Na Thompson Mpanji, Mbeya
MAELFU ya Wakazi wa Jiji la Mbeya wamejitokeza kumzika Shemasi wa Kanisa la EAGT, Kisima cha Bubujiko lililopo Mtaa wa Iyela II, Uwanja wa Ndege wa Zamani, jijini Mbeya, Allen Achiles Mapunda (20), aliyefariki Machi 25, mwaka huu, katika hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya.
Kifo cha Mapunda kimezua utata mkubwa kwa kufariki muda mfupi baada ya kupewa dhamana na Jeshi la Polisi. Mapunda alikamatwa na vijana wengine12 wakati Askari Polisi wakiwa katika doria Machi, 24, mwaka huu majira ya saa 6.15 usiku.
Mazishi yamefanyika katika makaburi ya Iyela, jijini Mbeya na kuhudhuriwa na maelfu ya waombolezaji kutoka maeneo mbalimbali jijini Mbeya huku vilio na simanzi vikiwa vimetawala. Mwili wa Mapunda ulipokewa kutoka Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya majira ya saa10 jioni maeneo la Mafiat na kushushwa kwenye gari kisha ukabebwa begani hadi nyumbani kwao huku vijana wakiimba nyimbo za maombolezo.
Akiongoza ibada ya mazishi, Mchungaji Andrew Kalata wa Kanisa la EAGT Kisima cha Bubujiko lililopo Mtaa wa Iyela II, amesema maisha ya mwanadamu yanaweza kutoweka muda wowote.
“Lakini unapokufa uwe na ushuhuda mzuri kama ulivyo kwa Allen. Alikuwa ni Shemasi wa Kanisa na Mwalimu wa uimbaji na mtoaji mzuri wa sadaka, nami nilikula matunda ya biashara yake ya machungwa,” amesema Mchungaji Kalata.
Mchungaji Kalata amesema kifo cha Allen kimekuwa pigo kwa Kanisa, lakini ameacha alama katika Kanisa kutokana na hekima zake kwani muda mwingi alijitolea kumtumikia Mungu katika uhai wake licha ya umri mdogo aliokuwa nao.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Iyela II, Boaz Kazimoto Kyejo amewataka wakazi wa mtaa wake kuwa watulivu katika kipindi hiki cha maombolezo na kuvuta subira wakati Jeshi la Polisi likiendelea na uchunguzi kubaini kifo cha Allen ambaye pia alikuwa mfanyabiashara wa matunda aina ya Machungwa na Shabiki wa timu ya soka ya Mbeya City kimetokana na nini.
Baada ya Mazishi, Baba Mzazi wa Allen, Mzee Achiles Mapunda amesema alipata taarifa za mwanawe kukamatwa akiwa safarini Moshi, lakini alizungumza na watoto wake wengine kupitia simu ya mama yao, Alice Mapunda akimwambia ana maumivu makali ya kichwa baada ya kupata kipigo kutoka kwa baadhi ya Askari waliomkamata.
Mapunda amesema muda mfupi alipata taarifa kuwa mwanawe amefariki akiwa mapokezi majira ya mchana katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya na kwamba hana lolote la kuzungumza zaidi ya kusubiri taarifa za uchunguzi wa daktari, huku akimuomba Mungu awape faraja katika kipindi hiki kigumu wanachopitia cha maumivu ya kumpoteza mpendwa wao.
“Mwanangu hakuwa akijihusisha na makundi ya uhalifu. Muda wote alikuwa akifanya biashara zake na baada ya biashara alikuwa akienda kufanya ibada katika Kanisa la EAGT… naiomba Tume inayochunguza mazingira ya kifo cha mwanangu itende haki kwani mwanangu hakuwa na ugonjwa wowote na alikamatwa akiwa mzima na alipotoka polisi baada ya kudhaminiwa alipelekwa hospitali ya Mkoa baadaye Rufaa alipokutwa na mauti Machi 25, mwaka huu,” amesema Baba Mzazi wa Allen.
Kutokana na sintofahamu hiyo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limetoa taarifa kwa vyombo vya habari kukanusha kuhusika na mauaji ya kijana huyo.
Akizungumza na vyombo vya habari ofisini kwake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Naibu Kamishna wa Polisi, Mohamed Mpinga, amesema Jeshi lake limeendelea kukabiliana na vitendo vya uhalifu kuhakikisha wakazi wa Mkoa wa Mbeya wako salama, huku akikanusha askari wake kuhusika na kifo cha kijana Allen anayefariki Machi, 25 majira ya saa 12.00 jioni.
