Katika toleo lililopita sehemu ya tatu tuliishia aya isemayo: “Leo sijaonana naye hata kidogo,” alisema rafiki yake Noel akiwa anasogea na kuegemea mtini. “Shule ni ngumu sana?’’ alihoji Mama Noel. Sasa endelea…
Japo kuwa kwao Noel kulikuwa ni mjini lakini walikuwa wakipika kwa kutumia kuni, si kwa kupenda, bali ulikuwa ni ukata uliokuwa umetawala katika maisha yao. Kupikia mkaa kama wengine ilikuwa ni gharama kwao kuweza kumudu.
Punde si punde Noel akawa ametoka bafuni, maji yalikuwa yakimdondoka kutoka mwilini kwa matone. “Gilbeth?’’ aliita Noel kisha Gilbeth akaitika: “Naam Noel!’’ akamsogelea karibu wakaanza ongea na kusalimiana kwa ukarimu.
Noel na Gilbeth walitokea kupendana na hatimaye wakawa marafiki walio sikilizana kwa kila jambo. Na wote walikuwa wakisoma mchepuo mmoja, yaani (HGL) ingawa katika malengo yao kila mmoja alikuwa na yake tofauti na mwenzake.
Noel alipenda kuwa mwandishi mzuri wa vitabu wakati Gilbeth yeye alikuwa anataka kuwa mwanasheria mzuri na mtazamo wa “Succes is on my Mind’’ wote walikuwa nao. Walipenda kuutumia kama kaulimbiu kila walipokuwa wakipita.
“Leo haukuingia darasani?’’ alihoji Gilbeth. “Ngoja tutaongea, kuna jambo limetokea,’’ alisema Noel huku akisogea kukaa karibu na Gilbeth.
***
Baada ya miezi mitatu kupita Noel alikuwa amefanikiwa kuhitimu masomo yake ya kidato cha sita. Wakati huu maisha ndiyo yalimwendea vibaya, maana alishinda kutwa nzima akiwa amebeba bahasha ya kaki. Marafiki zake karibu wote hakuweza kuwa nao wakati huo.
Jua lilikuwa kali na kumuishia lote Noel kiasi hata cha kuunguza ngozi yake. Alikuwa katikati ya mji wa Mwanza, alitembea lakini hakuchoka. Siku hiyo Noel alitembea na kuamua kwenda eneo moja zuri lililokuwa katikati ya mji wa Mwanza na kuamua kukaa.
Eneo lilikuwa na bustani nzuri ya majani ya kuteleza, mawe yake pia yalikuwa ni ya kihistoria katika taifa la Tanzania.
Eneo hilo lilikuwa mwambao wa Ziwa Victoria. “Dah! Niliambiwa leo saa ngapi?’’ alijiuliza mwenyewe akilini mwake. Siku iliyokuwa imepita alikuwa amekwenda kuomba kazi katika ofisi moja ambayo ilikuwa ni kituo cha matangazo ya redio.
Walimwambia afike siku inayofuata ambayo ilikuwa ndiyo siku hiyo. Wakati akiwa pale kwenye ufukwe uliokuwa na bustani nzuri, Noel alikuwa hana hata shilingi moja mfukoni mwake, njaa ilikuwa ikimuuma lakini ikafikia hatua akawa ameizoea hali ya kukaa bila kula kwa muda mrefu. Akiwa amekaa, mara akaona gari zuri la kifahari likiwa limekuja karibu na ule ufukwe na kuegeshwa pembeni.
Akamuona baba mmoja akishuka kutoka katika lile gari la kifahari, kwa muonekano yule baba alionekana kuwa ni mtu mwenye uwezo sana wa kifedha. Alikwenda kukaa pale pale alipokuwa amekaa kijana Noel.
Alimsemesha Noel: “Kijana vipi hali yako?’’ aliongea yule baba huku akienda kukaa kwenye kiti. “Salama,’’ Noel aliitika huku akiwa hana furaha kutoka moyoni.
Yule mzee alikuwa na soda ya kopo, aliitoa na kuanza kunywa taratibu. “Unaitwa nani rafiki?’’ aliuliza yule mzee. Noel naye hakusita kumjibu au kumwambia jina lake: “Naitwa Noel.’’ Hata ongea yake ilikuwa kama analazimishwa kuongea kutokana na njaa aliyokuwa nayo kijana Noel.
