Congolese workers search for rough diamonds Kangambala mine in Lunged, in the south west region of Kasai in the Democratic Republic of Congo, the heart of the diamond mining area in the DRC, August 9, 2015. Diamond buyers and manufacturers in the west are trying to find a way to make the diamond industry cleaner and more responsibly-sourced, in order to combat human rights abuses, child labor, the degradation of the environment, and unfair trade practices. (Credit: Lynsey Addario/ Getty Images Reportage for Time Magazine)

Toleo lililopita katika sehemu ya pili tuliishia aya isemayo: “‘Dah! Biashara hii sasa mbona inaendelea kufilisika?’ aliwaza kichwa kikawa na msongo wa mawazo. Siku hiyo ilikuwa ngumu kwa Mama Noel kutengeneza pombe nyingine, kwa kuwa hakuwa na pesa hata senti moja. Wateja wake walianza kuja mmoja baada ya mwingine, alihisi Mwenyezi Mungu hathamini uwepo wake katika dunia hii.” Sasa endelea…

Tumboni kwa mama yake Noel walizaliwa watoto wawili tu ambao ni Noel na dada yake. Dada yake alikuwa ameishia kidato cha nne na alikuwa mama wa nyumbani aliyeolewa na mfanyabiashara mmoja wa hali ya kati.

Ilikuwa mchana, jua likiwa linawaka, hali ya dada yake kule ndani ya nyumba ilikuwa si nzuri, mambo yaliharibika. Alifukuzwa na mume wake. Ilikuwa ni vita ndogo ndani ya nyumba. “Toka maskini wewe,’’ yalikuwa maneno ya kuchoma kwa dada yake Noel akiambiwa na mume wake.

“Nisamehe mume wangu,’’ alijitetea Zawadi ili kulinda ndoa yake.

Alizungumza huku akiwa analia na kumpigia magoti hadi chini mume wake. Mafurushi yake ya nguo mume wake alikuwa tayari ameyaweka katika sebule.

“Sikutaki,’’ aliongea kwa hasira na kufoka sana. Kosa lilikuwa ni kile alichodai mume wake ni matumizi mabaya ya pesa ambayo hakufurahishwa nayo. Zawadi alijitahidi kumbembeleza mume wake lakini haikuwezekana, aliendelea kumtolea matusi na maneno ambayo yalilenga ufukara wa nyumbani kwao Zawadi.

“Umaskini wa kwenu unaniletea mimi?’’ alisema mume wa Zawadi. Wakati mtafaruku huo ukiendelea, Mama Noel alikuwa njiani kuelekea nyumbani kwa Zawadi.

Pesa zote askari walichukua, alibaki hana pesa hata senti moja. Kanga na nguo alizokuwa amevaa zilikuwa zina matobo mengi sana. Hakika, ilionyesha dhahiri kuwa ana dhiki katika maisha yake. Zawadi alipokuwa ameolewa palikuwa si mbali na nyumbani kwao, ulikuwa ni umbali wa kilometa moja au nusu.

“Leo lazima uende kwenu,’’ alisema mume wa Zawadi. “Nisamehe,’’ alisikika Zawadi huku akimuangukia miguuni mume wake.

“Zawadi, niachie,’’ alisema mumewe huku akienda chumbani kwao akiwa hataki hata kusikia sauti ya mke wake.

“Nitakwenda wapi Mungu wangu!’’ aliwaza Zawadi huku akizidi kujaza mapigo mengi katika moyo wake. Akiwa analia na mikono akiwa ameiweka mashavuni, mara akasikia sauti ya mtu akibisha hodi nje ya nyumba yao, sauti alikuwa ameshaijua ingawa ilikuwa ikitoka kwa mbali. “Hodi hapa?’’ akaitikia ndugu yake mume wa Zawadi.

Zawadi alikuwa amekaa kwa huzuni, hata nguvu za kwenda kufunga mlango zikawa zimekosekana.

“Wamo humu ndani?’’ aliuliza Mama Noel huku akiwa na wasiwasi. “Ndiyo, wamo ingia mpaka ndani,’’ alimfungulia geti. Mama Noel aliingia mpaka ndani. Wakati akiwa anafungua tu geti na kuingia alimuona kwa mbali Zawadi akiwa amejawa machozi mengi katika paji lake la uso.

Raha aliyokuwa nayo Zawadi katika kumkaribisha mama yake ilikuwa ni ya kawaida. “Zawadi,’’ alimuita huku akiwa anamshangaa.

Zawadi alipomuona mama yake uchungu ulizidi katika moyo wake.