Kamanda Mpinga amefafanua tukio hilo kwamba mnamo Mach, 24, 2018 majira ya saa 6.15 usiku askari polisi waliokuwa katika doria na oparesheni ya kukamata wahalifu huko maeneo ya Mtaa wa Airport ya Zamani, Kata ya Iyela, Tarafa ya Iyunga, Jiji na Mkoa wa Mbeya walifanikiwa kuwakakamata vijana 12 akiwemo kijana mmoja ambaye alifahamika kwa jina la Allen Achile (22).
Amesema kuwa mtuhumiwa huyo pamoja na wenzake baada ya kukamatwa walifikishwa kituo kikuu cha Polisi Mbeya Mjini na kufunguliwa mashitaka ya uzembe na ukorofi ambapo walishikiliwa na kuhojiwa na baadaye Machi 25, majira ya saa 4.45 asubuhi mtuhumiwa Allen alidhaminiwa na ndugu zake na kwenda nyumbani kwao na ilipofika saa 12.00 jioni zilipatikana taarifa kuwa mtuhumiwa huyo amefariki dunia.
Amefafanua kuwa baada ya taarifa hizo, wananchi wa eneo la Airport ya Zamani hasa vijana walianza kufanya fujo kwa kutuhumu kuwa polisi wamehusika na kifo hicho hivyo kwenda nyumbani kwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa aliyetajwa kwa jina la Boaz Kazimoto (74), Mkazi wa Iyela kwa kumtuhumu kuwa yeye ndiye aliyewaita polisi kwenda kumkamata Allen wakaanza kuvunja madirisha ya nyumba yake.
Kamanda Mpinga amesema baadaye kundi la wananchi lilielekea kwenye barabara za mtaa huo na kupanga mawe barabarani na kuchoma moto meza za wafanyabiashara wa Soko la Maendeleo ikiwemo kubomoa milango yote, kuharibu samani za Ofisi ya Afisa Mtendaji wa Kata ya Iyela na baadhi ya nyaraka za ofisi ambazo hadi sasa thamani yake bado haijajulikana.
Amebainisha kuwa baadhi ya wananchi hao walikwenda nyumbani kwa askari aitwaye H.4325 PC Yohana wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia na kuvunja madirisha ya nyumba yake huku wakitoa kauli ya kuwa wataichoma moto nyumba hiyo hali iliyosababisha kuongeza nguvu kudhibiti vurugu hizo ikiwemo kutumia mabomu ya machozi ambapo gari yenye namba za usajili PT 1987 aina ya Toyota Land Cruiser Mali ya Polisi Wilaya ya Mbeya mjini ilivunjwa kioo cha mbele kwa mawe.
Amesema kutokana na vurugu hizo Polisi waliwakamata watuhumiwa nane Eliud Daud [22], Mkazi wa Iyela, Bariki Masudi [30], mkazi wa Iyela, Frank Kilemi [33], Mkazi wa Airport ya Zamani, Krist Nelson [33], Mkazi wa Airport ya Zamani, Estom Mbalo [24], Mkazi wa Airport ya Zamani, Robert Mwangupili [24] Mkazi wa Iyela, Issa Nelson [26] Mkazi wa Iyela na Felix Mbilinyi [21] Mkazi wa Airport ya zamani.
Watuhumiwa hao wanahojiwa na Jeshi la Polisi na watafikishwa Mahakamani wakati wowote baada ya taratibu za kisheria kukamilika na kwamba juhudi ya kuwasaka wengine waliohusika na kuanzisha vurugu hizo zinaendelea.
“Nichukue nafasi hii kuwapa pole wazazi, ndugu na hata walioguswa na kifo cha kijana huyu, niwathibitishie wananchi kuwa Jeshi la Polisi halikuhusika na kifo cha kijana huyu kwa aina yoyote… nimefungua jalada la uchunguzi [PE] kupitia Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai [RCO] ofisini kwangu kwa ajili ya uchunguzi wa kifo cha Marehemu,” amefafanua Kamanda Mpinga.
Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, William Ntinika inaelezwa kuwa alifika nyumbani kwa Allen kutoa pole kwa wafiwa akiwa ameongozana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Mpinga baada kuagizwa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla.