Padre Dk Faustin Kamugisha

Kushindwa ni sababu ya mafanikio ilmradi kusiwe desturi. Bill Gates, tajiri mkubwa duniani, amesema, “Ni vizuri kusherehekea mafanikio, lakini ni muhimu kujifunza masomo unayopewa na kushindwa.”

Kushindwa huwafanya baadhi ya watu kuvunjika moyo na wengine kuvunja rekodi baadaye. Ndugu msomaji, umeshindwa mara nyingi ingawa huwezi kukumbuka. Ulishindwa mara ya kwanza ulipojaribu kusimama. Ulishindwa mara ya kwanza ulipojaribu kutembea. Ulishindwa kwa mara ya kwanza ulipojaribu kuogolea.

Mwandishi wa riwaya za Kiingereza, John Creasey, amepata barua za kukataa maandishi yake mara 753 kabla ya kuchapisha vitabu vyake 564.

Kukosa njia ni kujua njia. “Hakuna ulinganisho kati ya kilichopotea kwa kutofanikiwa na kilichopotea kwa kutokujaribu,” amesema Francis Bacon. Ukishindwa jaribu tena. Kushindwa ni fursa ya kujipanga tena. Ukijifunza kutoka katika kushindwa hujashindwa.

Kushindwa ni sehemu ya njia ya kushinda. “Mtu yeyote ambaye hajawahi kushindwa hajajaribu kufanya jambo jipya,” amesema Albert Einstein.

Mwanasayansi Thomas Edison baada ya kufanya majaribio 10,000 na kushindwa amesema: “Sikushindwa, ila nimegundua mambo 10,000 ambayo hayawezi kufanya kazi.” Huyu alifanikiwa kama mwanasayansi na kuwa na hatimilki ya vitu zaidi ya 1,000 katika uwanja wa sayansi.

Kipimo cha mafanikio cha mtu ni vikwazo alivyoweza kuvuka akijaribu kufanikiwa. Booker T. Washington alikuwa na haya ya kusema juu ya hilo. “Nimejifunza ya  kuwa mafanikio hayapimwi sana na nafasi aliyoifikia mtu katika maisha, bali vikwazo alivyoweza kushinda akijaribu kufaulu”.

Kukosa njia ni kujua njia. Vikwazo na kushindwa hapa na pale visikukatishe tamaa. Kushindwa ni hatua ya kwanza ya kufanikiwa.  “Tofauti kati ya mtu aliyeshindwa au aliyefanikiwa na aliyeshindwa mara nyingi imejikita katika ukweli kuwa mtu aliyefanikiwa, atafaidi zaidi kutokana na makosa yake  na kujaribu tena njia nyingine,”  amesema Dale Carnegie.

Biblia inatualika kuinuka tukianguka, kujaribu tena tukishindwa: “Wewe Yeremia utawaambia kuwa mimi Mwenyezi Mungu nasema hivi: Mtu akianguka, je, hainuki tena? Mtu akipotea, je, hairudii tena njia yake? (Yeremia 8:4).

Kuna askari aliyetoroka kwenye uwanja wa mapambano baada ya kuona kikosi chake kinaelekea kushindwa. Akiwa amejificha kwenye pango, aliona sisimizi anapanda kwenye jiwe anavuta chakula. Alidondoka mara tisa. Mara ya 10 alifanikiwa. Askari alivyoona sisimizi aliyeshindwa mara tisa lakini mara ya 10 alifanikiwa, alitoka kwenye pango na kurudi kwenye uwanja wa mapambano.

Kushindwa ni tukio na siyo mtu, jana ilimalizika usiku,” amesema Zig Ziglar. Wewe huitwi kushindwa. Kushindwa si jina la mtu.  Kama ulishindwa jana, jana ilipita. Leo ni kesho ya jana. Usikubali mafanikio yajae kichwani mwako utakuwa na majivuno. Usikubali kushindwa kujae moyoni mwako, utakata tamaa.  

Katika kujaribu kufanikiwa usiwe na visingizio vyovyote. Tuna ushahidi kutoka vitabu vitakatifu. Nilipokea ujumbe kwenye simu uliokuwa na maneno haya: “Mungu haangalii kwamba zamani ulishindwa, ndiyo maana alimbariki Saulo akamfanya Paulo, alimbariki Simoni akawa Petro.

Mungu haangalii uzoefu wako ndiyo maana alimbariki Daudi kuwa mfalme akiwa kijana mdogo. Mungu haangalii jinsia au jinsi yako ndiyo maana alimbariki Esther. Mungu haangalii mwonekano wa umbo ndiyo maana alimbariki Zakayo mfupi sana wa kimo.

Mungu haangalii ufundi wako wa kuongea, ndiyo maana alimbariki Musa mwenye kigugumizi. Mungu haangalii shughuli yako, ndiyo maana alimbariki Maria Magdalena aliyekuwa na shughuli pevu. Mungu hana mdhambi ambaye hawezi kumsamehe. Hawezi kusikiliza sala ambayo hawezi kujibu. Hawezi kufanya ahadi ambayo hatatimiza.”