Maelfu ya watu wameendelea kujitokeza kutoa heshima zao za mwisho kwa aliyekuwa kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Maelfu ya watu wameendelea kujitokeza kutoa heshima zao za mwisho kwa aliyekuwa kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro  mjini Vatican. Ni wakati maziko yake yakitarajiwa kufanyika Jumamosi wiki hii. 

Waombolezaji kutoka maeneo mbalimbali duniani wataendelea kujipanga hii leo kuuona mwili wa Papa Francis ambao umelazwa katika jeneza la wazi katika Kanisa Kuu la mtakatifu Petro siku moja kabla ya mazishi ya kiongozi huyo.

Jana Alhamisi Vatican ilisema zaidi ya watu 90,000 walipata nafasi ya kutoa heshima zao za mwisho huku milango ya kanisa hilo ikiachwa wazi hadi usiku wa kuamkia wa leo kuwaruhusu watu wengi zaidi kupata nafasi hiyo.

Picha mbalimbali za nje ya uwanja wa Kanisa la Mtakatifu Petro zimeonyesha maelfu ya waombolezaji wakiwa kwenye foleni ndefu ya kuingia kanisani kuutazama mwili wa aliyekuwa kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis aliyefariki siku ya Jumatatu akiwa na miaka 88.