Toleo lililopita tuliishia katika aya isemayo: “Aisee, kumbe mchungaji alikuwa akiniambia ukweli kuwa wewe ni mwandishi mzuri,’’ alizungumza profesa huku akitaka mara baada ya Mariana kumaliza kuangalia gazeti ampatie pia.

Mariana alipofungua ukurasa wa tisa wa gazeti akakutana na picha ya Noel. “Dah! Baba ona namna Noel anavyoandika,” alikuwa akimuonyesha baba yake, kisha profesa akalichukua gazeti na kuangalia, akapendezwa kwa  namna mpangilio wa makala ulivyokuwa, lakini akashindwa kusoma kwa kuwa alikuwa hana ufahamu wa lugha ya Kiswahili.

“Safi sana,’’ alimpongeza profesa. Meninda naye alitaka kuona, baba yake akampa gazeti lile ili aweze kuangalia. 

“Aisee, wewe Noel utakuwa mwandishi mkubwa baadaye,” alisema. Kila mmoja katika familia ya profesa alikuwa akimtia moyo Noel. 

“Nina mpango wa kuandika vitabu vingi na makala za kimataifa,’’ alijikuta Noel akizungumza ukweli uliotoka ndani ya moyo wake. 

“Inawezekana.” Walipokuwa wakiongea Meninda alikumbuka ofisini kwake walikuwa na jarida lililokuwa likiandika masuala ya wakimbizi. Akafikiria sana pasipo kuongea kisha akamuuliza Noel.

“Wewe ninaona unaongea lugha ya Kiingereza vema, sijui unajua na kuandika Kiingereza pia?’’ Noel akatabasamu kidogo kisha akamjibu: “Ninaweza, tena ndiyo ninaipenda kuliko lugha yangu ya Kiswahili.” Meninda akapanga akilini mwake namna ya kumsaidia Noel. “Ninafikiri anaweza ku….vema,’’ aliwaza Meninda akilini mwake.

***

Ulikuwa muda wa usiku, Noel akiwa amekaa mezani alikuwa na familia nzima ya profesa, Meninda na Mariana pamoja na mfanyakazi wa ndani.

Walikuwa wakila chakula cha usiku. “Noel wewe unatakiwa kufanya kazi kabla haujapata nafasi ya kusoma chuo,’’ alisema Mariana. 

Baba yake alikuwa makini kumsikiliza. “Ndiyo, hata mimi ninapenda iwe hivyo, lakini tunawezaje?’’ Profesa alikuwa akiwaza hilo, Mariana hakutaka kusema moja kwa moja alichokuwa anataka kukifanya, ilibaki kuwa sirini mwake.

“Ngoja Mungu atupe wepesi tuone,’’ alisema Mariana huku wakiwa wanakula chakula. “Mimi nikipata nafasi nitajitahidi kuandika,’’ alisema Noel. Meninda alikuwa akila lakini moyoni alikuwa akifikiria sana kuhusu Noel. 

“Kesho nikienda ofisini inabidi niongee na mkurugenzi wetu,’’ aliwaza akilini mwake Meninda. Yeye ndiye alikuwa akiwaza vitu chanya kwa Noel, alitaka kumsaidia Noel kwa moyo wa dhati.

Familia ya profesa pamoja na kuwa ni wasomi, lakini walikuwa ni watu wa kusali muda wa usiku pamoja kama familia.

“Jamani tule haraka tusali,’’ alisema profesa huku akimalizia kula. “Noel wewe huwa unasali?’’ aliuliza profesa akiwa ni mwenye tabasamu lisilokuwa na kifani. “Huwa ninasali sana prof.,’’ alijibu Noel.

Baada ya muda wa dakika kumi na tano walimaliza kula na kwenda kwenye makochi kukaa. Utulivu ukachukua sehemu kubwa, kila mmoja aliacha shughuli aliyokuwa akifanya ukawa ni muda wa mazungumzo ya kiroho. Meninda alikuwa ameshikilia Biblia na yeye siku hiyo ndiye alikuwa akiongoza tafakuri na ibada kwa usiku huo.

