Mafanikio, changamoto
Chuo Kikuu Huria
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Profesa Elifas Bisanda, amezungumza na Gazeti la JAMHURI kuhusu historia, mafanikio, changamoto na hatima ya chuo hicho. Mwandishi MANYERERE JACKTON, aliyezungumza naye, analeta maelezo ya Profesa Bisanda neno kwa neno. Endelea…
Umuhimu wa kozi ya ‘foundation’
Kozi ya foundation ilianzishwa mwaka 1994/1995 na iliwawezesha wale ambao hawana sifa kwa maana kwamba hawana A level, hawana diploma, lakini labda wana certificate wakati huo au diploma ambazo hazikuwa na ufaulu wa kutosha wakawapa kozi ambayo iliwanyanyua na wakapata sifa ya kudahiliwa kusoma shahada.
Kwa namna hiyo chuo kimeweza kuingiza wanafunzi zaidi ya 26,000 katika mfumo wa elimu ya juu. Si wote waliomaliza. Waliomaliza ni kama 7,000 tu na hiyo naeleza jinsi nature ya elimu huria ilivyo. Elimu huria ilivyo ni mlango mpana – wanaingia watu wengi, lakini wanaopita ni wachache. Na ndicho kitu kinachodhibiti ubora kwamba watu wasifikiri elimu huria ukiingia tu unatoka – kwamba vyovyote vile ukiingia unatoka, ukiwa kilaza unatoka, hapana.
Sisi tuna chujio kwenye kutoka – kwenye kuingia tunapaswa kuwa na mlango mpana, lakini kwenye kutoka tunabana; kwamba lazima uweze kukidhi vigezo vinavyotakiwa ndipo uweze kupata shahada.
Hiyo ni sehemu ya kwanza. Sehemu ya pili, mwaka 2005 ilipoingia Serikali ya Awamu ya Nne, Mheshimiwa Lowassa akiwa Waziri Mkuu walianzisha programu ya MES – Shule za Sekondari za Kata – kwamba kila kata iwe na shule ya sekondari. Kwa hiyo kukatokea upungufu mkubwa sana wa walimu. Kukawa na uhaba mkubwa wa walimu wa kufundisha shule za kata. Walimu wote waliokuwa shule za msingi waliokuwa na diploma wote wakahamishiwa kwenye shule za sekondari. Kwa hiyo ikaonekana kwamba shule za msingi zimebakiwa na walimu wenye certificate.
Na sisi kama chuo tukawasiliana na wizara tukawambia jamani mnajua ubora wa elimu unaanzia chini. Ubora wa nyumba ni msingi, sasa kama tumeporomosha ubora wa msingi ni kwamba tutapata shida huku chini. Kwa hiyo wizara ikaturuhusu kuanzisha programu ya diploma ya ualimu wa shule ya msingi. Tukaandaa mtaala mwaka 2007 tukaupeleka TCU (Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania), mwaka 2008 ukapata ithibati ya TCU. Kwa hiyo tukaanza Diploma in Primary Teachers Education. Ndiyo diploma ya kwanza ya walimu wa shule ya msingi.
Diploma zilikuwepo. Zote zilikuwa ni diploma za walimu wa sekondari. Mpaka sasa bado tunapambana Utumishi (Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma) kule kwa sababu kuna dhana kwamba hii diploma ya ualimu wa msingi haipo sawa na diploma ya walimu wa sekondari. Diploma ni diploma tu. Unaweza hata ukawa na diploma ya walimu wa chekechea. Unaweza hata ukawa na digrii ya ualimu wa chekechea – ni digrii, lakini kule Utumishi waliohitimu bado wanapata shida sana kupata promosheni kwa sababu wanasema haimo kwenye mfumo wa Utumishi.
Watu wanaomaliza diploma wanalazimika kusoma digrii na hiyo si kitu kizuri. Sisi tumefanya sehemu yetu kama taasisi ya elimu – tumefanya sehemu yetu, taasisi zinazofuata kama wizara na Utumishi wao nao wana sehemu yao ya kufanya – kuhakikisha hizi qualification zinatambulika. Tumekwisha kuwaandikia wizara, tumewapelekea nyaraka zote kuhusu hiyo diploma, kwamba hii diploma ina ithibati ya NACTE, maana tulipoianzisha NACTE nao baadaye wakaanzisha diploma yao na bahati mbaya ilikuwa inafundishwa kwa Kiswahili, sisi ya kwetu ilikuwa inafundishwa kwa Kiingereza.
Ndiyo hii waliichukia UDOM na vyuo vingine baadaye serikali ikaondoa. Lakini sisi pia diploma yetu ni kwa walimu walio kazini. In service, hatuchukui mtu anayetoka shule hata kama amemaliza kidato cha sita hatuchukui. Tunataka lazima awe ameshakuwa mwalimu kwa maana mafunzo ya msingi ya ualimu tayari anayo na angalau ameshafanya kazi miaka miwili kama mwalimu, kwa hiyo anakuja kuongeza – na hii anaisoma kwa masafa – kwa maana anasoma yuko kazini. Haiondoi mwalimu darasani. Siyo diploma nyingine mwalimu anaomba likizo ya miaka miwili kwenda kusoma diploma – shule inabaki haina walimu.
Sisi diploma yetu ni win win – huku mwanafunzi anasomeshwa, huku mwalimu naye anasoma. Raha yake ni moja, raha ya kusoma kwa mfumo huu ni kwamba unapojifunza jambo jipya unalitekeleza pale pale. Husubiri mpaka unakapohitimu. Nikikufundisha concept mpya ya kufundisha ya saikolojia ya watoto unaenda kufundisha na kuona saikolojia ya watoto.
