Huu ni mwendelezo wa kitabu cha toleo la kwanza. Ni hadithi inayozungumzia mwenendo na ndoto ya kijana Noel ambaye alitokea katika familia duni na hatimaye akafanikiwa kwa kiwango kikubwa. Fuatilia hadithi hii yenye mafunzo na hamasa…

Noel akiwa nyumbani kwa mwenyeji wake aliyempokea uwanja wa ndege jijini Moscow

Ni muda wa jioni kwa saa za Urusi, Noel alikuwa amefika nyumbani kwa mwenyeji wake. Alipokewa kwa furaha na bashasha. “Noel karibu jisikie upo nyumbani,’’ alisema profesa. Alikuwa ni mtu aliyejaa tabasamu usoni mwake. “Sawa profesa, asante,’’ alijibu Noel.

Nyumba aliyokuwa akiishi profesa ilikuwa kubwa, ikiwa na kila kitu ndani. Wakati Noel akiwa amevaa koti zito kwa ajili ya kujikinga baridi huku akizungumza, profesa alikuwa amekaa mezani na Noel, akiwa hataki kumuona Noel akiwa mpweke.

Profesa alikuwa anaishi na mabinti zake wawili; Meninda na Mariana, mabinti zake walikuwa ni wasomi. Mmoja alifanya kazi katika shirika la kuhudumia wakimbizi kutoka Afrika ambaye ni Meninda. Mariana yeye alikuwa mhadhiri katika chuo cha kidini kilichokuwa katika Jiji la Moscow. 

Wakiwa wanaongea, Meninda alikuwa jikoni akimsaidia mfanyakazi wao wa ndani kupika. “Chemsha chai kwanza, ni baridi mno,” alisema Meninda akiwa ameshikilia chupa ya chai. “Ndiyo ipo jikoni,’’ alijibu mfanyakazi wao. Maisha ya nyumbani kwa profesa waliishi kwa upendo. Punde Mariana alitoka na kwenda sebuleni alikokuwa amekaa baba yake pamoja na Noel, kijana kutoka Afrika.

Noel alikuwa anahisi baridi na isitoshe hakuwa amezoea maisha ya baridi. “Huku kuna baridi sana,’’ alisema Noel huku akitetemeka mpaka meno. 

“Ni kweli jiografia yetu ndivyo ilivyo,’’ alisema profesa. Mbele ya meza aliyokuwa amekaa profesa kulikuwa na tanakilishi mpakato ambayo alikuwa akiitumia kwa kazi zake mbalimbali ikiwemo kuandalia vipindi vya kufundishia chuoni.

Mariana naye alikuwa na tanakilishi yake akaitoa akiongea huku akifanya mambo yake. Profesa alimtambulisha Noel kwa Mariana binti yake. “Mariana, huyu anaitwa Noel, Mtanzania.” Aliposema Tanzania, Mariana alikumbuka kuwa aliwahi kufika nchini Tanzania akiwa anatembelea mbuga za wanyama.

“Unapafahamu Kilimanjaro?’’ alikuwa anauliza Mariana, akikumbuka maisha ya nchini Tanzania namna alivyokuwa akitalii na kuangalia mbuga mbalimbali. Ilikuwa inakumbusha matukio ya nyuma namna ilivyokuwa.

“Ninapafahamu, ulikwishafika huko?’’ aliuliza Noel, wakajikuta wakitengeneza maongezi mengi. Profesa aliendelea kusema: “Mariana, huyu ni mwandishi mzuri na amekuja kufanya mtihani wa majaribio katika Chuo Kikuu cha Moscow.’’ 

Mariana alimpongeza Noel. “Oooh! Hongera sana.’’ Huku akimpa mkono. “Asante,’’ alisema Noel akiwa anajisikia mwenye furaha kwa namna ambavyo profesa aliishi na familia yake. Pia ndiko kulifanya Noel kuendelea kuwa sehemu ya furaha ya maisha yale. 

“Tutakuwa naye hapa nyumbani,’’ aliendelea kuzungumza Profesa. “Nimefurahi sana baba kuwa ninaishi na mwandishi ndani,’’ alisema Mariana.  Mariana alikuwa mchangamfu na alikuwa akipenda kuandika kitabu lakini hakuwa na uwezo huo, akahisi huenda kwa ujio wa Noel anaweza kujifunza mengi katika eneo hilo.

