Na Padre Dk Faustin Kamugisha
 
Nia ni sababu ya mafanikio. Penye nia pana njia. Mtazamo wa “lazima nifanye kitu,” unatatua matatizo mengi kuliko mtazamo wa “kitu fulani lazima kifanyike.” Mtazamo wa kwanza una nguvu ya nia. “Nia yetu inaumba uhalisia wetu,” aliandika Wayner Dyer katika kitabu chake The Power of Intention.
Yote ambayo umeyafanya kuna wakati uliyanuia. Mambo mengi yanayoonekana ni watoto wa nia. “Kabla hujatoka kwenye nyumba leo ulikuwa na nia ya kuvaa nguo na ulizivaa. Hukujaribu kuvaa nguo za ndani bali ulizivaa.
“Zoezi hilo halina budi kufanyika kwa yote tunayonuia. Hatujaribu kuwa wenzi wenye upendo. Tunanuia na tunaweka katika matendo,” alisema Patch Adams. Ukinuia kufanya jambo zuri lifanye, kama ambavyo unanuia kuvaa nguo na unavaa nguo kweli.
 
Gilbert Becker alikuwa askari mpenda Mungu ambaye siku moja alienda kuhiji nchi takatifu. Alikamatwa na kufanywa mfungwa wakati wa vita na bwana mmoja katika nchi takatifu. Huyu bwana alikuwa na binti mrembo ambaye alimpenda Gilbert na kumsaidia kutoroka na kurudi London.
Hakumsahau Gilbert. Siku moja alitoka nyumbani na kuelekea London kumtafuta Gilbert. Alikuwa mgeni jijini London hakuweza kuzungumza hata neno moja la Kiingereza. Licha ya hilo hakuwa na anwani ya Gilbert.
Akiwa amenuia, alizunguka mitaa akiita: Gilbert, Gilbert, Gilbert. Siku na miezi ilipita hakupata matokeo mazuri. Polepole neno lilienea jiji zima na kumfikia Gilbert. Baada ya kusikia jambo hili Gilbert aliguswa na upendo wake kwake na kumuoa. Hapa tunaona nguvu ya nia na uvumilivu.
 
“Ukitaka kufanikiwa ufanye uvumilivu mwandani wako, uzoefu mshauri wako, tahadhari kaka yako mkubwa na matumaini malaika wako mlinzi,” alisema Joseph Addison.  Nguvu ya nia inapaliliwa na uvumilivu. Nguvu ya nia inaboreshwa na tahadhari.
Nguvu ya nia inapewa nguvu na matumaini. Nguvu ya nia ikuletee matunda mazuri lazima uwe kwenye njia sahihi. Nia njema haitakusaidia kwenye njia yako kama hauko kwenye njia sahihi. Pia nguvu ya nia inasaidiwa na kuthubutu.
“Si kwamba mambo ni magumu ndio maana hatuthubutu kufanya kitu. Ni kwa sababu hatuthubutu kufanya kitu ndio maana mambo ni magumu,” alisema mwanafalsafa wa Kirumi Seneca.
Kutothubutu au kutojaribu ni kosa. Kwa kujaribu mara nyingi, tumbili hujifunza kuruka kutoka mtini. “Binadamu hawezi kuvumbua bahari mpya kama hana ujasiri wa kupoteza kule kuona ufukwe,” alisema Andre Gide (1869-1951) Mfaransa mwandishi na  mshindi wa zawadi ya Nobel katika fasihi mwaka 1947.
Ili kuvumbua bahari mpya lazima uende mbali lazima ufanye kitu. Nguvu ya nia inapewa msukumo na kupiga picha akilini. Ukianza kuamini unalonuia kulifanya utaanza kuliona.
 
Hoja si bora nia, bali nia njema. “Nia njema ilivyo kwa matendo ni kama roho ilivyo kwa mwili, au mizizi ilivyo kwa mti,” alisema Jeremy Taylor. Nia njema ni mzizi wa mafanikio. Nia njema ni roho ya mafanikio. Usafi wa nia ni jambo muhimu. Kumbuka nia ni kusudio la kufanya jambo. Ni lengo, ni dhamira, ni tarajio. Dhimira hii na iwe safi. Lengo hili na liwe safi.
“Tendo dogo sana ni zuri zaidi kuliko nia kubwa sana,” alisema Roger Nash Baldwin. Si vizuri kupanga tu lazima kutekeleza. Si vizuri kuota ndoto za maendeleo tu lazima kuziwekea msingi. Bwana Nilitaka Kufanya ana rafiki yake anaitwa Bwana Sikufanya. Je, uliwahi kukutana nao? Je, waliwahi kukuita au kukualika?
Hawa jamaa wawili wanaishi nyumba moja inayoitwa ‘Hufanikiwi Kamwe’. Hawa wanasumbuliwa na mzimu wa unaoitwa ‘Mambo Yangekuwa’. Kama tuvitegemeavyo vingegeuka na kuwa farasi hata maskini wangepanda farasi.
Haitoshi kunuia, tenda. Haitoshi kuwa na nia piga hatua ya kwanza. “Hakuna uchache wa fursa wa kujipatia riziki kutokana na lile unalolipenda. Kuna uchache wa uamuzi wa kufanya mambo yawe,” alisema Wayne Dyer. Amua nia yako kuifanyia kazi. Amua leo, usingoje kesho.