Na angela kiwia
Mbunge wa Bukombe, Dotto Biteko, katika mahojiano maalumu na JAMHURI kuhusu mambo ya maendeleo yanayoendelea jimboni kwake, amesema katika kipindi cha miaka mitatu mtazamo wa wananchi wa Bukombe umebadilika, tofauti na ilivyokuwa mwanzo.
Biteko, ambaye pia ni Waziri wa Madini, amesema wananchi wamekuwa na mwamko mpya wa maendeleo, jambo ambalo linasaidia kubadilisha taswira ya jimbo na Wilaya ya Bukombe kwa ujumla.
Amesema serikali imekuwa ikitoa pesa nyingi katika shughuli za maendeleo ikiwa ni pamoja na ahadi ya Rais Dk. John Magufuli aliyotoa kwa wananchi kuwa hatawatupa.
Akizungumzia utekelezaji wa ahadi zake na ilani ya uchaguzi ya mwaka 2015/2020 anabainisha kuwa ilani ya CCM ukurasa wa 77 mpaka 79, inaeleza kuwa na taifa lenye watu wenye afya bora inayowawezesha kuzalisha mali na kutoa huduma mbalimbali.
Amesema serikali iliendelea kuyapa kipaumbele maeneo yaliyoainishwa katika MKUKUTA na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Milenia, ambapo mafanikio yafuatayo yamepatikana:-
Ukarabati vituo vya afya
“Katika kuhakikisha tunaendelea kuboresha huduma za afya kwa wananchi tumefuatilia upatikanaji wa fedha kutoka kwa wahisani mbalimbali ikiwa ni pamoja na Benki ya Dunia kwa ajili ya vituo vyetu vya Ushirombo, Uyovu, Bulega, Ikuzi, Iyogelo, Bugelenga,
Ikuzi, Bugando na Bukombe,” amesema Biteko.
Kituo cha afya Uyovu
Biteko amesema Sh milioni 400 zimetumika kuboresha Kituo cha Afya cha Uyovu kwa kujenga nyumba ya mtumishi, maabara, wodi ya wazazi, jengo la kliniki ya mama, baba na mtoto.
Pia ujenzi wa wodi ya watoto, ukarabati wa jengo la upasuaji, jengo la kuhifadhia maiti, ukarabati wa jengo la kufulia, ujenzi wa njia ya kuunganisha wodi na majengo mengine ya kuchomea taka.
Amesema kukamilika kwa majengo haya kutasaidia kuboresha huduma za afya kwa wananchi na kusogeza huduma karibu nao. Kwani kituo hiki sasa kitatoa huduma zote ikiwa ni pamoja na upasuaji.
Kituo cha Afya Ushirombo
Waziri Biteko amesema wamefanikiwa kujenga majengo mapya, majengo hayo ni wodi ya kina mama, maabara, jengo la upasuaji, chumba cha kuhifadhia maiti pamoja na nyumba ya mtumishi. Zimetumika Sh milioni 500.
“Kituo hicho ni moja ya vituo vinavyotegemewa kwani kitasaidia kupunguza msongamano katika hospitali yetu ya wilaya.
“Tumekamilisha ujenzi, sasa tupo kwenye hatua za kukusanya vifaa tiba vinavyohitajika huku tukiendelea kuwasiliana na Wizara ya Afya,” amesema Biteko.
CHF jimboni
“Katika kutambua umuhimu wa wazee tumeanzisha mfuko wa bima kwa wazee jimboni kwetu na tumetenga Sh milioni nane kwa ajili ya matibabu hayo. Bima zimeshaanza kutolewa na wazee 800 tayari wamepata bima hizo. Tunaendelea kutekeleza hili kwa kutoa bima kwa wazee wengi zaidi ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya.
“Pia tumefanya ujenzi wa nyumba za watumishi wa afya katika zahanati za Miyenze, Msasani, Bugelenga, Bulega na Uyovu. Tunaendelea kuboresha maisha ya watumishi wetu wa afya ili waweze kutoa huduma kwa ufanisi zaidi na tayari tumepata fedha Sh milioni 511 kutoka Taasisi ya Mkapa (Mkapa Foundation) ili kujenga na kukamilisha nyumba kumi za watumishi ambazo zimekamilika na tayari zinatumika.
“Nyumba hizi zimesaidia kuboresha mazingira mazuri ya kuishi kwa wataalamu wetu wa afya na watumishi hawa wanapatikana muda wote, jambo linalosaidia kutoa huduma kwa kiwango bora na huduma za dharura nyakati za usiku.
“Kwa dhati kabisa, tunapenda kuishukuru Taasisi hii ya Mkapa Foundation iliyoanzishwa na Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, kwa kutusaidia ufadhili wa nyumba hizi.
