Na Padre Dkt. Faustin Kamugisha
Mtazamo chanya ni sababu ya mafanikio. Mtazamo chanya unakufanya uyaone matatizo kuwa ni baraka katika sura ya balaa. Mtazamo chanya unakufanya kuhesabu siku zako kwa saa za furaha na si kwa saa za karaha. Mwenye mtazamo chanya akijikuta katika maji anaamua kuoga.
Washindi wengi wana mtazamo chanya. Kuna aliyesema “Mshindi kila mara ni sehemu ya jibu; mshinde (mtu aliyeshindwa) kila mara ni sehemu ya tatizo. Mshindi anasema, wacha nifanye kwa ajili yako; mshinde anasema, hii si kazi yangu. Mshindi anaona jibu kwa kila tatizo; mshinde anaona tatizo kwa kila jibu…Mshindi anasema, jambo hili linaweza kuwa gumu lakini linawezekana. Mshinde anasema, linawezekana lakini gumu sana.”
Ndugu msomaji, bila shaka umesoma kitabu kiitwacho Robinson Crusoe. Mtunzi wake ni Daniel Dafoe (1660-1731). Kitabu hiki kabla ya kuchapishwa alikipeleka kwa wachapishaji 20 na kilikataliwa. Kilipochapishwa kilipendwa. Kimekuwa kwenye soko zaidi ya miaka 250 na kimetafsiriwa katika lugha mbalimbali.
Daniel Dafoe alikuwa na mtazamo chanya. Alisema, “Katika shule ya mateso nimejifunza falsafa zaidi kuliko chuoni, na mambo ya Mungu kuliko kwenye mimbari ya mahubiri. Nimeona upande wa kuchafuka wa dunia na upande shwari wa dunia.” Katika mateso alijifunza jambo zuri, huo ni mtazamo chanya.
Alikuwa na matumaini kwamba kazi yake itachapishwa. “Matumaini ni nguzo ya dunia.” Ndivyo isemavyo methali ya Kiafrika. Mtu anayechukua mkopo ili aulipe ndani ya miaka thelathini ana mtazamo chanya na matumaini ya kuwa ataishi muda mrefu.
Biblia yasema, “Mtu anavyofikiria, ndivyo anavyokuwa” (Mithali 23:7). Mawazo yamekufikisha hapo ulipo. Lakini mawazo chanya yanaweza kukupeleka juu zaidi. Na mawazo hasi yanaweza kukupeleka chini. Kuwa na mawazo chanya.
Kuna methali isemayo, “Chawa alitoka kwenye nywele akaenda kwenye ndevu na kusema, yote makazi.” Jaribu kuona jambo zuri katika mambo mengi. Magari mengi yanakuwa yameandikwa maneno yenye mtazamo chanya.
Mifano michache: ‘Mbele daima, kurudi nyuma mwiko.’ ‘Kuendelea mbele kupitia kwenye ukungu’ na ‘Kuendelea mbele na ndoto.’
Mwenye mtazamo chanya anaona uzuri katika ubaya. Mwenye mtazamo hasi anaona ubaya katika uzuri. Mwenye mtazamo hasi mvua ikinyesha anasema kuna matope, mwenye mtazamo chanya anasema, vumbi limetulia. Mwenye mtazamo chanya anasema, leo nina hali nzuri zaidi. Mwenye mtazamo hasi anasema, jana hali yangu ilikuwa mbaya.
Mwenye mtazamo chanya anasema nafurahi naishi. Mwenye mtazamo hasi anasema, nasikitika kuwa siku moja nitakufa. Mwenye mtazamo chanya anaona mazuri katika matatizo, mwenye mtazamo hasi anaona matatizo katika mazuri.
Mchoraji wa Kifaransa, Pierre Auguste Renoir, alichora michoro inayovutia sana. Ingawa alikuwa na kipaji lakini kwake haikuwa kazi rahisi kutokana na afya yake mbaya. Alishambuliwa na magonjwa mengi. Hakuweza kusimama vizuri kukamilisha michoro yake. Wakati mwingine hakuwa na pesa ya kutosha kuweza kununua rangi na turubai za kuchorea.
Licha ya viunzi hivi, Pierre Auguste Renoir aliendelea kuchora michoro yenye rangi. Kuna mtu mmoja aliona Pierre Auguste Renoir akichora mchoro akiwa na mateso makubwa. Alimuuliza, “Kwa nini unateseka sana na unaendelea kufanya kazi hii?” Pierre Auguste Renoir alijibu, “Maumivu yangu yatatoweka karibuni au baadaye. Uzuri wa kazi hii utabaki daima.” Mchoraji huyu alikuwa na mtazamo chanya.
Ndugu msomaji, mtazamo chanya lazima uzingatie na uhalisia. Kama kuna mawingu mazito ya mvua usiseme mvua haitanyesha nina mtazamo chanya. Badala yake nenda na mwavuli.