Padre Dk Faustin Kamugisha
Kuwajali wateja ni sababu ya mafanikio. Mteja ni kama damu muhimu kwa uhai wa biashara
yako au shughuli yako. Kanuni ya msingi kwa yeyote anayehudumia mteja ni mteja kwanza.
Mteja ni mfalme. Inaweza kukuchukua miezi kumpata mteja na sekunde moja kumpoteza.
Usipowajali wateja wako, mtu mwingine atawajali.
Yatafakari maneno ya Mahatma Gandhi: “Mteja ni mgeni muhimu sana katika maeneo yetu,
hatutegemei sisi. Tunamtegemea. Si katizo la kazi yetu. Ni lengo la kazi. Si mtu wa nje katika
shughuli zetu. Ni sehemu ya shughuli. Hatumpendelei kwa kumhudumia. Anatupendelea kwa
kutupa fursa ya kumtendea hivyo.”
Mteja kama mgeni muhimu, anatukumbusha msemo wa Kiswahili: karibu mgeni mwenyeji
apone. Mtu wa namna hiyo mpokee kwa mikono miwili.
Mteja ni lengo la kazi. Siku moja niliingia kwenye hoteli ndogo Dar es Salaam kununua chai.
Mhudumu niliyemkuta alikuwa anaongea na simu. Nilingoja amalize. Niliomba nipewe chai.
Aliniambia kuwa chai imekwisha. Aliendelea kupiga simu. Nilimgonja amalize.
Nilimwambia: “Dada haichukui muda kutengeneza chai. Ukichemsha maji. Majani ya chai na
sukari nitajiwekea. Lakini hata hivyo ni saa sita naona chakula tayari, ungenipa uwezekano
mwingine na kuniambia chakula tayari.” Ni kama nilikatisha shughuli yake ya kuzungumza na
simu. Alisahau kuwa mimi kama mteja nilikuwa lengo la kazi yake.
Mpe mteja wako huduma bora na si bora huduma. “Si kazi ya wateja wako kukumbuka, ni
wajibu wako na kazi yako kuhakikisha hawana nafasi ya kukusahau,” alisema Patricia Frippo,
mtaalamu wa kutoa hotuba za utangulizi.
Huduma kwa wateja isiwe nzuri sana tu, bali iwe gumzo kwa ubora wake. Huduma kwa wateja
ni zaidi ya kitengo, ni kuwa na mtazamo chanya. Kuna kaulimbiu ya familia moja isemayo:
“Ubora unakumbukwa kwa muda mrefu baada ya bei kusahulika.”
Mteja anapoingia mkaribishe. Mpokee kwa uso wa tabasamu. Kuna methali ya Kichina
isemayo: “Mtu asiye na uso wa tabasamu asifungue duka.” Mpokee kama unavyoweza
kumpokea mgeni rasmi kwenye sherehe. “Tunawaona wateja wetu kama wageni waalikwa
kwenye sherehe, na sisi ni wenyeji wa sherehe. Ni kazi yetu kufanya uzoefu huo uwe mzuri
zaidi kidogo,” amesema Jeff Bezos, mwanzilishi wa Amazon.
Nakubaliana na maneno ya Seth Godin aliyesema: “Watu hawanunui bidhaa na huduma.
Wananunua mahusiano, hadithi…” Kumuona mteja kama mfalme ni jambo muhimu. “Wakaribie
sana wateja wako kwa namna ambavyo hujawahi kuwakaribia. Kuwa karibu sana kiasi cha
kuwaambia wanachohitaji kabla ya wao kugundua,” alisema Steve Jobs. Ni vizuri kuwa na
mahusiano mazuri na mteja.
Mtendee kila mteja kama kwamba ni mteja peke yake duniani. Zungumza na moyo wake na si
kichwa chake tu. “Ukizungumza tu na vichwa vya watu na si na mioyo yao hawatakusikiliza,”
alisema Les Brown, mtunzi na mratibishaji semina za kutia moyo.
Kuna mteja aliyeenda kununua viatu kwenye duka la viatu; bahati mbaya namba yake
haikuwapo mguu wake ulikuwa mkubwa sana. Muuza viatu baada ya kuona mguu wake
alimwambia: “Viatu vyetu ni vidogo.” Hakusema: “Mguu wako ni mkubwa.” Hakushambulia
mguu wa mteja bali viatu.
Namna hiyo unagusa kwa namna nzuri moyo wa mtu. Methali ya Kijapani inasema yote: “Neno
moja zuri linaweza kupasha joto miezi mitatu ya baridi.”
Mtendee mteja kwa heshima. “Kumtendea kwa heshima mteja kutamfanya awe tangazo la
biashara linalotembea,” alisema James Cash Penney, mwanzilishi wa J.C. Penney Stores.
Mfanye mteja awe na furaha.
Nakubaliana na Derek Sivers, mwanzilishi wa CD Baby, aliyesema: “Jambo moja muhimu sana

ni kuwafanya watu wawe na furaha. Kama unawafanya watu wawe na furaha, matokeo yake
watakuwa na furaha kufungua pochi zao na kukulipa.”
Mfanye mteja ajisikie kuwa yeye ni mtu muhimu. Wateja wako kama wanabaki wale wale na
wanazeeka na wewe ni hatari sana. Ongeza wateja, tafuta wateja wapya ukihakikisha
huwapotezi wateja wako wa zamani.