Machozi yaliendelea kutoka kwa wingi. “Zawadi unalilia nini?’’ aliuliza Mama Noel kwa mara ya pili huku na yeye akikaribia kububujikwa machozi.

“Baba Janeth ananifukuza,” alisema huku akiendelea kulia. “Umekosa nini?’’ Hali hiyo ili mshangaza Mama Noel. Alikuwa hakutarajia wala kufikiria kuikuta hali ile.

Wakati wakiwa wanazungumza Zawadi na mama yake, mara mume wake akatoka nje akiwa na hasira isiyokuwa na kifani. Tena alizidi kusisitiza kauli yake ile ile: “Ondoka hapa kwangu,’’ alishangaa Mama Noel kisha akamuuliza: “Imekuwaje tena jamani?’’  alihoji Mama Noel huku akimuona mkwe wake hana muda naye.

Alitoka nje, akatoa bastola na kuwanyooshea: “Wote ondokeni, sitaki kuwaona hapa,’’ alivaa roho ya ujasiri mpaka kwa mama mkwe wake. Baada ya kufanya hivyo kila mmoja alimkimbia na kumuacha. Aliendelea kutoa maneno ya kukashifu familia yao.

“Mwanangu twende,’’ alisema kwa woga Mama Noel. “Yaani sirudi tena hapo,’’ alisema Zawadi huku akiwa anafuta machozi yake taratibu.

“Leo ametukashifu na kututolea maneno ya kejeli hivi!’’ alishangaa Mama Noel. Njaa nayo ilikuwa ikisumbua tumbo lake. “Nilikuwa sijui kama mume wangu yuko hivyo!’’ alisema Zawadi akiwa ameweka azimio moyoni mwake la kurudi nyumbani kwao moja kwa moja, ajue la kufanya ni lipi baada ya kufukuzwa kwa mume wake.

Muda ulikuwa ukiyoyoma. Noel akawa ameishamaliza kazi yake aliyopewa. Watu walijua atakuwa ni kijana wa mtaani na mpambanaji, hawakuweza kufikiria kama angekuwa mwanafunzi.

“Wewe Bwana mdogo?’’ alimuita yule mtu ambaye alikuwa amempa kibarua Noel. Noel aliitikia kwa heshima akiwa amechuchumaa chini, kwa maana alikuwa amechoka sana. “Naam!” aliitika huku akimfuata yule mtu.  Alipofika karibu zaidi yule mtu hakupoteza muda, alimpatia ujira wake Noel.

“Bwana mdogo shika pesa yako kabisa,’’ ilikuwa pesa tasilimu Sh elfu thelathini. Ilikuwa furaha kwa kijana Noel ingawa kazi ilikuwa ngumu sana. Furaha ilikuja baada ya kufikiria kwamba hakutarajia kama angeweza kupata kazi kama hiyo. “Kesho kama utaweza njoo,’’ alimwambia yule ntu kijana Noel, maana alikuwa ameupenda utendaji wa kazi wa Noel.

Noel akamjibu: “Nitakuja kesho asubuhi,’’ alipoambiwa hivyo ilimpa moyo na faraja, aliondoka huku akiwa anachezacheza na kurukaruka. Noel alipoondoka kitu cha kwanza aliwaza kwenda sokoni kununua chakula.

Usiku ulikuwa umeingia, Mama Noel pamoja na Zawadi walikuwa wamekaa nje ya nyumba yao wakiwa wamejikunyata. Mtoto wa Zawadi alikuwa analia: “Mbembeleze mtoto,’’ alisema Mama Noel huku njaa ikiwa inawatafuna, hata ongea yake ilikuwa imebadilika.

“Noeli naye mbona hajaja mpaka muda huu?’’ alisema akiwa anasonya sonya akimuwazia Noel .

Kumbe ilikuwa ni kwa neema Noel alikuja kuishibisha familia yake.

“Naona atakuwa amepita kujisomea kwa wenzake,’’ alisema dada yake Noel. Punde si punde Noel akawa amefika akiwa ameshikilia mifuko miwili ya rambo ikiwa imejaa vyakula mbalimbali alivyokuwa amenunua sokoni kwa ajili ya kumletea mama yake aweze kupika wale.

“Mama! Mama,” alianza kuitia akiwa mbali. Kabla hata hajapokewa mizigo aliyobeba, ghafla akawa amedondosha chini viazi vyake. Mfuko mmoja ulikuwa umepasuka.

“Noeli umeleta nini?’’ aliuliza Mama Noel huku akiwa anainama katika giza usiku huo kuangalia. “Nimekuletea viazi mama,’’ alisema Noel huku na yeye akiwa ameyaelekeza macho yake chini kuangalia viazi vitakuwa vimedondokea uelekeo gani.

Mama yake pamoja na dada yake baada ya kusikia ni chakula, kitu ambacho hawakutegemea kutoka kwa Noel, waliinama na kuanza kuviokota sambamba na kuviosha. Walifikiri huenda siku ingeisha wakilala njaa, matumaini yalikuwa yamekwisha kuwatoka.

Lakini Noel alikuja kuibua tumaini lao. “Na dada Zawadi amekuja saa ngapi?’’ aliuliza Noel huku akimpatia mfuko mwingine uliokuwa na vyakula vingine. Mama yake Noel alikuwa hawezi kumjibu maana njaa ilikuwa ikimsumbua sana.

Kisha akamwambia: “Mwanangu umejuaje kama leo hali ni mbaya?” Noel akamwambia: “Mama nilijua ndiyo maana nikafanya hivyo.” Jasho lilikuwa likimtoka mwilini. Noel akaamua kuchukua ndoo na kufuata maji ili kuja kuweka mwili wake safi.

Alipofika bombani alikuta vijana wenzake wakiwa wanateka maji huku wakiongea. Vijana hao nyumbani kwao walikuwa na maisha mazuri ya wastani, walianza kumsema na kumg’ong’a Noel.

“Huyu sasa hivi yuko kidato gani?’’ waliulizana kisha mmoja akawajibu: “Yuko kidato cha sita.’’ Walipokuwa wakiongea Noel alikuwa amewasikia vizuri. “Kwa hiyo ndiyo anataka kuikomboa familia yake?’’ mmoja wao alisikika akisema. Maneno yaliyokuwa yakiongelewa kuhusu yeye na  familia yake yalikuwa yakimpa uchungu Noel.

Akiwa bado angali ameinama, mara akasikia mwingine akisema: “Hataweza.’’ Walimzungumzia na kumcheka kutokana na ule umaskini wa nyumbani kwao.

Noel alikaa pale bombani kwa kujitenga, baada ya kumaliza kuteka maji aliondoka na kuwapa kisogo. “Huyu ataishia hapo hapo tu,”  waliendelea kumng’ong’a. “Wasomi kibao hawana kazi itakuwa yeye?’’ walimdhihaki.

Noel akiwa njiani akitembea na ndoo yake ya maji mkononi, wazo likamjia: “The success is on my mind.” Noel alikuwa ni mtu wa kushangaza hata alipokuwa akipitia magumu kiasi gani bado aliendelea kuwaza na  kuwa na imani kuwa mafanikio yamo katika maisha yake.

Ilikuwa kama ni sauti ambayo ilikuwa ikimjia katika moyo na akilini. Noel alikwenda moja kwa moja mpaka bafuni, alipofika bafuni akiwa anajiandaa kuvua nguo ili aoge, alianza kulitazama bafu lao namna lilivyokuwa limebomoka upande mmoja, akakumbuka alipotembelea mji mmoja siku moja alikuta mazingira mazuri ya bafu la kuogea, hisia kali zikawa zimeibuka akilini mwake.

Alipofikiria tena wazo lile lile likamjia: “The success is on my mind”’ kisha akapigapiga kifuani kwake huku akiwa anajimwagia maji kwa haraka ya ajabu. Mama yake alikuwa akiendelea kupika chapu chapu kwani njaa iliyokuwa ikimuuma ilikuwa si ya kawaida.

Yule rafiki yake wa shuleni ndiye walikuwa wakikaa naye chumba kimoja wakijisomea mara kwa mara wanapokuwa nyumbani kila jioni. Alipokuwa chumbani kwake aliwaza sana kuhusu Noel hatimaye aliamua kwenda nyumbani kwao Noel kufahamu Noel anaendelea vipi.

Walipokuwa wamepanga chumba cha kujisomea palikuwa si mbali na nyumbani kwao Noel. Punde si punde tu akawa tayari ameshafika nyumbani kwao Noel.

“Hodi mama!’’  Mama Noel akaitikia kwa hraka: “Karibu,’’ huku akiwa jikoni akipika chakula.

Zawadi yeye alikuwa kwake akimbembeleza mtoto wake aliyekuwa akilia. “Shikamoo mama!’’ alisalimia rafiki yake Noel.

“Marahaba,” aliitikia Mama Noel. “Noel yupo wapi mama?” aliuliza yule rafiki yake. “Noeli yumo bafuni anaoga,’’ alisema Mama Noel huku akikaa chini kwa uchovu.

 “Leo sijaonana naye hata kidogo,” alisema rafiki yake Noel akiwa anasogea na kuegemea mtini. “Shule ni ngumu sana?’’ alihoji Mama Noel.