Toleo lililopita tuliishia katika aya isemayo: Akakumbuka alivyokutana naye alivyomwangalia kwa macho ya dharau na maneno machafu, hii ilikuwa baada ya Noel kumwambia yeye ni mwandishi. “Wewe mwandishi gani? Huoni waandishi wengine wanapendeza?’’ alizungumza binti yule kwa madoido na kujikweza kwingi. Sasa endelea…
Noel alijiuliza akilini mwake: “Ni kwa nini alisema hivyo?” Lakini hakupata majibu kwa wakati huo. Noel akawaza na kuibua vitu vingi akilini mwake. Ikiwemo muonekano wake, alifikiria huenda yeye alijiona mwandishi na ana uwezo lakini watu hawakuuona uandishi wake kutokana na mwonekano kwamba haukusadifu kile anachokifanya.
Wakati Noel akiwa anawaza, akakumbuka ile barua pepe aliyoisoma usiku kisha akamsubiri Mariana ili aweze kutoka jikoni amuombe kompyuta yake. Haikuchukua muda mrefu, Mariana akatoka jikoni akiwa ameshikilia chupa ya chai, Noel akaamua kuwasilisha shida yake. “Unaweza kunisaidia kompyuta yako?’’ Mariana akakubali, ila hakujua lengo la Noel lilikuwa ni nini. “Haina shida Noel, kwani ulikuwa unataka kufanya nini?”
Aliuliza Mariana ili kumsaidia zaidi Noel. “Kuna mhariri wa gazeti moja huko Tanzania anahitaji nimtumie makala ndiyo nataka kuandaa,’’ alisema Noel. Mariana akafikiria akienda naye kule chuoni itakuwa sehemu sahihi kuweza kufanya hilo. Mariana akiwa anazungumza na Noel, aliweka chupa ya chai mezani pamoja na vitafunwa tayari kwa kunywa chai.
***
Penteratha binti aliyekuwa mwandishi wa riwaya alikuwa akitoka chumbani kwake. Alivaa begi mgongoni, akafunga chumba chake tayari kuelekea darasani. Masikioni alikuwa ameweka spika za masikio akisikiliza muziki. Akafunga chumba na kuanza kushuka ngazi kuelekea darasani.
Penteratha alikuwa na ndoto nyingi, mara baada ya kumaliza chuo kikuu alikuwa anataka kubaki chini Urusi aweze kuandika vitabu vingi kutokana na mtandao mkubwa aliokuwa ametengeneza katika mji wa Moscow. Akiwa anatembea simu yake ikaita, Penteratha akaipokea.
“Haloo!’’ akasimama kwa umakini kusikiliza aliyempigia. “Ninaitwa bwana… kutoka Bodi ya Vitabu Moscow, tunakuomba utuletee vitabu vyako.” Penteratha akalikubalia ombi hilo alilokuwa ameombwa.
“Sawa, nikitoka darasani nitawaletea,’’ wakamaliza maongezi. Binti huyo akaendelea kutembea lakini siku hii inakuwa njema kwa Penteratha, kwani alitaka kuonana na profesa ili amkutanishe na Noel kwa mara nyingine wakae wawili tu kuzungumza.
Profesa akatoka chumbani kwake akafika sebuleni akamkuta Noel na Mariana wakinywa chai. Siku hiyo mji wa Moscow ulikuwa umetawaliwa na baridi kali isiyo ya kawaida. Ukungu pia ulikuwa umetanda madirishani, ilionekana michilizi ya maji katika vioo vya madirisha hayo yaliyotengenezwa kwa vioo.
“Noel jiandae kikamilifu siku chache zijazo mtihani wa majaribio unaanza,’’ alisema profesa. Noel alikuwa yuko tayari na alikuwa mwenye kujiamini. “Sawa prof.’’ alikubali Noel na hakuonekana kutia shaka.
“Mmi ninaondoka, tutaonana baadaye,’’ alizungumza profesa huku akifungua mlango wa sebuleni na kuondoka. “Leo baridi imezidi,’’ alisema Noel huku akivuta sweta lake na kuliweka vizuri mwilini mwake. “Si baridi tu, leo ninaona hata ukungu upo,’’ alisema Mariana.
“Nataka nianze kuandika makala na kuituma Tanzania,’’ Mariana akampongeza Noel kwa hilo wazo lake. “Safi sana Noel wewe ninachokupendea unadhamira ya kweli, lakini pia wewe ni mpambanaji.’’ Hayo yalikuwa maneno ya Mariana kwa kijana Noel.
“Ni kweli dada Mariana, naamini ipo siku nitafika kule ninapotaka kufika,’’ alisema. Mariana alikaa kimya kidogo kisha akamwambia: “Noel ikitokea hata ukishindwa kupata nafasi chuoni mimi nitakulipia uraia ukae hapa Moscow.’’ Noel aliposikia hilo alifurahi sana. “Litakuwa suala jema Mariana, nitafurahi sana,’’ alisema Noel.
Yule mhadhiri mwenzake Mariana akampigia simu Mariana ili kumuulizia kama atakwenda na Noel. Mariana akiwa amenogewa kunywa chai huku akizungumza na Noel, mara simu ikaita. Mariana akaipokea: “Haloo! Umeshafika chuoni?’’ aliuliza Mariana akihisi atakuwa amefika. “Hapana, bado sijafika, unakuja na yule kijana mwandishi?’’ Mariana akamjibu: “Ndiyo ninakuja naye.’’ Mariana akakata simu wakaendelea kunywa chai.
Siku hiyo nyumbani kwao Noel waliamka mama yake pamoja na dada yake Zawadi wakiwa na matumaini makubwa ya mafanikio. “Mama ninataka nifunge safari niende Dar es Salaam,’’ alisema Zawadi. “Unakwenda kufanya nini?’’ aliuliza mama yake Noel.
Biashara ya kutoa dagaa katika mji wa Mwanza kupeleka Jiji la Dar es Salaam ilishindikana kwa Zawadi kutokana na maelewano mabaya kati yake na mwenyeji wake kule Dar es Salaam.
“Ninakwenda kuchakarika kama mwezi hivi ninataka kupata gazeti niwe ninachora na wakinilipa vizuri,’’ alikuwa akiongea Zawadi huku akionyesha shauku hiyo ya kwenda Dar es Salaam, jiji lililojaa watu wa kila namna.
“Utafikia wapi Zawadi, kwa sababu mwenyeji wako hauna maelewano naye kwa sasa,’’ Mama Noel alitia shaka katika hilo. “Mama, mimi ninamuamini Mungu hata kama ni wapi nitaishi tu,’’ alisema. Maongezi ya Zawadi yalikuwa ni yenye ujasiri.
Familia ya kina Noel pamoja na umaskini lakini walikuwa na vipaji. Zawadi alikuwa mchoraji mzuri na msomaji wa vitabu. Usomaji wa vitabu ulimfanya kujua lugha ya Kiingereza vema na alikuwa ni dada mwenye uwezo mkubwa katika kufikiria na kung’amua mambo. Kutokana na upeo wake wa kujua lugha ya Kiingereza vema, watu walimuona Zawadi kama msomi mzuri ilhali alikuwa ni dada mwenye vidato vinne tu.