Na Stella Aron,JamhuriMedia,Dar
Wadau wa sekta ya habari wamesema kuwa ili kufikia maendeleo chanya katika sekta hiyo ipo haja ya kufanyika kwa marekebisho ya vifungu vya sheria ya habari kandamizi katika sekta hiyo.
Hayo yameelezwa na Sylvester Hanga Mshauri Mfawidhi kutoka Taasisi ya Ushauri na Utaalam Elekezi ya Mseto wakati akichangia mjadala kuhusu Sheria ya Habari ya Mwaka 2016 katika kikao kazi cha Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), kinachofanyika kwenye hoteli ya Slipway jijini Dar es Salaam.
Hanga amesema kuwa haki za binadamu zinakwenda sambamba na demokrasia hivyo uwepo wa sheria zinazominya tasnia ya habari zinakwamisha maendeleo si kwa sekta hiyo tu bali kwa taifa kiujumla.
“Mchakato huu wa marekebisho ya sheria ya habari ni kuwa na sheria rafiki ambazo hazikwamisha maendeleo ya habari bali zitasaidia kuchochea demokrasia, haki za binadamu na maendeleo kwa Taifa,” amesema.
Amesema kuwa waandishi wa habari ni lazima wawe mstari wa mbele kuisemea jamii lakini ni lazima pia wahakikishe sheria zinazokizana na uhuru wa habari zinafanyiwa marekebisho ili kufanya kazi yao kwa uhuru na weledi
Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Salim Said Salim amewashauri wadau mbalimbali kushiriki katika kushawishi watunga sheria ili sheria hizo ziweze kuangaliwa na kurekebishwa kuwezesha waandishi wa habari kufanya kazi kwa uhuru.
Salim amesema kuwa mwandishi wa habari akijua haki zake, sheria zinazoongoza tasnia ya habari atafanya kazi kwa weledi bila ya kikwazo.
“Bado waandishi hatujawa na uelewa mpana wa sheria zinazotuhusu, tufanye jitihada kuzijua. Tuwashawishi wenzetu juu ya sheria zinazokwaza ukuaji wa tasnia ya habari na maendeleo ya Taifa,” amesema.
Naye Joyce Shebe amesema anaamini wahariri wakijua namna ya kushawishi watunga sheria, sera na mipango ya Taifa watakuwa kwenye nafasi njema ya kuchochea maendeleo ya mtu mmoja na Taifa.