Malinzi 1Zimesalia siku chache kumalizika kwa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, ambayo ni mara ya kwanza kushirikisha timu 16.

Miaka ya nyuma Ligi hiyo ilikuwa inashirikisha klabu 12 hadi 14 ambapo timu mbili za juu zilikuwa zinaenda kushiriki michuano ya kimataifa. Ila kabla ya Zanzibar haijapata uanachama Chama cha Soka cha Afrika(CAF), Tanzania ilikuwa inapata bingwa wake baada ya kucheza Sita Bora ya Kombe la Muungano ambapo bingwa alikuwa anaenda kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.

Lakini hii kwa sasa baada ya Zanzibar kupata uanachama CAF katika Tanzania Bara na Visiwani zinapata mabingwa wake kupitia ligi zao ambazo wanaenda kushiriki michuano ya Afrika.

Ukiangalia msimamo wa ligi hiyo, ni dhairi timu hizi tatu za Yanga, Azam na Simba bado zipo katika vita kali ya kutaka kuwa bingwa msimu huu ili ziweze kuliwakilisha Taifa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani.

Wakati Yanga, Azam na Simba zikiwa kwenye vita hiyo, lakini Coastal Union, Africans Sports na Mgambo Shooting wao wakisaka nafasi ya kujinasua mkiani ili zisishuke daraja. Ukiangalia Coastal Union inaburuza mkia ikiwa na pointi 22 huku mahasimu wao, African Sports yenye pointi 23 inashika nafasi ya 15 sawa na Mgambo iliyopo nafasi ya 14 lakini zikitofautiana wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Ila leo nizungumzie mambo yaliyofanywa na Shirikisho la Kandanda Nchini (TFF) na kusabisha kupoteza ladha ya Ligi Kuu Tanzania Bara huku ikiwa inafikia tamati mwishoni mwa mwezi huu.

Kwanza nianze na hili tatizo sugu la panga-pangua ya ratiba ya ligi hiyo, ambapo kinamna moja ama nyingine kumesababisha kupoteza ladha ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Ratiba ya ilikuwa inapanguliwa kila siku hadi kusababisha baadhi ya klabu kuwa na viporo vya michezo mitatu! Na hii ilikuwa ni aibu kubwa maana hakuna ligi yoyote duniani ambayo inaweza kupishana viporo zaidi ya mechi mbili ama tatu na timu nyingine ambazo zinashiriki ligi hiyo.

Madudu ya TFF yalijionesha mapema baada ya ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom msimu wa 2015/2016 kutolewa, ambapo ilishuhudiwa wiki nzima ikipotea bila kuwapo mchezo hata mmoja wa ligi kwa sababu tu kulikuwa na mechi za Taifa Stars za kirafiki za kimataifa, pamoja na zile za kuwania kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika 2017 na Kombe la Dunia 2018.

Hakukuwa na mantiki yoyote kwa ligi hiyo kutoendelea kwa sababu wachezaji wanaounda timu ya Taifa wanatoka katika klabu mbalimbali za ligi na kanuni zinasema timu ambayo ina wachezaji watano kwenye kikosi cha Taifa Stars ndiyo inayoweza kuahirishiwa mchezo wake wa ligi.

Kituko kikubwa kikajitokeza baadaye ambapo TFF ilisimamisha ligi (kwa mujibu wa ratiba yake) kwa siku 37 “kupisha mechi za kimataifa za kirafiki za Taifa Stars pamoja na mechi mbili za kuwania kufuzu kwa Kombe la Dunia, Mashindano ya Kombe la Chalenji, Kombe la Mapinduzi na usajili wa dirisha dogo”.

 

Hiki kilikuwa kituko kikubwa na TFF haikulenga kulisaidia soka la Tanzania kwa sababu katika kipindi cha mwezi mzima wachezaji hawajishughulishi na mchezo wowote, hatua ambayo inaweza kushusha viwango vyao vya mchezo.

