Katika toleo lililopita sehemu ya kumi tuliishia katika aya isemayo: “Mimi niko tayari,’’ alisema Noel kisha wakasalimiana na profesa. Maisha ya Moscow Noel alianza kuona kuwa ni mazuri, ambayo yangeweza kumfaa katika uandishi wake. Sasa endelea…
Meninda akiwa njiani akiendesha gari kuelekea ofisini alikuwa amefungulia muziki katika gari lake, barabara za mji wa Moscow zilikuwa nzuri na mandhari pia ilikuwa nzuri. Meninda alikuwa anawaza sana juu ya Noel: “Yule kijana ana uwezo, kwanini ashindwe kuwa tajiri hata kama elimu yake bado si ya chuo kikuu?’’
Alijiuliza mwenyewe akilini akiwa anaendesha gari akipanga mara baada ya kumaliza kikao ataweza kutenga muda afanye maongezi na mtu wa kitengo cha maandiko na machapisho ili kuona anawezaje kumsaidia Noel kupata nafasi katika eneo hilo.
Mariana akiwa anahangaika kuandika, mara simu yake ikaita na aliyekuwa akipiga alikuwa si mtu mwingine, bali ni yule mhadhiri mwenzake ambaye walikuwa wakiwasiliana usiku, Mariana akaipokea.
“Haloo!’’ aliongea kwa sauti ya chini. “Ndiyo Mariana, sasa uje na yule kijana usimuache,’’ alisema yule mhadhiri mwenzake Mariana.
“Leo kuna sehemu wanakwenda na baba huenda kesho ndiyo itakuwa vema zaidi,’’ alisema Mariana. Yule mhadhiri mwenzake akasikitika sana juu ya suala hilo, lakini ikawa haina budi yeye kukubaliana na kile alichokuwa amekisema Mariana.
Akiwa anaongea na simu, Noel alikuwa pembeni amekaa akifungua daftari lake, profesa naye alikuwa akiandika kitu katika tanakilishi yake.
Noel naye hakusita, akamfuata Mariana pale alipokuwa amekaa kisha akamuonyesha kile alichokuwa anakiandika. “Mariana, ona hiki ni kitabu changu nakiandika.’’ Mariana akachukua na kuanza kusoma kwa umakini kama ukurasa mmoja tu. Noel yeye alikaa kimya kusikiliza nini atasema Mariana. Kwanza aliamini Mariana ni msomi; pili, alijua anaweza kushauri kitu kiongezeke katika hayo maandiko yake.
“Ni nini hicho Noel, kitabu?’’ aliuliza profesa akiwa anaacha kuandika katika tanakilishi yake na kumwangalia Noel. “Ndiyo, ni kitabu nilichokuwa naandika tangu nilipokuwa nchini Tanzania,” alisema Noel, kisha profesa akapata ushawishi wa kuangalia alichokuwa akiandika Noel.
“Mariana ukimaliza nipatie na mimi nipitie nione alichokuwa akikifanya Noel,” alisema profesa. Mariana kila alipokuwa akisoma alijikuta kuhamasika zaidi na kile kitu alichokuwa amekiandika Noel. Alipomaliza akampa baba yake aweze kukiangalia.
Mariana alikaa kimya kwa dakika kadhaa kisha akamuuliza Noel: “Noel umefikiria nini mpaka kuandika hivi?’’ Noel alikuwa kijana anayeweza kuelezea mawazo yake vizuri, si kwa kuandika pekee, bali hata katika maongezi.
“Niliwaza sana juu ya Afrika, bara letu namna mabepari wanavyochukua rasilimali zetu,’’ aliongea Noel akiwa ametulia. Wakati alipokuwa akielezea, Mariana alikuwa akitikisa kichwa kumkubalia kile alichokuwa akikisema.
