Maendeleo ya mtu au watu (jamii ) yanahitaji masharti mawili – JUHUDI na MAARIFA, ambayo msingi wake mkubwa ni mtu (mwananchi) na uwezo wake. Katika utaratibu huu ili mwananchi aendelee atahitaji vitu vinne ambavyo ni Ardhi, Watu, Siasa safi na Uongozi bora.
Dhana na nadharia hizi za kisiasa hazina budi kuendana na mabadiliko ya mazingira ya duniani na ustawi wa watu ndani ya mfumo wa Maendeleo ya Jamii. Tangu dunia kuumbwa hadi sasa hatua mbalimbali za kisiasa na kiuchumi zimepitiwa na watu kupata maendeleo yao.
Nazungumzia maendeleo kwa maana ya hali ya kufanikiwa kijamii, kiuchumi na kisiasa, katika enzi ya ukoloni, enzi ya kupata uhuru na enzi hizi za mwendelezo wa maendeleo ya jamii yetu.
Nchi za Afrika bado zimekuwa katika harakati za kujinasua kiuchumi ndani ya kipindi cha karne moja bila ya kupata mafanikio ya kuridhisha.
Kabla ya uhuru wa Afrika wakoloni walitumia masharti ya maendeleo kwa masilahi yao. Baada ya uhuru kupatikana siasa ilitutaka kutimiza masharti hayo kwa umakini, lakini hatukutimiza kikamilifu kutokana na mabaki, kasumba na makovu ya kikoloni.
Hapa Tanzania, Azimio la Arusha lilituelekeza ili tupate maendeleo tunahitaji vitu vinne; Ardhi, Watu, Siasa safi na Uongozi bora. Lakini kwa makusudi baadhi ya viongozi na wananchi wakalitupilia mbali Azimio la Arusha na kusuasua kufuata masharti ya maendeleo.
Hivi sasa dunia imo katika mwendo kasi wa kutumia teknolojia kuwapatia watu wake maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii. Maendeleo ya dunia yana sukuma nchi za Afrika kwenda na mabadiliko ya mazingira na teknolojia. Tanzania ni moja ya nchi za Afrika, tuamke.
Dunia imo ndani ya kiganja chako, na inawaweka bayana watu katika kupata elimu yao, tafiti zao, kazi zao na starehe zao. Ukweli mambo haya yanataka uadilifu katika kuyaendea na kuyatenda. Mkazo mkubwa uwekwe katika matumizi na ulinzi wa teknolojia inayosukuma maendeleo.
Teknolojia haikatazi kwenda pamoja na masharti ya maendeleo wala mambo manne ya maendeleo ya watu. Teknolojia inahimiza na inachochea kwa haraka uwelewa na matumizi yake. Ni juu ya Watanzania (wananchi) tutakavyotumia teknolojia kupata maendeleo yetu.
Teknolojia hii inatuhimiza zaidi kuitumia katika tafiti za kisayansi juu ya kinga na tiba za magonjwa, maradhi na milipuko ya magojwa kama vile UVIKO-19. Na katika uhalisia huu utaondoa tofauti za fikra, hisia na kuwa na uhakika wa kinga na tiba.
Nguvu ya teknolojia inatufikisha katika matumizi ya ‘Teknolojia ya Habari na Mawasiliano – TEHAMA.’ Mfumo wa TEHAMA unahitajika na kueleweka vema na haraka na Watanzania, hasa vijana ambao wanachukua asilimia kubwa ya idadi ya Watanzania wote nchini.
Kuielewa, kuisambaza na kuitumia haikwepeki. Hivyo uhalisia wa mambo ni kuingia ndani ya teknolojia ya habari na mawasiliano katika shughuli na kazi zetu majumbani, maofisini, viwandani, mashambani, sokoni na michezoni ambako matangazo na mauzo ya bidhaa pamoja na miamala ya simu na benki.
Sera mbalimbali za maendeleo ya jamii hazina budi kuelekezwa katika maeneo hayo na mengineyo ili kuleta tija na ufanisi katika uchumi, siasa na huduma kwa watu. Vyombo vyetu vya mawasiliano na umma, asasi za kijamii na watu wa mitandao kutambua wana dhima kubwa katika kufanikisha maendeleo ya Watanzania.
Watanzania kupitia TEHAMA tunaweza kutumia ardhi yetu katika matumizi ya kilimo, makazi, ufinyanzi na mambo mengine kupata ufanisi mkubwa. Ardhi kuwa bidhaa katika soko, makazi kuwa vivutio baada ya watu kuhabarishwa na kuona mitandaoni. Misitu na mazingira kuwa vivutio kwa watu.
Turudi kwenye siasa kwa kuhamasishana mawazo na matumizi ya siasa safi na kuwa na uongozi bora kwa kufuata na kuzingatia maadili na utamaduni wetu kwa njia ya Tehama. Jambo la msingi ni kuzingatia matumizi mazuri ya mfumo huu na kuacha matumizi ya kutoa kedi, vitisho na dharau.
Tufuate maelezo na maelekezo ya wataalamu wa mfumo wa teknolojia ya habari na mawasiliano juu ya matumizi ya teknolojia, usalama katika uchumi na Tehama na upatikanaji wa ajira kwa watumiao teknolojia hii. TEHAMA kwa faida na masilahi si kwa hasara na umaskini kwa wananchi.