Pesa imejificha katika maeneo makuu matatu. Sehemu ya kwanza pesa ilikojificha ni katika uhitaji.Biashara yoyote kubwa yenye mafanikio ni biashara inayotoa suluhu kwa mahitaji yanayohitajika katika jamii. Ukiweza kutatua uhitaji wa watu kwenye jamii yako au kutatua matatizo ya watu kwenye jamii yako pesa itakufuata.
Tatizo la watu wengi wanaoanzisha biashara zinazokufa kila kukicha ni kwa sababu hawatoi majibu ya mahitaji ya watu katika jamii. Kuanzisha biashara ambayo haitoi suluhisho la mahitaji ya watu ni sawa na kujibu swali ambalo haujaulizwa.
Kijana aliyependa kusoma vitabu aliona kuna shida katika ununuzi wa vitabu. Akaona kuna uhitaji wa kampuni ya kuuza vitabu mtandaoni. Akaiita kampuni yake Amazon. Huyu ni Jeff Bezos ambaye leo hii anatajwa kama tajiri mkubwa duniani.
Usijaribu hata siku moja kutoa huduma fulani bila kuona kama kuna mahitaji. Mimi nimeona ni vyema leo hii kufundisha mada hii kwa sababu wengi wanatamani kujua pesa inakojificha.
Pesa unayoipata au kuipokea haiendani na kitu unachokifanya, lakini inaendana na uhitaji uliopo. Jamii inayotuzunguka ina mahitaji mkubwa, lakini ni watu wachache wanaoona mahitaji hayo. “Kuna watu hawawezi kuziona fursa hata kama zikiwapiga puani,” anasema Strive Masiyiwa.
Kuna hadithi ambayo watu wengi katika eneo la biashara hupenda kuizungumza, sijui umewahi kuisikia? Hadithi hiyo ipo hivi: Kampuni ya uuzaji wa viatu ilihitaji kupanua soko la biashara yake, hivyo ikaamua kumtuma kijana ambaye alikuwa mfanyakazi katika kampuni hiyo kwenda katika kisiwa fulani kuchunguza kama kuna mahitaji ya viatu huko.
Kijana yule alipofika katika kisiwa kile akakuta watu hawavai viatu kabisa. Akapeleka ujumbe makao makuu ya kampuni yake, ujumbe huo ulisomeka; “Hakuna kabisa soko la viatu, watu wa huku hawavai viatu.” Kijana yule alirudishwa na kampuni ikaamua kumtuma kijana wa pili. Kijana huyu alikuwa makini, siyo kama yule wa kwanza. Alipofika katika kile kisiwa na kukuta watu hawavai viatu yeye akapeleka ujumbe uliosomeka, “Soko ni kubwa, tumeni makontena ya viatu.” Kijana huyu wa pili aliona fursa. Fursa ni kama maembe, ukisubiri yiive, wenzako wanakula kwa chumvi.
“Kuwa na lundo la matatizo. Usiruhusu pesa liwe tatizo mojawapo.” Ni msemo wa Grant Cardone. Watu wengi ni maskini kwa sababu hawajajitoa kutatua mahitaji yaliyoko katika jamii inayowazunguka. Jiulize swali leo, kuna mahitaji ya kile unachokifanya? Je, kuna mahitaji ya huduma unayoitoa?
Unapoanza kutatua mahitaji ya watu hakikisha unaongeza thamani kwenye maisha ya watu. “Lengo la biashara ni kutengeneza wateja,” anasema Peter Drucker.
Ili wateja waje kwenye biashara yako lazima utoe thamani. Kwa msingi huo nakubaliana na Henry Ford aliyewahi kusema, “Biashara yoyote inayotengeneza pesa pekee ni biashara ya kimaskini.” Biashara yoyote unayoona inafanikiwa ni ile inayofanya maisha ya watu yawe bora na ya kufurahia.
“Tangu siku yangu ya kwanza ya kuwa mjasiriamali maono yangu makubwa ya kutimiza ni kufanya maisha ya watu yawe bora,” anasema Richard Branson.
Ukitoa huduma nzuri na bidhaa bora watu watakuwa tayari kukulipa. Watu watahitaji kufanya kazi na wewe. Kuna aina mbili za mahitaji unayotakiwa kuzifahamu. Aina ya kwanza ni mahitaji yaliyopo. Anayefungua duka la nguo ametazama mahitaji ya watu katika mavazi. Aliyefungua mghahawa ametizama mahitaji ya watu katika kupata chakula safi. Anayeanzisha saluni mtaani kwako anatizama mahitaji ya watu katika kuweka vichwa vyao katika hali ya kupendeza na kuvutia. Daktari anayeanzisha zahanati au kituo cha afya ametazama mahitaji ya watu katika mambo yanayohusu afya.
Mahitaji ya pili ni yale unayoweza kuutengeneza. Watu wanaweza kuwa hawaoni mahitaji ya kitu mpaka ukianzishe wewe. Inawezekana watu wengi wanalalamika kuwa uchafu umekuwa kero mtaani kwako, kumbe hiyo ni fursa ya kuanzisha kampuni ya kukusanya taka.
Watu hawakuhitaji facebook, lakini Mark Zuckerberg aliona anaweza kutengeneza mtandao unaoweza kuwakutanisha watu wengi kwa wakati mmoja. Huo ndio ukawa mwanzo wa facebook iliyoanzisha mwaka 2004.