Padre Dk Faustin Kamugisha

Kutoa ni sababu ya mafanikio. Mtu anaweza kufilisika si kwa sababu anatoa bali kwa sababu hatoi. Asiyepoteza haokoti. Kwamba kutoa ni sababu ya mafanikio, jambo hili limethibitishwa na watu wengi.

“Mtu mwenye busara haweki hazina kwa ajili yake. Anavyotoa zaidi kwa wengine, ndivyo anapata zaidi sana,” alisema Lao-tzu mwanafalsafa wa China. Mawazo hayo yanafanana na ya Anne Sophie Swetchine (1782 – 1857) aliyesema: “Tuko matajiri kupitia tu tunachokitoa.”

Mama huyu alizaliwa Moscow alikuwa na mafanikio katika shughuli za Saloni huko Paris. Ukweli ni kuwa tunazidisha kwa kugawana.  Leonard Nimoy (1931 – 2015 mwigizaji wa Marekani) alisema, “Muujiza ni huu: tunavyogawana zaidi tunakuwa na zaidi.”

“Binadamu ni kama shimo: kadiri unavyochukua zaidi kutoka kwake ndivyo anavyopata kuwa mkubwa. Ukubwa upo katika msingi wa kutoa, si kupata,” alisema Richard C. Jalverson (1916 – 1995 mwandishi wa vitabu wa Marekani).

 John D. Rockfeller (1839 – 1937 mfanyabiashara  wa Marekani aliyefanikiwa katika sekta ya mafuta) akiwa na umri wa miaka thelathini na tatu alikuwa tayari amejipatia dola milioni moja, kadiri ya Dale Carnegie  katika kitabu chake- How to Stop Worrying and Start Living.

Akiwa na umri wa miaka 43 alikuwa na Kampuni kubwa ya mafuta -Standard Oil Company. Alipokuwa na miaka 53 alikuwa wapi? Alidhoofishwa na hofu.Alipatwa na ugonjwa uliofyeka nywele zake.

Alilazimishwa kuishi kwa kunywa maziwa kidogo. Katika umri huo alionekana mzee sana sababu ya kazi zisizoisha, hofu isiyo na kikomo, siku nyingi za kulala bila usingizi na kukosa mazoezi.

Alikuwa tajiri sana duniani lakini aliishi kwa mlo ambao hata maskini angedharau kuuchukua. Ngozi yake ilipoteza rangi yake. Matibabu ya hali ya juu yalichelewesha kifo chake.

Alipopata faida alicheza dansi ya kivita na alipopata hasara alikuwa kama mgonjwa, alienda kitandani kulala. Mambo yaliyomdhoofisha yalikuwa hofu, uchoyo na wasiwasi.

Baadaye madaktari walimshauri kutokuwa na hofu, kupumzika, kuwa makini na anachokula na kufanya mazoezi. Lakini alifanya jambo la zaidi. Aliacha kufikiria sana kiasi cha pesa cha kupata na kuanza kufikiria kiasi cha pesa cha kutoa na  kusaidia watu.

Alitoa mamilioni ya hela. Alianzisha taasisi iliyoitwa Rockfeller Foundation ambayo ilipigana dhidi ya maradhi na ujinga duniani kote. Alisaidia tafiti mbalimbali zilizopelekea kwenye vumbuzi mbalimbali kama muujiza wa penicillin.

Baada ya kuanza kutoa alibadilika kabisa. Alipata   amani ya moyoni. Ingawa alichungulia kaburi akiwa na umri wa miaka 53 baada ya kubadili mtazamo na kuanza kutoa aliishi na kufikia umri wa miaka 98.

Tuna mikono miwili: mmoja kwa ajili ya kutoa na mwingine kwa ajili ya kupokea. Lakini tunapokea zaidi kuliko tunachotoa. Ulivyonavyo kama havitoshi, toa.  Ukimpa Mungu kwa mkono wako anakurudishia kwa mkono wake.

Martin Luther alisema: “Nimeshikilia mambo mengi mikononi mwangu, na nimeyapoteza yote; lakini kila kitu ambacho nimeweka mikononi mwa Mungu, bado nakimiliki.” Winston Churchill alisema: “Tunatengeneza riziki kwa kile tunachopata, lakini tunatengeneza maisha kwa kile tunachotoa.”

Charles H. Spurgeon alipendekeza: “Wahisi wengine katika mfuko wako.”

Kutoa ni sababu ya mafanikio. Methali nyingi zinabainisha ukweli huu.

“Kutoa vingi sana kwa masikini kunajaza ghala lako.” Ni methali ya waingereza.  “Asiyepoteza haokoti – atanaga taronda” (Ni methali ya Wahaya).

“Watu wengi hutazama kwa jicho moja kwa wanachokitoa na kwa macho saba kwa wanachopokea,” ndivyo isemavyo methali ya Kijerumani.

Ina maana watu wengi wanatilia mkazo wapokeacho kuliko watoacho.  “Afadhali kutoa kidogo kuliko kumnyima mtu-Kake Ntaimire.” Ni methali ya Wahaya.

Wazo kwamba utakachotoa ni kidogo ni adui wa ukarimu. “Sisi wenyewe tunahisi kuwa tunachofanya ni tone katika bahari. Lakini bahari itakuwa inapungukiwa kwa kukosa tone hilo,” alisema Mama Teresa wa Calcutta. Pia mama huyo alisema, “Kama hauwezi kulisha watu mia moja, basi lisha mmoja.”