“Kwa hiyo ni kama ujumbe unaoutoa kwa bara lako?’’ Noel alimkubalia. Profesa alikuwa amenogewa na kusoma kile alichokuwa ameandika Noel akiwa haamini kama Noel ndiye mwenye uwezo wa kutiririsha mawazo namna ile.
“Dah! Wewe Noel sijui niseme nini, sasa baada ya kuandika ulitaka kukiuza, au?’’ aliuliza profesa. “Ninataka kukiuza nipate pesa lakini pia kitumike kwenye mitaala ya elimu,’’ alisema Noel.
Profesa alikuwa amefikiria zaidi ya vile Noel alivyokuwa akiwaza, kisha naye akamwambia kitu kizuri cha kufanya.
“Nafikiri kiandike, mimi nitafanya kila linalowezekana ukichapishe kwanza.’’ Neno hilo la profesa lilimfanya Noel awe mwenye furaha. “Noel wewe subiri, tutaandika vitabu vingi na vitakuletea pesa,’’ alisema Mariana.
Kwa namna alivyokuwa akiahidiwa, Noel alijikuta akifurahia maradufu na kuona kama alichelewa kufika Moscow.
“Karibuni mesini,’’ alisema mfanyakazi wa ndani akiwa anawakaribisha katika mesi. “Sawa Yolanda, tunakuja,’’ alisema profesa. Mariana akanyanyuka na kuelekea mesini kunywa chai. Noel naye akafuata. Profesa alibaki kuhitimisha kitu alichokuwa akifanya huku akimuwazia Noel kwa mapana zaidi. “Lakini huyu kijana nimegundua ana kipaji cha hali ya juu sana,’’ aliwaza profesa kisha akatoka kwenda pia mesini.
Wakiwa wanakunywa chai, Noel alikuwa anawaza kuhusu kuandika vema kitabu chake. Malengo yake yalikuwa ni kutoa kitabu kikubwa kwa umbo na ujumbe pia. Noel aliiona familia ya profesa haikuwa na mama mwenye nyumba, kwa maana ya mke wa profesa. Kitu hicho kilimpa hamasa ya kutaka kuuliza swali ila akashindwa.
“Noel kesho nitakukutanisha na mtu,’’ alisema Mariana huku akiwa anakunywa chai. “Noel una kipaji, ukiongeza na elimu ndiyo kabisa, utafikia viwango vikubwa vya uandishi,” alisema profesa.
Akawa ameamsha hisia za Noel, akawa anaomba Mungu kimoyo moyo afanikiwe kusoma katika chuo chochote pale mjini Moscow. Noel alikuwa anawaza namna atakapokuwa amefikia mafanikio makubwa ya uandishi atarudi Afrika kuwasaidia Waafrika wenzake kufikia ndoto zao.
“Na ni lazima siku moja nihojiwe BBC au VOA,’’ alikuwa akinywa chai huku akiwaza mwenyewe akilini mwake.
Ulikuwa muda wa saa tatu asubuhi, Meninda akiwa amewasili ofisini kwake, purukushani zinakuwa nyingi. Meninda kama bahati akakutana na mhariri wa lile jarida lao la wakimbizi. Meninda akamsimamisha: “Derek!’’ Kisha Derek akaitikia huku akisimama na kukatisha safari yake alikokuwa akielekea.
“Nilikuwa na maongezi ya kina na wewe, sijui utakuwa na muda tuonane ofisini kwako?’’ alisema Meninda kwa nidhamu. “Baada ya saa moja uje tuongee,’’ akamkubalia kisha wakaachana kila mmoja akiendelea na mambo yake. Meninda akaenda ofisini kwake. Ofisini kwake walikuwa wakikaa watu wawili, yeye na mtu mwingine, raia wa Ujerumani.
Meninda alipofika akamkuta yule Mjerumani akiwa amekaa akipanga kablasha zake. “Meninda karibu,’’ alimkaribisha kwa furaha akiwa mwenye tabasamu. “Asante,’’ alijibu Meninda huku akikaa katika kiti. Meninda alikuwa akimuwazia Noel ilhali hakuwa anajua hata historia ya maisha yake kwa undani. Zaidi aliingiwa na moyo wa kufanya kitu kuhusu Noel hasa kutokana na uandishi wake.