“Leo tutaangalia namna Mungu anavyotuahidi mambo mbalimbali katika Biblia,’’ alikuwa akiongea kwa lugha njema Meninda. Alikuwa ni binti mwenye imani. Mariana pia alikuwa na imani kwa vitu walivyopitia siku za nyuma, maisha ya mateso, umaskini na kubaguliwa na watu matajiri wa Kirusi kuliwafanya kuwa watu wa kusali na kuamini katika maombi na tafakuri ya Neno la Mungu. 

Alipokuwa akiongea Meninda kila mmoja alifungua biblia yake. Noel hakuwa na Biblia, walibaki kushangaa, Mariana akauliza: “Mbona Noel hauna Biblia?’’ Noel akakumbuka aliisahau alikotoka kutokana na  purukushani za safari.

Noel akatafutiwa Biblia kisha akapewa ili kuendana sawa na wengine. “Meninda unaweza kuendelea,” alisema profesa. Utaratibu huo haukuchukua muda sana, ilikuwa ni dakika arobaini pekee kisha kila mtu akaendelea na ratiba yake.

Muda ulikuwa umepita baada ya kumaliza maombi. Noel akapelekwa mpaka alikokuwa akienda kulala. Meninda anamkaribisha mpaka chumbani. Kilikuwa ni chumba cha kisasa na chenye ufahari. Noel akaelekezwa kila kitu. “Jisikie upo nyumbani,’’ alisema Meninda kisha akatoka na kwenda moja kwa moja chumbani kwake.

Noel akabakia mwenyewe akiwa anashangaa namna maisha yalivyokuwa tofauti na vile alivyokuwa amezoea. “Dah! Chumba kizuri, hapa inaonekana prof. ana pesa sana,’’ alikuwa akijiuliza hayo huku akiwa anazunguka kuangalia namna uzuri wa chumba ulivyokuwa.

Noel kabla hajapitiwa usingizi akachukua Biblia aliyokuwa amepewa kisha akapiga magoti na kuanza kusali tena. “Mungu nisaidie niweze kufanikisha azima ya kile kilichonileta.” Alikuwa akiomba akiwa anamaanisha. Chumba kilikuwa na runinga ndani, kilikuwa ni chumba kilichokuwa kimekamilika kwa kila kitu.

Noel kufika Moscow, Urusi ulikuwa ni muujiza ingawa alikuwa na matamanio siku nyingi kufika nchi za dunia ya kwanza. Ilikuwa ndiyo shauku yake pamoja na kutokea familia yenye hali duni kimaisha, lakini alikuwa na tamanio siku moja kufika katika nchi zilizoendelea.

***

Ulikuwa muda wa usiku kwa saa za Afrika Mashariki, mchungaji akiwa katika nyumba yake Mtaa wa Pasiansi jijini Mwanza, alikuwa amemaliza kusali, akawa anafikiria kuhusu maisha ya Noel, kisha akaongea mwenyewe: “Mungu, watu wote walio na nia na dhamira ya dhati katika maisha uwape wepesi,’’ alikuwa akinena kwa maneno mchungaji. 

Shauku yake ilikuwa ni Noel aweze kufika mbali katika ndoto yake na awe mtu wa kutumainiwa.

Wakati mchungaji akiwa anawaza hayo usiku huo, pia dada yake Noel, Zawadi, alikuwa  ameshalala kitandani. Ghafla, ndoto ikamjia, akaona akiwa amekaa katika hoteli fulani kubwa, ambayo ilikuwa imesheheni watu mbele. Akamuona Noel akiwa amesimama akiongea na watu lukuki wakiwa wanamsikiliza na kufuatilia kwa umakini kile alichokuwa akikiongea Noel.

“Mmh! Noel anaongea nini?’’ alikuwa akimuona akiongea lakini alichokuwa akiongea ni kama hakifahamu vema, akaamua kusogea karibu, akakuta ndiye, akaanza kushangaa. 

