Wadau wa mchakato wa kuagiza mafuta wamekubaliana kupunguza kasi ya uingizaji wa mafuta kwa mwezi Aprili kama njia ya kukabiliana na mrundikano wa bidhaa hiyo.
Makubaliano hayo yanatokana na ombi la Umoja wa Kampuni za Biashara ya Mafuta (TAOMAC) kutaka meli zilizopangwa kuleta mafuta kwa mwezi Aprili zicheleweshwe kwa wiki mbili.
Katika barua hiyo ya Machi 4, 2020 yenye kumbukumbu namba PBPA/OP/2929/2 ambayo JAMHURI imeiona, TAOMAC imeeleza kuwa wamelazimika kuomba ucheleweshwaji huo kutokana na biashara ya mafuta ulimwenguni kuathirika kutokana na kuibuka kwa virusi vya corona.
Aidha, wafanyabiashara hao wanabainisha kuwa hapa nchini biashara hiyo imeathirika zaidi kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha sehemu mbalimbali zilizosababisha kuharibika kwa miundombinu, hivyo kutatiza usambazaji wa mafuta.
“Kuibuka kwa virusi vya corona kumesababisha matatizo makubwa kwenye biashara ya usambazaji wa bidhaa za petroli duniani kote hivi sasa. Uchumi wa China umeathiriwa sana na madhara ya corona na matokeo yake matumizi ya mafuta yameshuka kwa kiasi kikubwa,” inasomeka sehemu ya barua hiyo iliyosainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TAOMAC, Raphael Mgaya.
Kwa hapa nchini, TAOMAC inasema katika barua hiyo kuwa usambazaji wa mafuta umeathiriwa kwa kiasi kikubwa na sababu mbili.
Mosi, mvua zinazoendelea kunyesha zimesababisha mafuriko na uharibifu wa miundombinu, hivyo kukwamisha usambazaji wa biadhaa za mafuta.
Pili, TAOMAC inasema Zambia, ambayo ni moja ya nchi zinazochukua mafuta kwa wingi nchini, siku za hivi karibuni imeanza kununua mafuta ya bei rahisi kutoka Beira, Msumbiji.
“Hii imeathiri biashara ya mafuta yanayopitia nchini na baadhi ya bidhaa ambazo awali ziliagizwa kwa ajili ya nchi nyingine zimeanza kutumika nchini, hivyo kufanya kuwe na akiba kubwa kuliko mahitaji,” inasomeka barua hiyo.
Kwa mujibu wa Mgaya, Bodi ya Utawala ya TAOMAC ilikutana Machi 4, mwaka huu katika kikao cha dharura na kukubaliana kuomba ucheleweshwaji wa meli zitakazoleta mafuta mwezi Aprili kama njia ya kukabiliana na hali hiyo.
Kikao hicho cha Bodi ya TAOMAC kilihudhuriwa na wawakilishi wa kampuni za Oryx, Petrofuel, MOIL, TOTAL, AUGUSTA, PUMA na PetroAfrica.
Akizungumza na JAMHURI mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA), Erasto Mulokozi, amesema ni kweli TAOMAC walipeleka maombi hayo ambayo yamekwisha kupatiwa ufumbuzi.
Akifafanua, Mulokozi anasema wamekubaliana kuchelewesha meli zitakazoleta mafuta kwa ajili ya mwezi Aprili si kwa wiki mbili kama TAOMAC walivyoomba, bali kwa muda tofauti kulingana na mikataba ya waleta mafuta.
“Hatukuchelewesha meli kwa wiki mbili kama walivyoomba, zipo meli zitachelewa kwa wiki moja, nyingine siku tano na zipo zitakazochelewa kwa siku tatu… hii ni kulingana na mikataba na waleta mafuta hao,” anasema Mulokozi.
Anasema hilo limefanyika baada ya kukubaliana na waleta mafuta kulingana na mikataba waliyonayo. Anasema kuwa kwa mujibu wa mikataba hiyo, PBPA inapaswa kuwasiliana na waleta mafuta katika kipindi kisichopungua siku 30 iwapo kuna mabadiliko yoyote katika ratiba ya uletaji mafuta nchini.
Amebainisha kuwa walikubaliana na ombi la TAOMAC baada ya wao kufanya hesabu na kubaini kuwa ni kweli kuna shehena kubwa ya mafuta kwenye hifadhi.
“Tukaona si vema kuendelea kuleta meli wakati bado tuna hifadhi kubwa. Ukileta meli kama hakuna nafasi ya kuyaweka hayo mafuta ina maana meli italazimika kusubiri kwa muda mrefu kabla ya kushusha shehena na hiyo ni gharama kubwa,” anasema.
Akifafanua, Mulokozi anabainisha kuwa meli moja yenye ujazo wa lita 40,000 za petroli hulipiwa dola 20,000 za Marekani kwa kila siku itakayokaa ikisubiri kushusha shehena wakati meli ya ujazo wa lita 100,000 za dizeli hulipiwa dola 25,000 za Marekani kwa siku moja.
Kuhusu uwezekano wa TAOMAC kuomba ucheleweshaji huo kama njia ya kuhakikisha bei ya mafuta haiporomoki kutokana na kuwepo kwa bidhaa hiyo kwa wingi nchini, Mulokozi anasema hilo haliwezekani kwa sababu upangaji wa bei hufanywa na taasisi nyingine.
“Kila mwezi EWURA (Mamlaka ya Nishati na Maji) ndiyo inatoa bei elekezi na bei hiyo hukokotolewa kwa kuzingatia vitu vingi, ikiwemo bei ya manunuzi kwenye refinery (viwanda vya kusafisha mafuta), gharama za usafirishaji na kodi za serikali. Kwa hiyo TAOMAC wala haiwezi ku-influence (kushawishi) upangaji wa bei,” anafafanua Mulokozi.
Kwa kawaida Tanzania huagiza kati ya tani 250,000 na 450,000 za mafuta kwa mwezi kulingana na mahitaji.
Uwezo wa kuhifadhi mafuta nchini ni lita bilioni 1.1 katika hifadhi zilizopo Dar es Salaam, Tanga na Mtwara. Hifadhi hiyo inahusisha mafuta yanayotumika nchini na yale yanayopita kwenda nchi jirani.
Akizungumza jijini Dar es Salaam mwezi uliopita, Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani, alibainisha kuwa hali ya mafuta nchini hivi sasa ni nzuri.