“Tunaiomba taasisi hiyo iendelee kutuunga mkono sisi Bukombe, kwani bado tunayo mahitaji katika jimbo letu ili kuhakikisha tunajenga miundombinu bora na ya kisasa zaidi katika sekta hii nyeti ya afya ili kuimarisha afya za watu wetu,” amesema Biteko.
Zahanati ya Businda
“Shilingi milioni nane zimetumika kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa zahanati. Zahanati hii ni moja ya ahadi zilizotolewa wakati wa Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.
“Tuliahidi kujenga zahanati kwa kila kijiji, ni wazi kukamilika kwa zahanati hii kutaendelea kuboresha huduma za afya kwa wananchi na ndiyo azima ya serikali yetu kuendelea kusogeza huduma karibu na wananchi wetu,” amesema Biteko.
Maji
“Ukarabati wa visima 10 umefanyika katika vijiji vya Ituga kisima 1, Katente kisima 1, Bugelenga visima 2, Iyogelo kisima 1, Ikuzi kisima 1, Ihulike visima 2, Bulangwa kisima 1 na Ishololo kisima 1.
“Katika ukarabati huu, jumla ya Sh milioni 44 zilitumika na ukarabati umekamilika ambapo wananchi wanaendelea kunufaika na mradi huu.
Zimetengwa fedha Sh milioni 340 kwa ajili ya kusambaza maji ndani ya mji wa Ushirombo. Tunatambua kuwa maji bado ni changamoto katika mji wetu.
“Wataalamu wetu wa maji wanaendelea na jitihada za kutandaza mabomba ya maji ili kila kaya iweze kupata maji,” amesema Biteko.
Miundombinu
“Hapo awali tulikuwa na mtandao wa barabara za lami kilometa 256 na sasa tumefanikiwa kuongeza hadi kufikia kilometa zaidi ya 1,500 na kuwa wilaya ya pili katika Mkoa wa Geita kwa kuwa na mtandao mkubwa wa barabara za lami.
“Ili kuhakikisha kuwa tunaunganisha maeneo ndani ya Jimbo letu la Bukombe na maeneo jirani na kurahisisha mawasiliano, kuna matengenezo ya barabara kwa hatua mbalimbali ambayo yamefanyika katika kipindi kifupi,” amesema Biteko.
Barabara zilizo katika utekelezaji
“Barabara ya Namonge – Uyovu. Barabara hii imetolewa halmashauri na kuwekwa chini ya Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kutokana na umuhimu wake na hasa ukubwa.
“Barabara ya Msonga – Chato; Barabara hii imefunguliwa na lengo ni kurahisisha namna ya usafiri kati ya maeneo haya. Barabara ya Ushirombo – Mbogwe kupitia Katome, barabara hii iko katika hatua za mwisho na tayari ishafunguliwa.
“Barabara ya Musasa – Mji mwema kupitia Msangila, Kaziramuyaye. Barabara hii inajengwa na Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (TARURA) na tayari ipo katika utekelezaji ambapo kilometa 18 zinajengwa.
“Barabara ya Butizya – Igwamanoni inaendelea na ujenzi. Barabara hii ina urefu wa kilometa 10 iko katika utekelezaji na ikikamilika itaunganisha maeneo haya na kurahisisha usafiri na usafirishaji. Barabara ya Butizya – Ng’anzo. Barabara hii ina urefu wa kilometa 8.8 na iko katika utekelezaji,” amesema Biteko.
Ujasiriamali
“Kutokana na ilani ya uchaguzi inayosema kuwa shughuli za kiuchumi kwa mtu mmoja mmoja ni muhimu katika kujenga uchumi wa jimbo letu na taifa kwa ujumla. Tumehamasisha kuanzishwa kwa vikundi vya ushirika kama vile Saccos na Vicoba.
“Tuliwahakikishia vijana na kina mama kuwa wanapata fedha waweze kukopeshana ili kuinua uchumi wao kupitia shughuli za ujasiriamali. Pia nimekuwa nikihamasisha halmashauri iendelee kutoa asilimia 4 kwa vijana, asilimia 4 kwa kina mama na asilimia 2 kwa walemavu.
“Tumeweza kushiriki kikamilifu kuwaendeleza kina mama kupitia kuchangia fedha kwenye vikundi vyao vilivyopo hapa Bukombe.
“Mbali na kutoa fedha za jimbo, nimefuatilia kupata fedha kutoka ofisi ya waziri mkuu Sh milioni 56 kisha kuzipeleka kwenye Saccos ya vijana (Bukombe Vikana Saccos) tukiwa na nia nzuri ya kuwafanya vijana wakopeshane wao kwa wao na kufanya ujasiriamali ili kuinua uchumi wao.
