Mkuu wa Wilaya ya Mafia Mhandisi Martin Ntemo ameongoza wananchi kuamua kuadhimisha sherehe za miaka 61 ya Uhuru wa Tanzania Bara kwa kupanda miti na kushiriki kwenye Kongamano ambalo lilikuwa maalum kujadili changamoto mbali mbali zinazowakabili walimu wanawake pindi wanapotekeleza majukumu yao.
Mkuu huyo wa Wilaya amesema kwamba Kongamano hilo limefanyikia katika ukumbi wal CARITAS na kuratibiwa na Shirika lisilo la Kiserikali la Action Aid ambapo pia kulifanyika zoezi la kupanda miti katika eneo kinapojengwa Chuo cha VETA.
Amesema kuwa katika zoezi la upandaji miti lilihitimishwa katika eneo inapojengwa Shule mpya ya Sekondari katika Kata ya Ndagoni kisiwani Mafia lengo ikiwa ni kuboresha mazingira katika shule hiyo.
Akizungumza katika kongamano hili mkuu huyo wa Wilaya alieleza kuwa ratiba hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa mikoa na wilaya zote kuadhimisha sherehe za miaka 61 ya Uhuru wa Tanzania Bara kwa kuandaa makongamano.
“Tumepokea maagizo ya Rais wetu ya kuadhimisha sherehe za miaka 61 ya uhuru katika kuandaa makongamano lakini pia kushiriki katika shughuli mbali mbali za kijamii na sisi katika Wilaya ya mafia tumetekeleza hilo,”amesema Ntemo.
Akifafanua zàidi amesema kwamba ratiba hiyo ya kuadhimisha miaka 61 ya Uhuru wa Tanzania Bara itaendelea kwa mashindano ya mashule kwa upande wa mashairi na ngonjera lakini pia itahusisha mashindano ya michezo mbali mbali kabla ya siku ya kilele ambayo ni tarehe 9 Desemba mwaka huu.
Katika hatua nyingine alibainishwa kutakuwa na mkutano mkubwa wa hadhara katika viwanja vya Mkunguni kwa ajili ya kukutana na wananchi,wadau wa maendeleo ili kujadili mambo mbali mbali.