“Noel mbona una mawazo?’’ aliuliza huku akiwa anamwangalia Noel.
Noel alimficha na hakutaka ajue chochote kuhusu yeye. Alimjibu kwa kumridhisha. “Hamna, niko kawaida,’’ alisema kijana Noel akiwa amegeuza macho yake kuelekea upande wa ziwani.
Yule mzee bado aliendelea kumuuliza maswali: “Unasoma?’’ Noel alimjibu: “Nimemaliza kidato cha sita.” Kisha akakaa kimya.
“Ina maana unasubiri kwenda chuo kikuu?” aliuliza. Noel aliitika: “Ndiyo.’’ Alionekana kumfurahisha yule mzee kwa maana alikuwa anawapenda vijana wasomi japokuwa yeye alibahatika kuwa na pesa lakini alikuwa hana elimu.
“Safi sana na sasa hivi unafanya kazi gani?’’ aliuliza yule mzee. “Natafuta kazi ya muda nifanye,” Noel alizungumza kwa kusononeka kwa sababu alikuwa hayapendi maisha ya umaskini.
Aliona namna umaskini unavyo yagharimu maisha ya nyumbani kwao. “Mmmh! Utapata kweli?’’ alimuuliza yule mzee huku akizidi kumkatisha tamaa Noel. Lakini kwa kuwa Noel alikuwa si mtu wa kukata tama, alimwambia: “Najaribu, nikishindwa basi.’’ Yule mzee alitaka kujua kwa nini Noel anatafuta kazi badala ya kusomea kitu chochote ili kujiandaa kwa maisha ya chuo kikuu ili kiweze kumsaidia baadaye.
Noel baada ya kuulizwa hivyo aliamua kusema ukweli halisia wa maisha yake. “Mimi ninatokea katika familia duni’’, alisema Noel. Yule mzee akawa anamtazama Noel kisha akamuuliza: “Wewe unahisi kazi gani itakusaidia?’’ aliuliza huku akimgeukia na kumuangalia kwa umakini.
“Nikiwa mtangazaji nahisi nitaisaidia familia yangu,’’ alisema kwa kujiamini Noel, akijua utangazaji pamoja na uandishi wa habari ni vitu alivyovipenda kutoka moyoni.
“Aisee! Lakini…’’ alishangaa kumuona kijana kama Noel katika taifa la Tanzania. “Kwa hiyo utaweza utangazaji?’’ aliuliza zaidi yule mzee. Noel aliendelea kumuaminisha: “Naweza kusema sijapata kituo cha utanngazaji.’’ Alikuwa akizungumza kwa hisia, maana alikuwa akizungumzia kitu alichokipenda.
Kitu ambacho kilimfanya Noel aweze kujiamini ni pamoja na kugundua kwamba alikuwa na sauti nzuri. “Sasa nitakupeleka kwa rafiki yangu fulani,’’ alimuahidi kwa sababu aliona Noel akijiamini. “Ana redio?’’ aliuliza Noel kwa umakini huku akigeuza uso wake kumtazama yule mzee. “Ndiyo ana redio kubwa sana,’’ alisema. Ilikuwa ni furaha iliyoleta mtikisiko katika moyo wa Noel na kuleta tumaini jipya.
“Una simu?’’ aliuliza yule mzee. Noel akamwambia: “Hapana.’’ Nyumbani kwao Noel hata mtu mmoja alikuwa hana simu wala hata uwezo wa kununua simu hawakuwa nao. Yule mzee aliwaza kisha akamwambia Noel: “Sasa nitakupataje?’’ yule mzee alikuwa akiumiza kichwa atampataje Noel mara baada ya kuachana ikiwa hana simu.
Noel naye alikuwa anawaza atumie njia gani au namba ya ndugu yake yupi ili aweze kumpatia ili waweze kuwasiliana kwa urahisi.
“Ninafikiri nina simu nyingine.’’ Alikumbuka kuwa ana simu ambayo ilikuwa ni mbovu ampatie Noel ili aweze kumpata kwa urahisi. Kwa njia ambayo ni rahisi katika mawasiliano ‘mmmh’ aliguna huku akienda kwenye gari lake kisha akatoa begi kubwa lenye rangi nyeusi akaanza kulipekua.