***
Baada ya saa moja kupita; Noel, Mariana pamoja na profesa wakawa wamemaliza kupata kifungua kinywa. Profesa akamuaga binti yake Mariana. “Sisi tunaondoka, tutarudi baadaye,’’ alisema profesa. Mariana alimkubalia: “Sawa baba, mimi pia ninataka kuondoka, punde tu nitakuwa na kipindi.’’
Alikuwa akizungumza Mariana huku akiwa anaandika pointi za kitu alichokuwa akitaka kuandika. Profesa akaondoka akiwa ameambatana na Noel huku wakiwa wamevaa makoti mazito katika miili yao. “Noel, ndiyo tunakwenda chuoni sasa hivi,” profesa alimwambia Noel. Naye alijibu: “Sawa profesa.”
Walikuwa wanatoka nje, walipofika mlangoni profesa akashika kichwa kisha akamwambia Noel: “Nimekumbuka pale chuoni kuna wahadhiri ni waandishi, pengine unaweza kuonana nao.’’
Noel akakumbuka magazeti yake. “Prof. niende na magazeti yangu?’’ aliuliza Noel kwa hekima na upole. “Ndicho nilichokuwa nikimaanisha,’’ alisema profesa.
Noel akarudi ndani kwa haraka kisha akaenda hadi chumbani kwake alikokuwa ameweka vitu vyake. Akafika na kupekua kisha akachukua magazeti yake aliyokuwa hayaachi. “Noel ulisahau nini?’’ aliuliza Mariana huku akiendelea na shughuli zake. “Nilikuwa nimesahau magazeti yangu,’’ alisema. Aliposema vile Mariana akampa wazo.
“Tunza hayo magazeti yako yanaweza kukusaidia muda wowote,’’ alisema Mariana kisha Noel akamkubalia. Profesa yeye alikuwa nje akimsubiri Noel. Punde Noel akatoka akiwa ameshikilia magazeti yake. “Safi Noel, unajua hizi ni CV zako pia,’’ alisema profesa huku wakitembea na kuingia ndani ya gari.
Wakiwa ndani ya gari, Noel alikuwa akifikiria kwa mapana maisha ya pale nyumbani kwa profesa. “Dah! Prof. ana maisha mazuri,’’ alikuwa akiwaza akilini mwake.
Alipoangalia kushoto, aliona kuna eneo kubwa la kupaki magari likiwa limebaki gari moja katika eneo hilo la kuegesha magari. Noel akafikiria moja kwa moja kuwa lilikuwa gari la Mariana. Profesa alianza kuongea na Noel mambo kuhusu Afrika hususan nchi ya Tanzania.
“Noel, lakini nyumbani niliambiwa unaishi na mama,” Noel alimkubalia. “Ndiyo, ninataka nihakikishe ninamtoa mama katika shida alizonazo,’’ alisema Noel katika hali ya uhalisia usioweza kufichika.
“Na itakuwa hivyo, Mungu atakusaidia Noel’’, alisema profesa maneno ya kumtia moyo kijana Noel huku akiwa anaendesha gari kulitoa nje ya geti. Kwa maongezi profesa alikuwa ameshafahamu Noel ni mtu wa kutoka mazingira ya aina gani, ukiachia mbali alikuwa ameshapewa historia ya Noel tangu zamani alipokuwa akizungumza na mchungaji.
“Noel, mimi naona utafanya mambo makubwa, wala usikate tamaa,” alisema profesa. Noel alikuwa amekaa kwa huzuni akiwa na mawazo tele, maana alikuwa akifikiria kuhusu umaskini aliouacha Tanzania. Umaskini ulikuwa ukimpa fikra nzito, hasa hali aliyokuwa ameiacha katika familia yake.