“Binafsi nimekuwa nikiifuatilia kwa ukaribu Saccos hii ili iweze kutumika kuboresha maisha ya Wana Bukombe na taifa kwa ujumla,” amesema Biteko.
Umeme
“Jumla ya vijiji tulivyo navyo ni 52, lakini tumebadilisha baadhi ya vitongoji kuwa vijiji ili kufikia malengo yetu ya kuifanya Bukombe yetu nzima ipate umeme na tumepata jumla ya vijiji 80.
“Ni matumaini yangu kufikia mwaka 2020 asilimia kubwa ya jimbo letu litakuwa na umeme kwani tayari nguzo zinaendelea kusambazwa,” amesema Biteko.
Kilimo na mifugo
“Ili kuendana na ilani ya uchaguzi, tumejitahidi kuhudumia kilimo na mifugo kwa kufanya yafuatayo:
“Kilimo ni uti wa mgongo wa maendeleo kwa jamii yoyote ile, wananchi wa jimbo letu wanalima mazao ya chakula na biashara ili kujiletea maendeleo. Tumejitahidi kuboresha kilimo kwa kuwawezesha wakulima pembejeo za kilimo ikiwa ni pamoja na mbegu za pamba, dawa na vinyunyizi.
“Jumla ya wakulima 13,569 walisajiriwa na kulima zao la pamba huku kilo 480,327 za mbegu yenye manyoya zilikopeshwa kwa wakulima zikiwa na thamani ya Sh milioni 336.
“Jumla ya chupa (A/P) 192,748 za viuatilifu zenye thamani ya Sh milioni 385 na vinyunyizi 650 vyenye thamani ya Sh milioni 26 vilikopeshwa kwa wakulima. Jumla ya deni lote la pembejeo ni Sh milioni 747.7, kati ya deni hilo, Sh milioni 411 (vinyunyizi na viuadudu) serikali ililisamehe.
“Na wakulima walitakiwa kulipa deni la mbegu tu ambapo mpaka sasa ni Sh milioni 270.7 tu sawa na asilimia 81 ya deni zimerejeshwa,” amesema Biteko.
Soko la kisasa
“Soko la kisasa limejengwa Kata ya Namonge ambalo limegharimu Sh milioni 581 ambao ni ufadhili wa MIVAP kwa ajili ya ujenzi wa soko la muhogo la kisasa Namonge.
“Soko hili limeboresha mazingira ya kufanyia biashara hii ya mihogo.
“Pia wananchi wetu wanashiriki kikamilifu katika shughuli za ufugaji wa ng’ombe, mbuzi, kondoo n.k.
“Jimbo letu pia linazo changamoto kwa wafugaji ambazo pia tunaendelea kushughulika nazo ambazo ni upungufu wa maeneo ya kulishia mifugo kutokana na kuwa eneo kubwa ni la hifadhi.
“Hali hii imesababisha mgogoro kati ya wahifadhi na wafugaji na kuwa kero kwa wafugaji wetu. Ni wazi sehemu yoyote yenye migogoro maendeleo yatabaki kuwa ni ndoto.
“Pamoja na chamgamoto hii, tumeendelea na jitihada za kutatua changamoto hii kwa kutumia mamlaka zinazohusika ambapo Mheshimiwa Rais aliagiza wizara zinazohusika kukaa pamoja na kutafuta ufumbuzi.
“Jitihada hizo zinalenga kupunguza eneo la hifadhi na kupewa wananchi wetu kwa ajili ya shughuli za ufugaji na kilimo, haya ndiyo maagizo ya ilani yetu ya uchaguzi ya Chama chetu Cha Mapinduzi kuhakikisha kero hii inamalizwa kufika mwaka 2020.
“Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamis Kigwangalla, alifika na kuvitembelea vijiji vilivyo pembezoni mwa hifadhi na kueleza dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kutatua mgogoro wa upungufu wa ardhi ya shughuli za kilimo na ufugaji, ambapo mifugo pia hutaifishwa,” amesema Biteko.
Ufugaji wenye tija
“Jimbo letu la Bukombe linakadiriwa kuwa na ng’ombe zaidi ya 100,000 lakini bado maisha ya wafugaji si mazuri. Tumeendelea kuwashauri waendelee kufuga kisasa zaidi ili kuboresha maisha yao kwa kupunguza idadi kubwa ya mifugo ili maeneo yasiwe changamoto kubwa kwao na pia wapate tija kutokana na ufugaji wao,” amesema Biteko.
Madini
“Wananchi wa jimbo letu wanajishughulisha na shughuli za uchimbaji wa madini hasa dhahabu. “Tumewasaidia wachimbaji wadogo ili wapate leseni, tuna lengo la kuwafanya watambulike kisheria ili kuendelea kujenga uchumi wao na taifa kwa ujumla,” amesema Biteko.
