Maendeleo yana sheria zake. Ingawa tunasema kwamba, maendeleo yao yanakwenda mijini, mendeleo yote yanakwenda mijini. Ni kweli tunasema hivyo, lakini mnafikiria mijini wana uchawi? Kuna masharti ya maendeleo. Nimepata kutumia mfano- nadhani hapa hapa kwamba, mvua inaponyesha, kuna kitu uvutano – huyavuta na kwenda baharini. Vijito hivi vyote huvutwa viongeze baharini – vyote kabisa vinaongeza baharini. Maji hata Dodoma, huelekea baharini. Kuna uvutano- unayavuta yatoke sehemu ya juu yaende sehemu ya chini. Sehemu ya chini ni bahari. Maji yote ni 2/3 yanakwenda kule. Miji ina uvutano wa namna hiyo hiyo.

Unaona sasa jumba hili hapa. Sasa, utakwenda kulipachika Chamwino hivi hivi tu hili? (kicheko) watu watakusema. Wakikukuta unalijenga huko Chamwino watasema kwamba huyu hasa anataka nini hapa? Mnaona mataa haya yanawaka hata mchana; unaweza ukayaweka Nyanguge? (kicheko). Mataa mazuri namna hii na limtambo kubwa la kuvuta umeme ukalipachika Nyanguge, watakuona unawazimu. Huyu hasa anatafuta nini hapa(kicheko).

Maendeleo yana sheria zake na sheria moja ni mkusanyiko wa watu. Watu wakishakusanyika mahali, wanalazimisha mambo fulani fulani. Lazima yatafanyika. Lazima! (Makofi). Sasa, waheshimiwa mnapiga makofi, harafu mnarudi, mnabaki vilimani kule kule. (Kicheko na Makofi)

Maendeleo yana sheria zake. Dar es Salaam inavuta maendeleo sasa hivi siyo kwa sababu Serikali au TANU inawapenda sana watu Dar es Salaam hata kidogo. Ilikuwa lazima hospitali ya Mhimbili tuijenge Dar es Salaam, huwezi kwenda ukachukua mahali tu hivi hivi tu. Hakuna watu ukapachika hospitali ya Dar es Salaam una wazimu? Wewe unajenga hospitali kubwa namna ile mahali hivi hivi tu.

Sasa tunao mpango mkubwa sana wa maji, tuna mpango mkubwa sana wa maji, tuna mpango mkubwa sana wa maji ya kuvuta kutoka Ruvu yanakuja hapa- yanawapita Wazaramo- wako wazaramo wengi zaidi kuliko hawa wote wanaokaa Dar es Salaam. Lakini maji yale yanakuja hapa yanawafuata hapa kuna uvutano hapa una watu wengi namna hii hapa usiwape maji halafu utafanya nini?. Lazima uyalete ukipenda usipende utayaleta maji hayo. Sasa hili jambo tumekubali wananchi acha kwanza habari ya ujamaa, lakini habari ya maendeleo ya kawaida yanataka watu wakae pamoja- lazima mkae pamoja.

Maendeleo ya kawaida hivi tunazo shule chungu nzima hazikujaa watoto. Kwa nini watu wako mbali. Shule iko hapa, watu wenyewe wako huko, darasa hili litajaa namna gani?. Na watu wako mbali mbali litajaa namna gani?. Nimekwenda Kilwa juzi. Kilwa wanazo dispensari za kutosha kabisa watu wote- za kutosha kabisa lakini hazitoshi; kwa sababu wako mmoja mmoja huko Dispensaries walizo nazo ni nyingi zaidi kuliko tulizokubaliana katika mpango wetu wa miaka mitano. Wamekwisha vuka hapo; lakini hazitoshi; lakini hazitoshi kwa sababu watu wako huko huko. Sasa nasikia kuna operesheni kimya kimya huko, huenda ikatusaidia. Huenda ikatusaidia watu hawa wakazitumia ziko hazitumiki kwa sababu hawapo karibu na dispensaries zile. Sasa jambo la kuishi pamoja wananchi tunalisema, mimi nafsi yangu nalisema mwaka wa kumi na moja huu. Nalisema. Sasa tumeanza kuwaambia vijijini.