Soka ndiyo ajira ya wachezaji wetu na wanapaswa kushiriki mashindano lakini siyo kusimamishwa kwa ligi kwa mwezi mzima. Siku chache kabla ya kuanza kwa mzunguko wa pili wa ligi kuu ‘matajiri wa Bongo’ Azam wakaondoka kwenda kushiriki bonanza huko Zambia lililoshirikisha timu za Zesco United na Zanaco za Zambia pamoja na Chicken Inn ya Zimbabwe, huku ikijitetea kwamba hayo ni maandalizi kwa ajili ya mechi yake ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Bidvest Wits ya Afrika Kusini.

 

Ajabu ni kwamba mwaliko wa bonanza hilo haukuletwa na Chama cha Soka cha Zambia (FAZ), bali Azam ilialikwa na klabu ya Zesco.

 

Hii ilikuwa ni aibu ya mwaka licha ya Rais wa TFF, Jamal Malinzi, kujitetea na kuomba radhi, lakini hatua muhimu zaidi ambayo ingefaa kuchukuliwa ni kwa kiongozi huyo kujiuzulu na siyo kujitetea kwamba yeye alikuwa nje ya nchi wakati ruhusa hiyo ikitolewa. Jambo la kusikitisha zaidi ni kwamba, Bodi ya Ligi pamoja na TFF wenyewe wamekuwa wakirushiana mpira kwamba hawajui nani aliyewapa ruhusa Azam.

 Azam isingeweza kuondoka bila kuruhusiwa. Kuna watu waliotoa ridhaa hiyo – iwe kwenye Bodi ama TFF na kwa hakika walikidhalilisha chombo hicho kikuu cha usimamizi wa soka nchini.

Kuna baadhi ya matukio ambayo yalitokea kwenye mechi kama mshambuliaji wa Yanga, Donald Ngoma, ambaye alimpiga Hassan Ramadhani ‘Kessy’ wa Simba katika mechi yao. Cha kushangaza, mechi ile imechezwa Februari 20 mwaka huu lakini hukumu yake imekuja kusikilizwa wikiendi iliyopita.

Matatizo mengi yalitokea na yalisikilizwa kwa haraka na kutolewa uamuzi, sasa tatizo hili la Ngoma ambalo lilitokea miezi miwili iliyopita kwanini halikusikilizwa?

Huu ni uozo wa TFF na kamati zake ambazo zimeshindwa kusimamia weledi wa kazi zao na kuonekana shirikisho hilo limesimama upande mmoja wa kuzibeba baadhi ya klabu.

Matatizo kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, TFF iliingia katika kashfa ya rushwa ya kupanga matokeo ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kiasi cha waamuzi na viongozi wa shirikisho hilo kutia mchanga vitumbua vyao.

Hiyo ilitokana na kukariri mifumo ya soka ya zamani kwa kuzipandisha

klabu kwa ‘magumashi’, kitu ambacho msimu huu jipu hilo limefahamika. Ukiangalia katika Kombe la Shirikisho (FA) ambalo limefikia fainali ambayo itazikutanisha Azam FC dhidi ya Yanga ilikuwa na matatizo lukuki na kupoteza ladha.

 

Udhaifu wa TFF waliuonesha katika nusu fainali ya Kombe

hilo kati ya Yanga na Coastal ambapo mchezo huo ulivunjika baada ya dakika ya 110 kutokana na mashabiki wa Coastal kufanya fujo.

 

Mchezo ule uliharibiwa na refa Abdallah Kambuzi,  alishindwa kumudu mikiki mikiki ya mechi ile. Lakini ajabu TFF wanamfungia Kambuzi mwaka mmoja kuchezesha soka hapa nchini huku mwamuzi namba mbili, Charles Simon, ameondolewa kwenye ratiba ya waamuzi kwa kuzingatia Kanuni ya 38(1) ya Ligi Kuu.

 

Simu 0652933918 ama 0786733729

Email: [email protected]