Punde tu Meninda naye alitoka jikoni na kuja sebuleni akiwa na chupa ya chai, alifika na kuikalisha mezani. “Jamani samahani kwa kuwa nimechelewesha chai,” alisema Meninda. Wakamsamehe, kisha profesa akamimina chai.

“Noel, mimina chai upate kutuliza baridi,” alisema. Wakati huo walikuwa wakingoja chakula cha jioni. Kila mmoja alikuwa akizungumza huku akifanya shughuli nyingine katika kompyuta yake. Noel peke yake ndiye alikuwa amekaa tu akinywa chai.

“Noel, mimi nina ndoto ya kuandika kitabu kuhusu wakimbizi, utanielekeza ili tuandike,’’ alisema Mariana. Lilikuwa wazo lake alilokuwa nalo siku nyingi akilini mwake.

“Tutafanya hilo,’’ alisema Noel akiwa anamaanisha. “Ndiyo, mnaweza kuandika na kwenda Afrika kufanya utafiti wa kutosha,’’ aliwashauri profesa.

“Mariana bado wazo lako unalo tu!’’ alishangaa Meninda, maana ilikuwa ni miaka mingi imepita akiongelea suala hilo. “Ndiyo, bado ninawaza halafu Mungu ametuletea Noel, huyu ni mwandishi.’’ Walikuwa wakijadili mambo mengi. Noel aliendelea kufurahia namna ilivyokuwa. “Kumbe mgeni ni mwandishi! Aisee safi sana,’’ alisema Meninda kwa tabasamu na bashasha. Noel alibakia kutabasamu.

“Enzi za ujana wangu nilisoma vitabu vingi sana,’’ alisema profesa. “Kumbe! Ndiyo maana baba ulitengeneza kabati kubwa la vitabu,’’ alisema Mariana kwa furaha. 

“Ndiyo, siwezi kuishi bila kusoma, nitakuwa vipi kiakili?’’ Kwa maneno hayo ya profesa, Noel alijikuta akiendelea kuhamasika zaidi. 

Wakiwa wanaongea, mchungaji akapiga simu kwa profesa. Simu iliita kisha profesa akapokea. “Haloo’’, kisha, mchungaji akauliza kwa mara nyingine: “Amefika salama kijana?’’ “Amefika tuko nyumbani tunaongea na vijana wenzake,’’ ilikuwa ni furaha mchungaji kusikia hivyo. Profesa akampatia Noel simu akazungumza na mchungaji mawili – matatu.

“Noel kazana, usikate tamaa, tambua huko unatengeneza njia nyingine.”  Maneno ya mchungaji Noel alikuwa akiyazingatia siku zote na hakutaka kuyaacha bila kuyafanyia kazi.

Baada ya mazungumzo mchungaji alikata simu kisha maongezi yaliendelea pale mezani walipokuwa wamekaa profesa, Noel pamoja na mabinti zake wawili. 

“Noel mbona umekaa kwa upweke sana?’’ aliuliza profesa.

“Baba unamaanisha nini?’’ aliuliza Mariana. “Hana cha kufanya chochote, chukua funguo achukue kitabu chochote asome,’’ alisema profesa huku akiwa anatoa funguo na kumpatia Mariana aende kumfungulia kwenye kabati la vitabu. Mariana alinyanyuka akiwa na funguo amezishika mkononi mwake na kuelekea kwenye kabati la vitabu.

“Noel twende uchague kitabu unachopenda kusoma,” alisema Mariana kisha Noel akanyanyuka, wakaambatana hadi kwenye kabati la vitabu.

Mariana alifungua mlango wa kabati la vitabu. Noel akakutana na shehena ya vitabu. Profesa alikuwa amevipangilia katika mtiririko sahihi. “Mbona ninakosa cha kuchukua, vyote ni vizuri,’’ alisema Noel. Akiwa anaangaza huku na kule ghafla akakiona kitabu kilichokuwa kimemvutia lakini hakujua kiliandikwa na mwandishi kutoka wapi.