Walimu wengi wanafikiri kiboko ndicho watoto wanasikiliza, kumbe kiboko kinawafanya wanakuwa sugu. Unaweza ukawafanya watoto wakawa na nidhamu bila kiboko, bila fimbo, bila uzio. Nilitembelea shule moja anasoma mtoto wangu pale Marian Boys, I was shocked kwamba shule haina uzio na hakuna mtoto anayetoroka. The fence is in their mind. Unaona, wamejenga uzio ndani ya vichwa vyao, kwa hiyo hakuna anayetoka. Mtu anafikiri ujenge ukuta, ushike fimbo, hakuna. Ni saikoloji. Mapadri wanajua saikolojia, wamejenga uhusiano mzuri sana na majirani pale. Ukitoroka tu wanampigia simu padri. Mtoto wangu alikuwa ananisimulia kwamba ukitoroka, ukirudi unakuta wanakusubiri, wameshampigia simu padri.
Na sisi tukaleta programu mpya, na mpaka sasa tumeshafundisha walimu zaidi ya 2,800. Walimu waliopata stashahada ya ualimu wa shule ya msingi zaidi ya 2,800 wameshaingia kwenye ajira ya serikali na wengi wao wamejiendeleza kwa kwenda kusoma digrii baada ya kuona Utumishi hawawatambui, kwa hiyo wakaona ni bora wajiongeze, na baada ya kuongeza digrii sasa wanawatambua. Wapo wengine wana-struggle watambulike.
OUT ilivyoenea
Tulipoanza azima yetu ilikuwa kuwa na kituo kwa kila mkoa, kwa hiyo mikoa iliyokuwapo ilikuwa 21 pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba. Tukafungua vituo vya mikoa. Mkoa wa Dar es Salaam tukawa na vituo vitatu. Kwa jumla tukawa na vituo 25, lakini baadaye serikali ilipoongeza mikoa (Songwe, Njombe, Geita, Katavi na Simiyu) tukawa na vituo 30. Kwa hiyo tuna vituo 30 vya mikoa (Regional Centers).
Lakini kwa upande wa mitihani tukagundua baadhi ya wilaya ziko mbali sana na mikoa. Kutoka wilayani kwenda mkoani ni mbali zaidi kuliko mkoa hadi mkoa! Kwa hiyo tukaamua kufungua vituo vya mitihani katika baadhi ya wilaya hasa zilizoko pembezoni. Nyingi tumezifungulia vituo.
Kwa mfano wilaya kama Ngara tumeifungulia kituo cha mtihani. Nkasi, Serengeti, Longido, Karatu, Mbulu, Mbinga, Makete, Tunduru, Masasi, Mafia, Pemba (waliomba kituo cha pili).
Kwa ndani, maeneo mengine yako katikati kama Mafinga kuna kituo cha mtihani, Tukuyu, Kasulu, Kibondo, Chato kwa sababu mitihani inapita kwenda Bukoba tukaona kuwe na kituo na kuna wanafunzi wengi pale.
Hapa katikati tuna Mpwapwa, Korogwe, Mwanga, Kondoa, Kiteto, Ifakara, tunafikiria Mahenge. Kwa hiyo utaona tumeingia wilaya nyingi – nafikiri wilaya 30 hivi ambazo tuna huduma za mitihani.
Bahati nzuri tumebadilisha mfumo wetu wa usambazaji mitihani.
Mabadiliko mfumo wa mitihani
Zamani tulikuwa tunaipeleka (mitihani) kwa magari na mapolisi – ilikuwa ni operesheni kubwa sana. Gari linakuwa na polisi wawili, mtu mmoja wa Takukuru, invigilator (msimamizi wa mitihani) na dereva – kwa hiyo kwenye gari tulikuwa na watu watano na huko ndani wamebeba mitihani. Ilikuwa inatugharimu sana. Lakini sasa hivi tunaisambaza kwa barua pepe. Kwa hiyo invigilator anakaa kwenye kituo chake, tumempa kompyuta na printa, halafu mtihani tunakuwa tumeutuma jana yake, lakini una password (nywila). Anaupokea, anau-download, lakini hawezi kuufungua, kesho ndiyo mtihani unafanyika, asubuhi saa 1 na saa 1:30 tunatuma nywila.
Saa 1:30 anapoanza kuchapisha ule mtihani wanafunzi wanakuwa wameshaanza kukaa kwenye chumba cha mtihani kwa hiyo akishamaliza kuchapisha anapeleka. Mtihani wa saa 4 nywila inapelekwa saa 3, saa moja kabla ili awe na muda wa kutosha wa kuchapisha kwa idadi ya wanafunzi.
Kwa sasa hatuingii gharama za kusafirisha mitihani, ile gharama tuliyokuwa tunatumia tumeamua kuwanunulia printa na kompyuta ili waweze kupokea mitihani na kuiwasilisha kwa muda.
Baada ya kufanya mitihani wanaifunga kwenye bahasha ili mtu mwingine asiweze kuiona – kama zile bahasha za DHL, akifungua tu utajua bahasha imefunguliwa. Anazifunga, anazipeleka DHL kwa hiyo mitihani inarudishwa kwa DHL. Hilo limetupunguzia gharama kubwa sana ya magari. Magari yetu yamechoka, hatuna hela ya kununua magari mapya kwa hiyo tukaona lazima tubuni mbinu mbadala.
Itaendelea…