Na Padre Dk. Faustin Kamugisha
Kujua unachokitaka ni siri ya mafanikio. “Kama unataka kufanikiwa maishani, lazima ujue unachokitaka,” amesema Fabienne Frederickson.
Amua unataka nini? Kama unataka kuishi bila kujutia, tafuta unachokitaka ili mradi ni kizuri na ni halali.
“Kama unataka kuwa mpishi mkuu aliyebobea katika upishi, lazima ufanye na wapishi wakuu waliobobea. Hicho ndicho kitu nilichofanya,” amesema Gordon Ramsay.
Ukishajua unachokitaka maishani basi kuwa na shauku ya kukipata. Aliko Dangote tajiri mkubwa sana Afrika amesema: “Shauku ndiyo inayonisukuma mbele. Shauku ndiyo inayonifanya nilale saa nane usiku na kuamka saa kumi na mbili asubuhi.”
Tajiri huyu mwenye kampuni inayoitwa Dangote Group anajua anachokitaka. Amesema: “Baada ya kifo changu, nataka nikumbukwe kama mmiliki mkubwa sana wa viwanda Afrika.”
Huyu ni tajiri ambaye utajiri wake unakisiwa kuzidi dola bilioni 16.7. Namna gani unapata unachokitaka?
Hatua ya kwanza ya kupata unachokitaka maishani ni kuamua unataka nini. Kama haupiganii unachokitaka usililie ulichokipoteza.
“Kuchagua ni bawaba ya hatma,” amesema Edwin Markham. Maisha yanahusu kuchagua. Unapoamka unachagua nguo ipi uvae.
Pili, unahitaji ujisiri. “Maisha yanatanuka au kusinyaa kuwiana na ujasiri wa mtu,” amesema Anaïs Nin.
Tatu, Ili kupata unachokitaka lazima uwasaidie wegine wapate nao wanachokitaka. “Utapata kile unachohitaji kama utawasaidia watu wa kutosha kupata kile wanachokitaka,” amesema Zig Ziglar.
Nne, anza na kitu kidogo. “Kuanza biashara yenye mafanikio, lazima anza na biashara ndogo na ota ndoto kubwa,” amesema Aliko Dangote.
Usichelewe wazo lako lifanyie kazi lisije likaota mbawa. “Wekeza sasa kabla haujachelewa. Treni ipo karibu kuondoka toka kituoni,” amesema Dangote.
Lazima kutamani unachokitaka. “Saizi ya mafanikio yako inapimwa na nguvu ya matamanio yako; saizi ya ndoto yako; na namna unavyoshughulikia mambo ya kukatisha tamaa njiani,” amesema Robert Kiyosaki.
Mwandishi huyu wa vitabu vya mafanikio katika maisha anaona mtu anayewezesha kukwamisha ni wewe mwenyewe.
“Mara nyingi utagundua si mama au baba au mke au watoto wako ambao wanakuzuia. Jipishe,” amesema Robert Kiyosaki.
Anapendekeza usiwe na hofu ya kuwa tofauti. “Hofu ya kuwa tofauti inawazuia watu wengi kutofauta njia mpya ya kutatua matatizo yao.”
Charles Shultz, mchoraji katuni alimchora Lucy akimwambia Charlie Brown: “Maisha ni kama viti vya kwenye deki ya meli ya kuvinjari.”
Charlie Brown ameuliza: Kama nini? Lucy alimjibu: “Haujasafiri kwenye meli ya kuvinjari Charlie Brown?
Abiria hufungua viti vya turabai ili waweze kuota jua. Baadhi ya watu huweka viti vyao wakitazama nyuma ya meli ili waone wanapotoka.
Wengine viti vyao hutazama mbele wanapoelekea. Wanataka kuona wanapoelekea. Kwenye meli ya kuvinjari ya maisha, Charlie Brown, kiti chako kinatazama wapi?”
Charlie Brown alifikiri kwa muda na kusema: “Ee, sijafungua kamwe kiti chochote acha kuzungumza juu ya kinapotazama.” Charlie Brown hakujua anataka nini maishani.
Unataka nini maishani? Unachukua hatua zipi kupata unachokitaka maishani? Katuni juu ya Lucy na Charlie Brown inakufundisha nini?
Bilionea Mark Cuban aliyehitimu masomo ya Chuo Kikuu akiwa na umri wa miaka 25 aliandika hivi katika kitabu chake How to Win at the Sport of Business:
“Nilizoea kuendesha gari nikizunguka (Dallas), nikitazama nyumba kubwa na kupiga picha namna mambo yanavyoweza kuwa kwa kuishi pale na nilitumia picha hii kama motisha.”
Si kwamba mambo yalikuwa rahisi kwa tajiri huyu. Kuna wakati alikuwa analala kwenye sakafu kabla ya mambo kuchanganya vizuri.
“Unaweza kuwa na kitu chochote unachotaka lakini huwezi na kuwa na kila kitu unachotaka,” amesema Peter McWilliams.
Ingawa ni ukweli kuwa huwezi kupata kila kitu unachotaka unaweza kupata kile unachohitaji.