Katika toleo lililopita tuliishia katika aya isemayo: “Idara ya uchapishaji wapo, na Mkurugenzi Caves yupo?’’ aliuliza Penteratha. Alikuwa amedhamiria kumpigania Noel, kijana mwenzake mwenye asili sawa na ya kwake. “Yupo, muone,’’ meneja wa machapisho alimruhusu Penteratha kuingia kuonana na Mkurugenzi Caves. Sasa endelea…
***
Noel na profesa walifika nyumbani, baridi nayo iliendelea kuwa kali. Yoranda, mfanyakazi wa ndani wa profesa alikuwa akifanya shughuli ndani, akaamua kutoka nje kuwafungulia profesa pamoja na Noel mlango.
“Karibuni,’’ alisema Yoranda huku akiwa anafungua mlango. “Asante,’’ walijibu kwa pamoja Noel pamoja na profesa. Lakini Noel mawazo yake yalikuwa katika kuandika kile kitabu ambacho alitaka ndani ya muda mfupi awe amekimaliza kukiandika.
Noel akafika na kukaa mezani, akafikiria kuhusu Penteratha aliyekutana naye, binti mwenye umri mdogo sawa na wake. Lakini alikuwa amechapisha riwaya zake mbili. “Inawezekana, mbona Penteratha si raia wa Urusi lakini ameweza kuandika na kuchapisha vitabu hapa hapa?’’ Alikuwa amekaa mezani akifikiria. Akaamua kuchukua daftari lake na kalamu na kuanza kuandika huku akijituma kwa juhudi. Profesa yeye alikuwa ameingia chumbani kwake.
Punde tu Meninda naye akawa amefika, akapaki gari lake na kulifunga kwa funguo zake kisha akaingia ndani. Alisukuma mlango polepole akamkuta Noel akiandika.
“Mmh! Huyu kijana atakuja kufanikiwa sana kwa anachokifanya,’’ aliwaza Meninda huku akitembea kuelekea mezani alikokuwa Noel. Noel alikuwa hajali, tangu mlango ulipokuwa ukifunguliwa mpaka Meninda alipoingia na kutembea hadi mezani kwake. Noel yeye alikuwa makini na kile alichokuwa akikifanya mezani, hakutaka kutangisha akiri yake.
Meninda akamgusa Noel begani kisha Noel akashituka na kugeuka: “Mmm! Kumbe dada Meninda, za kazi?’’ Meninda akaitikia kwa tabasamu: “Salama Noel, naona uko makini na kuandika hata unioni.’’ Noel akacheka huku akiwa anakuna kichwa chake.
“Yaani dada yangu ninataka nikiandike hiki kitabu kwa weledi mkubwa na nikichape katika kompyuta yako,’’ alisema. Meninda akamkubalia, wala hakutia shaka juu ya hilo. “Sawa Noel, tena nitakichapa mimi mwenyewe,’’ alisema. Noel alikuwa akifurahi kuona Meninda akionyesha kukubali. Meninda akaingia chumbani kwake kubadili nguo, Noel akaendelea kuandika kitabu chake.
***
Muda ulikuwa ukiyoyoma. Ilikuwa yapata saa mbili kasoro, Mariana akaamua kuahirisha kipindi chake, badala yake akatoa zoezi la kufanya.
“Niende nyumbani nikapumzike?’’ aliwaza mwenyewe akilini mwake akiwa anafungua gari lake. Akilini mwake alikuwa akiwaza kuhusu Noel. “Nikaongee na Noel kesho nije naye huku, hata kama atakosa nafasi ni vema abaki hapa Moscow,’’ yalikuwa mawazo ya Mariana juu ya Noel.
Wakati Mariana akiwa anawaza hivyo, binti Penteratha alikuwa amehitimisha mazungumzo yake na mchapishaji wake, kile alichokuwa amekiwasilisha kiliweza kukubaliwa. Penteratha akaamua kumpigia simu profesa usiku huo akiwa anatembea kurudi chuoni.
Profesa alikuwa chumbani, akasikia simu yake ikiwa inaita, akaichukua na kuipokea. “Nam Penteratha!’’ aliongea profesa kwa sauti ya chini. “Profesa nilikuwa ninakupa mrejesho wa ile kazi uliyonipa, nimeongea na mchapishaji amekubali.’’ Profesa akashukuru kwa ukarimu na upendo aliouonyesha Penteratha.
“Sasa inatakiwa umlete Noel hapa kisha ataonyesha kazi yake ikiwa kwenye nakala laini,” alisema. Aliendelea kutoa utaratibu kama alivyokuwa ameambiwa na mchapishaji wake. Akazungumza kwa kifupi kuhusu hilo, kisha Penteratha akakata simu na kuendelea na safari ya kurudi chuoni.
Profesa akatoka chumbani hadi sebuleni kumwambia Noel kilichokuwa kikiendelea kwa Penteratha. Profesa akamkuta Noel akiwa anaandika.
“Noel, Penteratha ameweza kukutafutia kampuni ya machapisho.’’ Noel akafurahia kisha akamuuliza: “Wapi, hapa hapa Moscow?’’ Profesa akamkubalia. “Ndiyo, ninafikiria maliza kuandika tukiweke katika nakala laini ili ukawaonyeshe kitabu chako,’’ alisema profesa. Wakati wakiwa wanaongea, Meninda naye kumbe alikuwa akiwasikiliza, akatoka chumbani akiwa mwenye furaha na bashasha, akafika na kusimama akitabasamu huku akimtazama Noel.
***
Ni muda wa saa mbili na nusu Mariana akawasili nyumbani, akafika getini akakuta tayari mlinzi alishafunga geti. Baridi ilikuwa kali sana, mvua nayo ilikuwa ikitiririka kwa matone. “Mmmh!’’ akaguna Mariana, kisha akatoka ndani ya gari na kwenda kusimama getini. Akanyoosha mkono wake na kuanza kubonyeza kengele ili aje kufunguliwa na aweze kuingiza gari lake ndani.
Sebuleni alikuwa amekaa Noel peke yake, Meninda alikuwa chumbani kwake, profesa naye alikuwa chumbani kwake. Noel alikuwa amebakia peke yake akijitesa kuumiza akili yake kuandika wazo la kitabu chake alichokuwa akikiandika. “Kengele inapiga alamu, ninahisi kuna mtu nje,’’ aliwaza Noel, kisha akasitisha kuandika na kuifikiria kengele iliyokuwa ikipiga alamu.
Meninda akiwa chumbani kwake alikuwa amesikia kengele iliyokuwa ikiita, akatoka hadi sebuleni. “Huyu atakuwa ni Mariana, si mwingine,’’ alisema Meninda huku akienda kufungua mlango wa kutoka nje ili kwenda kumfungulia geti. “Dada Meninda usiende mwenyewe usiku huu, acha nikusindikize,’’ alisema Noel huku akinyanyuka kutoka kwenye kiti alipokuwa amekaa.