Sasa hivi nilipokuwa naitayarisha ripoti hii tulikuwa na vijiji 5,556. Ripoti ya Katibu Mtendaji ameiandika baada ya ripoti yangu na yake itaonyesha vijiji ni vingi zaidi kuliko ripoti yangu. Yake ndhani itaonyesha 5,620 hivi. Sasa viko vijiji vingi na kiasi cha watu milioni 2 wanaishi katika vijiji hivyo. Katika watu kiasi cha milioni 14 ukichukua wengine wanaoishi Dar es Salaam na miji mingine ambao hawafiki hata milioni moja. Kusema kweli sasa watu wanaoishi katika sehemu za mkusanyiko miji na vijiji ni kiasi cha milioni 3 si zaidi ya hapo wala watu wetu waliobaki milioni 11 bado wanaishi ovyo ovyo. Miaka kumi na moja –miaka kumi na moja tangu tumeanza kupiga kelele hii ya kuishi pamoja vijijini. Sasa nasema tumeanza lakini ingawa vijiji hivyo sasa vingi lakini haviko katika Mikoa yote. Viko zaidi katika Mkoa wa Dodoma na Mkoa wa Mtwara.

Dodoma kwa sababu ya operesheni Dodoma na Mtwara kwa sababu ya operesheni yao wenyewe. Mtwara sasa hivi watu wengi wanaishi vijijini; wilaya ya Masasi karibu watu 80,000 (themanini kwa mia) wanaishi vijijini; wilaya ya Newala inawezekana wananiambia kwamba labda 96 kwa mia wanaishi vijijini. Wanne (4) ndio wamebaki na wale wanaoonekana kama wachawi; wachawi hivi kwamba hawaishi na wenzao.

Mikoa mingine ina taabu kama Kilimanjaro wana vijiji 24 lakini tulijua taabu zao, taabu za sehemu kama Kilimanjaro tunazielewa lakini iko Mikoa mingine ambayo haina taabu hizo kama tunazozijua na bado hawajatuonyesha dalili nzuri. Ziko dalili katika baadhi ya Mikoa lakini kwa kweli si nzuri sana; bado hazijawa nzuri, ingekuwa ni nzuri sana tungekuwa tuko mbali.

Kwa hiyo jambo ambalo tuko nyuma mpaka sasa tuko nyuma sana ni hili; na napenda kuwaambieni kwamba Halmashauri Kuu tulikutana, tukakumbushana jambo hili katika kipindi hiki tangu tumeachana, tulikutana tukalizungumza jambo hili, na tukakubaliana ; sasa hakuna tena operesheni Dodoma, sijui operesheni Kigoma iko Mikoa hii ina matatizo fulani fulani tutaendelea kuitilia mkazo lakini jambo la kuishi vijijini sasa ni jambo la nchi nzima, (Makofi).

Na napenda kusema zaidi ya hapo, nataka kusema zaidi ya hapo maana wakati mwingine kwa kweli ni lazima tukubali kuongoza nchi. Ama sivyo tunaweza kujikalia tu kama wajinga. Uongozi ni uongozi; na kama njia ya kupita ni hii basi viongozi tunasema tupite hapa, (Makofi). Jambo la kuishi vijijini kama ni kueleza lieleweke, tumeeleza miaka kumi na moja. Linaeleweka, linaeleweka. Tunazungumza habari ya kuishi vijijini; mimi sizungumzi habari ya ujamaa nazungumza hbari ya kuishi vijijini. Ujamaa si jambo naweza nikamlazimisha mtu kuwa mjamaa. Mtu mwenyewe utakuwa mjamaa- ujamaa ni moyo utawezaje kulifanya jitu lenyewe lina tamaa ya unyonyaji tu ukaligeuza liwe mjamaa.

Haliwezi kuwa mjamaa. Mimi ninazungumza habari ya kuishi vijijini. Habari ya kuishi vijijini ni utaratibu wa kuishi. Tunasema tu kwamba pale ni msitu huwezi kujenga nyumba katika msitu. Tunaweka akiba yam situ pale. Kwamba pale ni mahali pa mashamba ya kulima hatuwezi tukakuchia ukakaa pahala pa kulima. Kwamba pale ni mahala pa Machungaji tunachungia huko; tutakuwa tunapeleka ng’ombe huko, wanachunga huko, na ndiko tutakakotia mabwawa ya kunyweshea ng’ombe, (Makofi).