Tumetoa leseni kwa hatua zifuatazo
“Leseni zilizotolewa na zinafanya kazi ni leseni 195. Leseni zinazopendekezwa kutolewa ni leseni 64. Tayari wachimbaji wetu muda si mrefu watapewa leseni zao baada ya maombi yao kufanyiwa kazi, niwaombe wasubiri kidogo tu watapata leseni.
“Leseni zilizoombwa kwa kipindi hiki ni leseni 263.Tuna imani kuwa wachimbaji hawa walioomba leseni watapewa baada ya maombi yao kushughulikiwa. Tunaendelea kufuatilia kuhakikisha leseni hizi zinatolewa ili wachimbaji wadogo wengi wawe na leseni za uchimbaji.
“Pamoja na leseni hizo kuendelea kutolewa changamoto yao kubwa ni kukosa mitaji ili kupata nyenzo za kuwawezesha kufikia malengo yao ya kuchimba. Tumewasaidia wachimbaji hawa kwa kuleta wataalamu wa utafiti wa madini (GST) kutoka Wizara ya Madini ili kuwasaidia kuleta mitambo ya kuchimba,” amesema Biteko.
Ujenzi wa kituo cha kuchenjua dhahabu Katente
“Tumeishirikisha Wizara ya Madini kuwasaidia wachimbaji wetu, vipo vituo saba vya mfano kwa ajili ya kuwasaidia wachimbaji wadogo nchini katika vituo hivyo.
“Kituo kimoja kinajengwa Katente kutoka mradi wa Benki ya Dunia, utafiti umefanyika chini ya STAMICO na tathmini ya mazingira tayari imefanyika,” amesema Biteko.
Ujenzi wa vituo vya Polisi
“Ili kuhakikisha tunasogeza huduma za ulinzi kwa wananchi, tumeshirikiana na wananchi wetu katika kuhakikisha tunajenga.
“Vituo vidogo vya Polisi, ambapo jumla ya vituo vitatu vimekamilika na vimefunguliwa. Vituo hivyo ni Bulega, Bukombe na Namonge.
“Kukamilika kwa vituo hivi kunatoa fursa kwa wananchi wetu kuhudumiwa na kuwa na uhakika wa usalama wa mali na maisha yao.
“Askari Polisi wanaofanya kazi kwenye vituo vipya walikuwa na changamoto ya ukosefu wa huduma za usafiri wa kuwafikisha kwenye maeneo ya matukio mapema, hivyo tumenunua pikipiki moja kwa kila kituo cha polisi.
“Tumetumia Sh milioni 7.2 kununulia pikipiki tatu kwa ajili ya vituo vitatu vya polisi,” amesema Biteko.
Uwekezaji
“Jimbo letu ni moja ya maeneo katika nchi yetu yenye fursa nyingi za uwekezaji katika sekta mbalimbali. Ni wazi kuwa kwa wale wageni wanaotafuta maeneo ya kuwekeza, tunawakaribisha sana Bukombe, kwani ni mahali salama pa kuwekeza ili kujenga viwanda na kupata faida.
“Malighafi ambazo unaweza kuzipata ukiwekeza kwa kujenga kiwanda Bukombe, ni pamoja na malighafi za mifugo kama vile nyama, ngozi na maziwa.
“Bukombe ni wilaya inayopatikana asali safi na bora kabisa katika ukanda huu wa Afrika Mashariki. Tunawakaribisha wawekezaji kujenga viwanda katika maeneo yetu, kwani tunayo asali ya kutosha.
“Upatikanaji wa muhogo ni wa kutosha, muhogo ni moja ya kilimo kinachoshika kasi Bukombe ndiyo maana tumejenga soko la kisasa la muhogo Namonge.
“Tumejitahidi kila sekta kutekeleza kama tulivyoahidi kipindi cha uchaguzi. Kusema na kutenda, sasa tunatenda, tunafahamu kuwa maendeleo yanakwenda kwa awamu na tunaendelea kutekeleza, kikubwa tuwe na subira katika mapinduzi makubwa yanayokuja Bukombe.
“Madhumuni makubwa ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuyatekeleza yote yale tuliyoyaahidi kwenye ilani ya uchaguzi, nami nikiwa mbunge nitaendelea kupambana ili kutekeleza tuliyoyaahidi kwa kushirikiana na wakazi wa Bukombe,” amesema Biteko.
Michezo
“Michezo ni afya, michezo ni ajira kwa vijana wetu. Kwa miaka yote mitatu tumeendelea kuzipatia timu zetu mbalimbali za vijana vifaa vya michezo ambavyo ni jezi na mipira.
“Jimboni tuna ligi ya Mbunge inayojulikana kama Doto Cup, ligi hii imeendelea kuwaleta pamoja Wana Bukombe na kuibua vipaji vya vijana wetu,” amesema Biteko.