“Yaani watu hawa wote wanamsikiliza Noel!’’ Hakuamini kile alichokuwa akikiona mbele yake. Kwa muonekano akamuona Noel akiwa amevaa suti na akiwa mwenye kupendeza. Kushoto na kulia akaona watu wakubwa na wengine maarufu nchini Tanzania wakitega masikio yao kusikiliza alichokuwa akizungumza Noel.

Mama yake Noel, yeye alikuwa amekaa macho mikono akiwa ameiweka shavuni akitawaliwa na mawazo. “Mambo magumu sana, nifanye nini?’’ 

Mama yake Noel alikuwa hajui nini cha kufanya. Mama aliyekuwa amezaliwa kwenye shida na kukua katika shida, neema alikuwa hajaiona hata siku moja, kila kukicha kwake aliandamwa na matatizo.

Alikuwa amewasha kibatali ambacho walitumia kama mwanga kwa muda wa usiku. “Zawadi mwanangu ninajua anapambana lakini dah!’’ 

Alishika kichwa chake Mama Noel akagundua kwamba alikwisha kufanya makosa katika mfumo wa maisha. Akakumbuka hata wakati alipoondoka nyumbani kwao kwa kukimbia umaskini uliokuwa umekithiri. 

“Nilikimbia nyumbani umaskini na kuja mjini kusaka maisha mazuri, mbona bado shida tu?’’ alijiuliza mambo mengi akagundua kwamba huenda kuna mahali alikuwa ameteleza. 

Mtaani walikuwa bado wakidharauliwa, lakini Zawadi jitihada zake alizokuwa nazo kidogo zilikuwa zimeanza kuwafanya majirani kumtazama kwa jicho la tatu.

Zawadi akanyanyuka kutoka usingizini akiwa anafikicha macho yake: “Nimeingiwa na njozi mama,’’ alisema Zawadi, ndoto aliyokuwa ameota ilikuwa imetia hamasa ya aina yake katika moyo wake. 

“Njozi za nini Zawadi!’’ mama yake alisema  kwa kufoka. “Mama usifoke, ni kitu kizuri,’’ alisema kwa upole Zawadi akiwa anataka kumwambia mama yake kile alichokuwa amekiona ndotoni. “Usiamini katika ndoto, maana si vyote vilivyo katika ndoto hutokea kwenye uhalisia wa maisha,’’ alisema mama yake Noel akiwa anakanusha. “Mama ila kwa hili sijawahi kupata ndoto kama hii,’’ alisema Zawadi.

Zawadi alitokea kuamini ndoto aliyokuwa ameiona usingizini. “Haya niambie sasa tuone,’’ alisema Mama Noel huku akiwa anakaa vema kusikiliza. Zawadi akaanza kumwambia kile alichokuwa amekiota usingizini.

“Nimemuona Noel akiwa amesimama mbele ya umati mkubwa wa watu akiwa anazungumza,’’ alisema Zawadi. Alipomaliza mama yake akamjibu na kumwambia: “Hizo huwa ni ndoto tu Zawadi, uhalisia haupo,’’ alisema Mama yake Noel. 

Alikuwa ni mtu asiyeamini katika njozi, akijua hazina uhalisia wowote. “Ila sijawahi kupata njozi kama hii. Noel atakuja kuwa mtu mashuhuri na maarufu sana,’’ alisema Zawadi huku akifikiria kwa mapana na marefu.

Wakiwa wanazungumza, nyumba iliyokuwa jirani walikuwa wanakula chakula kama familia. Baba mwenye nyumba hiyo alikuwa akisikia Noel ni mtangazaji. Akagusia suala hilo: “Hivi huyu kijana jirani yetu amefikia wapi na fani yake?’’ alikuwa akiuliza baba wa familia hiyo iliyokuwa na uwezo kiasi.

“Simuoni siku kadhaa sijui amepotelea wapi?’’ alisema kijana wake aliyekuwa na dharau kwa kijana Noel. Alikuwa hamuamini kwa lolote na alimuona kama bango bovu lililofutika maandishi.