Katika kuangalia alibahatika kupata ile simu ambayo alikuwa akiiwaza kwa muda mfupi uliokuwa umepita. “Safi sana, hii hapa unaweza kutumia,’’ alisema huku akiwa anamkabidhi simu mkononi.
Rafiki yake Gilbeth aliamua kwenda kujikita katika uchimbaji wa madini kwenye migodi, naye maisha yalikuwa yakimwendea vibaya kila kulipo kucha. “Dah!’’ alikuwa akiwaza huku akipiga mihayo na mchana huo njaa ilikuwa ikimuuma na pesa za kununua chakula alikuwa hana. Maisha ya Kahama yalikuwa yamemshinda kijana Gilbeth.
Mtu wa kumsaidia pia alikuwa hamuoni. Huo ulikuwa ni wakati mgumu kwa kijana Gilbeth. “Kukaa hapa mimi bila kazi siwezi,’’ alisema kijana Gilbeth. “Wewe mwanaume unachagua kazi!’’ alisema kijana mwenzake ambaye alikuwa mchimbaji mdogo wa madini. Gilbeth akaghadhabika moyoni kwa kuwa hakuna ambacho huyo kijana mwenzake aliweza kumsaidia.
“Hapa kuna pesa’’ alizidi kumwambia. Gilbeth akamuangalia akamuuliza: “Ziko wapi hizo pesa?’’ alikuwa akimuona kama mtu anayeongea pasipo kuchunguza kitu. “Unataka zikufuate? Tafuta,’’ alimwambia yule kijana mwenzake.
Alimjibu pasipo kumuonea huruma mwenzake. Gilbeth alikuwa hayawezi maisha ya mgodini na hakuwahi kuyaishi. Gilbeth aliwaza: “Hivi nini ambacho kilinileta huku?’’ Yeye pia alikuwa na mawazo ya uandishi wa habari lakini ilikuwa si kama ya Noel. Gilbeth alikuwa na kipaji kizuri cha uchoraji na alikuwa ameshachora michoro mingi na kuitunza ndani.
Wakati alipokuwa akiwaza, yule kijana mwenzake aliondoka na kumuacha huku akimwambia: “Waza mwenyewe hapo.” Aliondoka huku Gilbeth akiwa anawaza na hata kumkumbuka rafiki yake Noel namna walivyokuwa wakipeana ushauri, mawazo na faraja katika maisha.
“Hapa nilipo hapanifai,’’ aliwaza Gilbeth moyoni akiwa katika msongo mkubwa wa mawazo. Mchimbaji mmoja mdogo aliyekuwa akifahamiana naye alimfuata na kumwambia: “Punguza mawazo.’’
Alimsemesha kwa kumshtukiza kisha Gilbeth akashituka: “Alaaa, bhana weee!’’ Yule mchimbaji akamwambia: “Punguza mawazo.’’ Gilbeth akawa mkali, kisha akamjibu yule mchimbaji: “Naomba niache.’’ Alisema huku akiwa amejawa hasira isiyokuwa na kifani.
Wakati yeye na Noel wakihangaika, wenzao waliomaliza wote kidato cha sita walikuwa nyumbani wakisubiri matokeo ya kwenda vyuo vikuu.
Lakini kwa Gilbeth na Noel wao ilikuwa tofauti, walipambana kwa kufanya kazi ili kuweza kufanikisha ndoto zao. “Twende chimbo,’’ alimwambia yule kijana mchimbaji mdogo.
Gilbeth baada ya kutuliza hasira alimwambia: “Hapana, akili yangu haiko sawa.’’ Yule mchimbaji mdogo wa madini alikuwa amezoeana sana na Noel. Alitoa Sh 30, 000 na kumpatia Gilbeth.
“Asante sana,’’ alisema Gilbeth huku akiwa na tabasamu. Ilikuwa kama nuru Yehova aliyoamuangazia na kumshushia. “Kawaida rafiki yangu itakusaidia,’’ alisema hivyo kisha akaondoka. Gilbeth alibaki mwenyewe kwa muda kidogo kisha naye alinyanyuka na kwenda hotelini kwa ajili ya kupata chakula.
Alimuona hakika yule kijana ana utu kuliko vijana wengine pale mgodini. “Dah! Amenisaidia kwa leo,’’ alijisema mwenyewe akiwa anakwenda mgahawani.