Noel akakichukua kisha akamwambia Mariana: “Hiki ninafikiri kitanifaa.’’ Alikiangalia mara mbili mbili. “Ni kitabu kizuri ameandika mwandishi maarufu hapa nchini Urusi,’’ alikuwa akitoa maelezo mafupi Mariana ya kile kitabu. 

Noel alikishika vema kisha Mariana akafunga kabati na kwenda mezani. Profesa alitaka kumuona Noel akiwa bize na  kitu fulani. Hakutaka kuona akiwa amekaa tu na kuongea. Noel alikuwa msomaji mzuri wa vitabu.

***

Noel alikuwa ameweka umakini wa hali ya juu wakati alipoanza kusoma kitabu kile. Alifungua na kuangalia mwanzo wa kitabu akakutana na mawasiliano ya yule mwandishi wa kitabu.

Noel akaomba kalamu kwa Mariana, kwa kuwa aliingiwa shauku katika yale mawasiliano mara baada ya kuyaona.  “Umepata kitu Noel?’’ aliuliza Mariana, huku akimpatia kalamu.

“Ndiyo nimepata kitu fulani,’’ alisema Noel pasipo kusema ni kitu gani alichokuwa amekipata. Noel aliandika katika karatasi mawasiliano ya mwandishi, kisha akaiweka ndani ya kitabu. 

“Dah! Japo simfahamu ila ipo siku nitamtafuta,’’ alijisemea moyoni Noel huku akiendelea kusoma. Muda huo walikuwa kimya kila mmoja akiwa bize na kile alichokuwa akikifanya.

Baridi ilikuwa kali, saa nazo zilikuwa zikiendelea kusonga. Noel ndiyo alikuwa amewasili nchini Urusi kila muongozo alisubiri kutoka kwa profesa. “Noel leo pumzika kesho tutakwenda chuoni ili kujua kitakachokuwa kikiendelea.’’ 

Noel aliposikia hivyo alifurahi sana, alitamani apate nafasi, aweze kusomea pale pale nchini Urusi. “Kumbe amekuja kufanya mtihani wa majaribio?’’ aliuliza Meninda. “Ndiyo, Mungu akupe wepesi Noel ufanikiwe,’’ alisema profesa. 

“Mimi kwa ninavyomuona Noel atafanikiwa tu,’’ alisema Mariana akiwa anampa moyo Noel. 

“Kwani Noel ulikuwa unataka kusoma shahada ya kitu gani?’’ Noel alisimama kusoma kitabu kisha akamwambia: “Mimi nilitaka kusoma shahada ya Habari na Mawasiliano.” Meninda aliendelea kumpa moyo: “Utasoma tu na utakuwa mwanahabari mzuri hapa hapa Moscow,’’ alisema Meninda akiwa anaamini hakuna linaloshindikana duniani.

“Asante sana,’’ alishukuru Noel. Hamasa aliyokuwa akiipata ilikuwa tofauti na nchini Tanzania kwani alidharaulika na kukosa watu sahihi wa kumtia moyo. “Mbona hawa watu wananitia moyo na faraja sana!’’ alikuwa akishangaa moyoni mwake. 

Noel alikumbuka, aliondoka na magazeti kwenda nayo Urusi.

Magazeti yalikuwa na makala zake alizokuwa akiandika nchini Tanzania. “Dada Meninda naomba begi langu dogo,’’ alisema Noel, Meninda anaondoka na kwenda chumbani alipokuwa ameweka begi la Noel.

Meninda alichukua begi la Noel na kwenda nalo mpaka pale mezani, kisha akampa Noel. “Humu kuna magazeti yangu niliyokuwa ninayaandikia nchini Tanzania,’’ alisema Noel, akiwa anafungua zipu ya begi lake. Akatoa magazeti na kumuonyesha Mariana, lakini profesa naye alipata hamasa akatamani kuona Noel alichokuwa ameandika. 

“Aisee kumbe mchungaji alikuwa ananiambia ukweli kuwa wewe ni mwandishi mzuri,’’ alisema profesa huku akitaka mara baada ya Mariana kumaliza kusoma ampatie.