Katika toleo lililopita tuliishia katika aya isemayo: Fatuma muda huo alikuwa yumo njiani na Zawadi dada yake Noel wakitembea kuelekea ofisi za ofisa utamaduni wa mkoa ili kuangalia namna ya kusajili kampuni yao ya mitindo waliyokuwa wanataka kuianzisha. Sasa endelea…
“Zawadi, tutafanikisha, hata mbuyu ulianza kama mchicha,’’ alisema Fatuma huku wakiwa wameshikilia bahasha iliyokuwa na nakala zao. “Ni kweli Zawadi,’’ alisema Fatuma. Simu ikawa inaita, Fatuma akaitoa na kuangalia akakuta ni mkurugenzi. “Mmh! Leo bosi wangu wa zamani amenikumbuka ana nini!’’ Akaamua kuipokea. Mkurugenzi akamsalimia kwa furaha na bashasha kisha akaelezea shida yake aliyokuwa nayo.
“Unaweza kumpata Noel, tuna shida naye,’’ alisema mkurugenzi. “Noel sijui yuko wapi, nina siku nyingi sijaonana naye,’’ alisema. Mkurugenzi akazidi kuingiwa wasiwasi. “Marafiki zake je, au kijiwe atakachokuwa akipendelea kwenda napo hupajui?’’ Fatuma aliendelea kusema ukweli: “Kwa kweli sipajui.’’ Mkurugenzi akakata simu.
Zawadi akamuuliza Fatuma: “Fatuma ulikuwa ukiongea na nani?’’ aliuliza hivyo baada ya kusika jina la mdogo wake Noel likitajwa. “Nilikuwa nikizungumza na mkurugenzi wa redio niliyoacha kazi,’’ alijibu Fatuma huku wakiwa wanatembea. “Noel uliyekuwa ukimzungumzia ni yupi?’’ aliuliza Zawadi ambaye hakutaka kukurupuka. “Nilifanya kazi na kijana mmoja mdogo tu kwangu pale redioni ana kipaji sana, alibuni kipindi cha redio ndiyo ninaona wanamuulizia.’’ Zawadi alitabasamu kisha akaguna, Fatuma akashituka kwa mguno alioutoa Zawadi.
“Mbona umeguna Zawadi?’’ aliuliza Fatuma. Zawadi alikaa kimya kwa dakika kadhaa kisha akamjibu Fatuma: “Nimeamini dunia ni ndogo sana.’’ Fatuma akawa bado hajaelewa alichokuwa akimaanisha. “Kwa nini unasema hivyo?’’ aliuliza. Zawadi akamuelezea ukweli ambao wote wawili walikuwa hawaujui. “Noel unayemzungumzia ni mdogo wangu mimi na sasa ana siku kumi yupo nchini Urusi,” alisema.
Maneno ya Zawadi yalimshitua Fatuma, akasimama na kumuuliza Zawadi: “Unasema ukweli?’’ Akiwa haamini kama ilikuwa kweli. “Fatuma, Noel ni mdogo wangu ninapoishi kule mtaani ndiko nyumbani kwao pia,’’ alisema Zawadi, lilikuwa ni jambo la kushangaza kwa Fatuma.
“Noel yuko Urusi! Alipata vipi nafasi mpaka akaenda huko?’’ aliuliza Fatuma. Ilimpasa kuamini kwa kuwa alikuwa na muda mrefu wakiwa hawajaonana na Noel mjini. “Mdogo wangu alipata wafadhili Warusi na akaenda kusoma huko,’’ alikuwa akielezea vema Zawadi, dada yake Noel.
Fatuma alianza kufikiri kwa mawazo chanya juu ya Noel. “Kama amekwenda Urusi kwa ninavyojua kipaji chake atakuwa mwanahabari mzuri siku za baadaye,’’ alisema Fatuma. “Nimemwambia mama, Noel atafanya vitu vikubwa baadaye,’’ alisema.
Walikuwa wakizungumza huku wakitembea taratibu. Fatuma alifikiria sana. “Shahada yake ya kwanza anasomea Urusi dah! Noel ametoka tayari,” alifikiria katika akili yake pasipo kumwambia Zawadi. Fatuma alikumbuka siku za nyuma Noel alikuwa akizungumza kama utani, akivuta kumbukumbu za maneno ya Noel kipindi kimoja walipokuwa wamekaa naye alivyokuwa akimwambia: “Dada Fatuma ninataka niwe mwanahabari mwenye utofauti.’’ Anakumbuka Noel alivyokuwa akizungumza kwa kumaanisha, lakini yeye akampuuza na kuona hana maana kwa wakati huo, hasa alipoona Noel akitokea maisha ya dhiki na yasiyo na matumaini. Alihisi huenda yalikuwa ni matamanio ya kijana Noel ambayo yangebaki kuwa katika maneno na si vitendo.
***
Ofisi ya gazeti alilokuwa akiandikia Noel zilikuwa katika Jiji la Dar es Salaam. Siku hii wao walikuwa wakifanya kikao cha bodi ya wahariri, wakiwa wamefungua kikao na kuzungumza mambo mengi kuhusu gazeti lao, ikawa ni nafasi ya mhariri mkuu kuzungumza.
“Jamani, kwanza sioni makala za yule kijana, mmezisitisha?’’ aliuliza mhariri, watu wakawa wakitazamana hawakujua aliyekuwa akimzungumzia alikuwa ni nani. Hakuwa mtu mwingine bali alikuwa ni Noel. “Nani, Noel?’’ alisema mhariri aliyekuwa akihakiki makala za Noel.
“Ndiyo, sioni mkichapisha makala zake, kwa nini?’’ alizungumza huku akionyesha hali ya kusikitika. “Hatumi siku hizi huyo kijana,” alisema mhariri aliyekuwa akihakiki makala za Noel. “Kwani si ulikuwa na barua pepe yake, hebu mwambie aendelee kutuandikia makala,’’ alisema. Alipomaliza kuzungumza, mara mhariri wa Noel wa makala zake akampigia simu, lakini simu haikupatikana.
Akafikiria, kisha akanyanyuka kutoka kwenye kiti na kwenda kutazama barua pepe ya Noel ili amtumie huko ujumbe wa maandishi kupitia barua pepe yake ili Noel aendelee kutuma makala zake.
“Ngoja nimtumie barua pepe, ninaona hapatikani,’’ alisema yule mhariri wa makala alizokuwa akituma Noel. Walikuwa hawajawahi kuonana hata siku moja na Noel, Noel alikuwa hajawahi kufika katika ofisi za gazeti hilo. “Fanya mawasiliano naye, makala zake ninazipenda, zimepangika na anachambua vema,’’ aliongeza mhariri mkuu. Sura ya Noel waliijua kupitia picha aliyokuwa akiambatanisha katika makala zake.