Katika toleo lililopita tuliishia katika aya isemayo: Walipokuwa wakiongea Noel akagundua ni Penteratha yule aliyekuwa amekutana naye. “Ina maana Penteratha ni mwandishi maarufu kiasi hiki!’’ alishangaa sana Noel. Sasa endelea …
Penteratha akiwa amekaa mezani akijaribu kutengeneza kichwa cha kitabu, simu ikaita akaiangalia kwa umakini akakuta ni namba iliyokuwa ngeni katika simu yake, akaipokea. “Haloo!’’ alisema kwa sauti ya chini na yenye staha. “Naam! Unaongea na Mhariri wa jarida la Mosco Today.’’ Penteratha akaweka umakini kumsikiliza. “Ndiyo mhariri.’’ Akaacha kazi aliyokuwa akiifanya. Mhariri aliendelea kueleza dhumuni lake hadi kusababisha kumpigia simu Penteratha.
“Mimi na jopo la wahariri wenzangu tumeamua kukuomba uwe ukiandiki hadithi katika gazeti letu,” alisema. “Mimi niko tayari ila hujaniambia nini kilikuvutia mpaka umeamua kunitafuta,’’ alisema Penteratha. Mhariri akamuweka wazi.
“Tulikuwa tunasoma riwaya yako imetuvutia, unaonekana unaijua Afrika.” Penteratha akacheka kisha akamjibu: “Hata hivyo mimi ni Mjamaica kwa kuzaliwa, ila wazazi wangu wana asili ya Afrika, ni wa Ghana.’’
Wakazungumza mengi na mhariri. “Utaanza lini kututumia?’’ aliuliza mhariri. “Mimi nawasikiliza nyie kwanza mnipe mkataba tuelewane malipo nianze kuandaa hizo hadithi.’’ Mhariri akakaa kimya kisha akamjibu: “Nafikiri kesho uje ofisini ili tujadilianea vema,’’ Penteratha alimkubalia na akampa ahadi ya kwenda kama walivyokuwa wameongea. Penteratha akapanga atakapofika ofisi za jarida hilo ataweza kumpigia upatu Noel naye apate nafasi katika jarida hilo.
Noel akaendelea kuandika, Mariana na Meninda wao wakaenda kulala pamoja na baridi kuwa kali, lakini Noel alipanga ni lazima aweze kuandika karatasi kadhaa amalize na hatimaye aweze kufikisha mbali wazo la kitabu chake. “Mungu nisaidie niweze kufika mbali, niwe mwandishi nguli Afrika,” aliongea kimoyo moyo Noel.
Aliendelea kuandika huku akiamini bila mchungaji yeye asingeweza kufika pale alipo, alihisi kulikuwa na kusudi ambalo Mungu alipanga yeye kuweza kukutana na mchungaji.
***
Ulikuwa usiku wa saa mbili kwa saa za Afrika Mashariki, Mchungaji akiwa amemleta Mama Noel hadi nyumbani kwake kwa gari lake. “Mchungaji karibu ndani usiondoke bila kuweka baraka,’’ alisema Mama Noel huku akiwa anaingia ndani. “Asante Mama Noel,’’ aliingia mchungaji ndani akamkuta Zawadi akiwa amewasha taa huku akiwa bize anachora. “Zawadi mpishe mchungaji,’’ alisema Mama Noel. Huko walikokuwa wametoka Mama Noel alipewa maneno ya faraja na mchungaji akawa ameona kama mambo yote ulimwenguni yanawezekana.
Zawadi alimpisha mchungaji. Lakini mchungaji alikuwa hajisikii vema kwa binti Zawadi kutolewa pale kwani alihisi alisitisha jambo lake alilokuwa akifanya. “Lakini Mama Noel umemkatisha binti jambo lake analofanya,’’ alisema mchungaji. Mama Noel alicheka na kuona jambo la kawaida. “Hapana mchungaji, yeye mwenyeji inabidi ampishe mgeni,” alisema Mama Noel. Mchungaji alikaa kimya.
Zawadi alimsalimu mchungaji kisha akaendelea na alichokuwa akikifanya. Alikuwa hafanyi kitu kingine bali alikuwa akichora michoro yake ili aweze kuituma gazetini.
Wakati alipokuwa akichora kumbe mchungaji alikuwa akiangalia kwa umakini namna Zawadi alivyokuwa akifanya. “Zawadi muandalie mchungaji chakula, unafanya nini lakini!’’ alisema Mama Noel akiwa anamshangaa Zawadi binti yake. Mtoto wa Zawadi alikuwa amelala katika godoro dogo.
“Hapana, Mama Noel muache binti, kuna kazi naona anaifanya ni nzuri,’’ alisema mchungaji. Mama Noel akaamua kufanya hekaheka za kumuandalia mchungaji chakula. Zawadi akiwa anachora, mara Fatuma akampigia simu. Zawadi akaitazama kisha akaipokea. “Fatuma za muda.’’ Fatuma akaitikia na kumwambia:
“Njema, huyu mkurugenzi wa redio ananisumbua nimpatie namba zako uweze kuwaunganisha na Noel waone nini cha kufanya.’’ Zawadi akafikiria kwa sekunde kadhaa kisha akamjibu: “Sawa Fatuma hakuna shida,’’ kisha akakata simu na kuendelea kuchora. Zawadi akaguna na mchungaji akawa amesikia.
“Binti unaguna nini?’’ aliuliza mchungaji huku akiwa anatengeneza miwani yake. Zawadi alikaa kimya kisha akasema kile alichokuwa ameambiwa na Fatuma. “Eti mkurugenzi wa redio anamtafuta sana Noel.’’ Aliposema hivyo mchungaji akakaa kwa umakini kisha akauliza: “Kwa nini anamtafuta ilhali walishamfukuza?’’ aliuliza mchungaji huku akiwa anashangaa.
“Wanasema kipindi alichokuwa anakifanya Noel kimepwaya, anahitajika,” mchungaji akacheka kisha akavua miwani yake na kumwambia: “Hawakujua hilo kwamba kipindi kitapwaya?’’
“Mchungaji hawa ndio wanaua vipaji vya watu,’’ alisema Zawadi akiwa anaendelea kuchora. “Ni kweli wamempotezea muda sana Noel, hawakuwa wanamlipa na atakuja kufanya mambo makubwa watamhitaji zaidi,’’ yalikuwa maneno ya mchungaji akimwambia Zawadi. Mama yake Noel alifika na birika lenye maji kisha akamnawisha mchungaji mikono kwa ajili ya kula chakula.