi na Ukraine. Miche ya sabuni imepanda bei, soda zimepanda bei, mikate na karibu kila kitu isipokuwa mchele na samaki.
Sitanii, kwa sasa samaki wameshuka bei. Ukienda kwenye ubao wa wauza samaki unapimiwa fungu la Sh 1,000 au 2,000 unashangaa. Unajiuliza iwapo muuzaji hapati hasara kwa wingi wa samaki unaopimiwa. Ila jibu nimelipata. Kupanda kwa bei ya mafuta ya kula, kumepunguza idadi ya wachuuzi wanaokaanga samaki kwa kuogopa bei ya mafuta. Hii imeleta neema katika kitoweo.
Ukiacha samaki walioshuka bei jijini Dar es Salaam, vitu vingine vyote ni balaa. Juzi nimekwenda kituo cha mafuta nikatoa Sh 50,000 nijaziwe mafuta, nikapewa lita 17.
Mwaka 2004 kwa gari hili la IST hiyo hiyo Sh 50,000 nilikuwa napata lita 47. Hii ina maana kuwa fedha yetu imepoteza thamani kwa wastani wa lita 30 katika kipindi cha miaka 18. Nimeamua nitumie lita badala ya asilimia, ambazo kwa baadhi inawezekana zisieleweke haraka.
Sitanii, nimesikiliza michango ya wabunge bungeni wiki iliyopita. Kwanza nipongeze na kusema nimepata Uhondo/Oroda kuangalia tena Bunge Live. Tumeukosa uhondo huu kwa miaka sita. Hii haikuwa sahihi na nampongeza Rais Samia Suluhu Hassan kuruhusu kilichozuiwa na mtangulizi wake. Katika kuangalia Bunge Live, nimeona mchango wa Mbunge wa Gairo (CCM), Ahmed Shabiby.
Nimefuatilia michango ya Shabiby bungeni kwa muda mrefu sasa. Mwanzo alikuwa haitaki Mamlaka ya Nishati na Maji (EWURA), ila kwa mchango wake wa wiki iliyopita, nimeona Shabiby amekuwa na mabadiliko kidogo. Kwa sasa amejikita katika hoja ya ushindani wa haki. Chini ya Serikali ya Awamu ya Pili ya Rais Ali Hassan Mwinyi tulianzisha sera ya Soko Huria, ambalo kwa bahati mbaya liligeuka soko holela.
Kwa ndugu zangu ambao tumejaliwa kuishi duniani kwa zaidi ya miaka 50, tutakumbuka miaka ya 1970 na ile ya 1980, nchi yetu ilikuwa na Tume ya Bei. Hadi kiberiti kilipangiwa bei na tume hiyo. Kwa bahati mbaya, hii tume ilijikuta inaingia katika mchezo mchafu. Iliamua kupanga bei bila kujali uhalisia. Gharama za bidhaa ziliongezeka kwa sababu ya mfumo wa ugavi.
Kwa mfano, sukari ilikuwa inazalishwa Kagera Sugar, inalazimika kusafirishwa kwanza hadi Dar es Salaam, inapangiwa bei kisha inasambazwa nchi nzima kwa mgawo, kwa maana ya kusafirishwa tena kwenda Kagera.
Unaweza kufahamu kiwango cha akili iliyokuwa inatumika kibiashara. Yaani sukari inatoka Kagera, inapelekwa Dar es Salaam, halafu baada ya kupitisha mgawo inasafirishwa tena kwenda Kagera. Hizo gharama za usafirishaji ni mzigo usiohimilika.
Sitanii, Mzee Mwinyi na baadaye Rais Benjamin Mkapa waliliona hili. Wakaruhusu soko huria. Kwa bahati mbaya, katika soko huria kanuni za mchezo hazikuwekwa vizuri. Tukajikuta soko letu halina kanuni kama ilivyo kwenye sekta ya mafuta kwa EWURA au kwenye madini kupitia Tume ya Madini. Huko zinatolewa bei elekezi.
Nilisema nimemfuatilia Shabiby kitambo. Mwanzoni alikuwa hataki uwepo wa EWURA ila kwa sasa anautaka. Anaona ni muhimu kuwa na Mdhibiti wa Bei Kikomo kama inavyofanya EWURA kisha wafanyabiashara washindane kupata mafuta ya bei rahisi huko duniani. Nafahamu kuna hoja kwamba hapa nchini yalikuwa yanaletwa mafuta machafu kabla ya kuanza utaratibu wa Ununuzi wa Pamoja (Bulk Procurement).
Nasema hoja ya mafuta machafu ni dhaifu. Tunalo Shirika la Ubora wa Viwango (TBS), ambalo linapaswa kusimamia ubora wa bidhaa. Iwe zimeletwa na mtu mmoja mmoja au kwa pamoja. Mafuta yanapaswa kuingilia eneo moja ambalo ni ama Bandari ya Tanga, Dar es Salaam au Mtwara. Hapa zinapaswa kuwapo mita za ujazo zenye ukubwa sawa na kasi ya upakuaji inayotoka kwenye meli. Akileta mtu mafuta machafu anapigwa faini na yanarudishwa alikoyatoa.
Nafahamu miundombinu pale bandarini bado haina uwezo stahiki. Shabiby amesema mita ‘zinaharibika’. Meli moja ya mafuta inashusha mafuta kwa siku 8 hadi 10. Hili ni tatizo. Inaongeza gharama pia. Tunapaswa kupanua miundombinu. Meli ipakue lita tani 120 sawa na lita milioni 144 hivi kwa siku moja au nusu siku. Msomaji, mafuta ni mepesi kuliko maji, hivyo usitumie kiwango cha lita 1,000 kuwa tani moja. Ndiyo maana mafuta yanaelea juu ya maji. Tani moja ya mafuta ni wastani wa lita 1,200.
Sitanii, ukurasa umekuwa finyu. Hili la miundombinu nitalidadavua zaidi wiki ijayo. Tunatumia wastani wa Sh trilioni 7, kuagiza mafuta kutoka nje ya nchi kwa mwaka. Tunaweza kuachana na utumwa huu tukipenda. Tunayo neema katika nchi yetu. Wakati Waarabu wanayo mafuta, sisi hapa kwetu tuna gesi kwa viwango vya Trillion Cubic Feet (TCF) 57 iliyogunduliwa, na bado ipo nyingi haijagunduliwa. Hiki ni kiwango tunachoweza kuchimba kwa hadi miaka 600 ijayo. Je, unafahamu kuwa malori ya Dangote zaidi ya 1,000 yote yanatumia gesi badala ya mafuta? Je, Tanzania hatuwezi kwenda huko? Usikose makala ya wiki ijayo.