Padre Dk. Faustin Kamugisha
Mafanikio yoyote yanahitaji watu. Yanahitaji rasilimali watu. Ndege kiota, buibui, utando, binadamu, mahusiano. Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alipotaja mambo muhimu ili tuendelee, alianza kutaja watu.
Ili kutimiza ndoto ya mafanikio unahitaji watu. Unahitaji watu wa aina mbalimbali: mbunifu, mwombezi, mshauri, mwanamtandao, msherehekeaji, mfadhili, mtia moyo, mtetezi, mfariji, muona mbali, mpendekezaji, mtabiri mzuri, mwenye maono, mratibishaji na mpangaji.
Ili ufanikiwe usiwaonee wivu watu waliofanikiwa. “Ukiwaonea wivu watu waliofanikiwa, unatengeneza eneo la nguvu hasi ya mvuto ambayo inakuweka mbali na kufanya vitu ambavyo unahitajiwa kufanya ili kufanikiwa…”
“Ukiwastaajabia watu waliofanikiwa, unatengeneza eneo la nguvu chanya ya mvuto ambayo inakuvuta kuwa zaidi na zaidi kama watu ambao unataka kufanana,” amesema Brian Tracy.
Unapowainua watu wengine na wewe unainuliwa. Unapotaka kufanikiwa usizungumze vibaya juu ya waliofanikiwa. Unapotaka kuwa na fedha, usizungumze vibaya juu ya fedha. Fedha kwa yenyewe si mbaya. Hoja ni namna unavyoipata na unavyoitumia.
“Kuwavuta watu wenye mvuto, lazima uwe na mvuto. Kuwavuta watu wenye nguvu, lazima uwe na nguvu. Kuwavuta watu wenye kuwajibika, lazima uwe mtu wa kuwajibika. Badala ya kwenda kuwafanyia kazi, unaenda kujifanyia kazi. Ukifanya hivyo, unaweza kuwavuta,” amesema Jim Rohn. Jambo tunalojifunza hapa ni kuwa unahitaji watu.
Kuna hadithi juu ya ndege ambaye alikuwa anajaribu kuruka majira ya baridi kwenda sehemu yenye joto. Alipokuwa njiani akakumbana na tufani ya theluji. Alikuwa na baridi akadondoka kwenye shamba.
Alikuwa karibu afe sababu ya baridi. Ng’ombe akapita hapo akamdondoshea samadi. Samadi hiyo ilikuwa na joto. Ikawa nafuu kwa huyo ndege. Alifarijika kwenye samadi hiyo. Akaanza kuimba.
Paka akasikia ndege anaimba katika samadi. Paka akamfukua kutoka kwenye samadi ndege huyo na kumla. Fundisho la hadithi hii ni kwamba. Siyo kila mtu ambaye anakutupia samadi ni adui yako.
Anakusaidia kukubeba. Pengine mtu anayekupiga teke ukaanguka mita tano mbele amekusaidia kupiga hatua. Lakini siyo kila mtu anayekutoa kwenye samadi ni rafiki yako.
“Kama unaweza kutimiza ndoto yako peke yako, ndoto yako ni ndogo,” alisema Askofu T. D. Jakes. Unahitaji watu. Mwenye duka anahitaji wateja. Mwenye basi anahitaji abiria. Mwenye hoteli anahitaji walaji.
Nilitumiwa ujumbe kwenye simu uliokuwa na maneno haya, “kuzaliwa kwako kumefanywa na watu wengine. Jina lako umepewa na watu wengine. Umepata elimu kutoka kwa watu wengine. Kipato chako kwa namna fulani kinatoka kwa watu wengine…”
“Heshima nayo unapewa na watu wengine. Wa kwanza kukuogesha ni watu wengine. Wa mwisho kukuogesha watakuwa ni watu wengine. Mazishi yako yatasimamiwa na watu wengine. Utapelekwa kuzikwa na watu wengine. Kila unachokimiliki kitarithiwa na watu wengine.” Kwa nini turuhusu “umimi” ututawale?
Ili kufanikiwa unahitaji marafiki wa kweli. Tunahitaji kuwavuta watu kwa kutumia vizuri maneno. “Maneno matamu yatamrudishia mtu rafiki, na midomo yenye neema itamwongeza wamsalimio” (Yoshua bin Sira 6:5).
Nakubaliana na Orlando A. Battista aliyesema, “marafiki wa kweli ni watu ambao wanajua upungufu wako, lakini hujivunia sifa zako nzuri. Watu ambao hawawezi kusema lolote nyuma ya mgongo wako ambalo hawawezi kusema mbele yako.
“Watu ambao wameshiriki pamoja nawe katika furaha na karaha. Watu ambao wamekuimarisha wakati wa shida.” Suala la kudumisha urafiki si suala la kupata rafiki wa kweli tu. Ni suala la wewe pia kuwa rafiki wa kweli, mwandani wa kweli, mwenzi wa kweli.
Urafiki wa kweli katika mazuri hatuna budi kuudumisha. Ni jambo muhimu. Helen Keller aliyekuwa kipofu na bubu aliandika: “Afadhali nitembee na rafiki gizani kuliko kutembea pekee yangu kwenye mwanga.”
Binadamu si kisiwa anawahitaji watu wengine hasa rafiki.