*Aliunda Kamati ikawa ndiyo Menejimenti
*Murunya naye ahusishwa kufaidi mabilioni
*Wameuza hadi mapitio ya wanyamapori
*Faru wengine watatu hawajulikani waliko
Timu ya ukaguzi iliyoundwa kukagua ‘madudu’ katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), imeanika ufisadi wa kutisha, JAMHURI inathibitisha. Spika wa zamani, Pius Msekwa, ni miongoni mwa watu mashuhuri ambao ripoti hiyo imependekeza wafikishwe mbele ya vyombo vya sheria kujibu tuhuma za ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka. Msekwa ndiye aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka hiyo inayosifika kwa ufisadi.
Huu ni mtihani mgumu kwa Kagasheki na uongozi wa juu wa Serikali, kwani Msekwa anaonekana kuwa mtu anayepaswa kuachwa ‘apumzike’ kutokana na utumishi wake kwa Taifa. Mbali ya kuwa Spika Msekwa amewahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Makamu Mwenyekiti wa CCM (Tanzania Bara), Mwenyekiti na mjumbe katika Tume na Kamati mbalimbali.
Historia ya mapambano dhidi ya ufisadi nchini kama ilivyo, inaweza kuendelea kumlinda licha ya ‘madudu’ mengi yaliyobainishwa kwenye ripoti ya Timu iliyoundwa na Waziri Kagasheki.
Mwingine ambaye hawezi kuchomoka kwenye kashfa hii ni aliyekuwa Mhifadhi Mkuu wa NCAA, Bernard Murunya. Kwa sasa Murunya ni Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki.
Kiongozi wa Timu hiyo ya watu watano alikuwa Flora Masami. Wengine ni Ali Mnyami, Evaristo Mwalongo, Leonard Lyatuu na Canius Kalamaga ambaye alikuwa Katibu.
Habari zilizopatikana zinasema ripoti hiyo tayari imeshawasilishwa kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki. Uchunguzi unaonesha kuwa waziri alikabidhiwa Julai 27, mwaka huu. Ilianza kazi Juni 3, mwaka huu.
Uzito wa yaliyomo kwenye ripoti hiyo yamemfanya Balozi Kagasheki asite kuchukua hatua zikiwamo za kisheria kwa watuhumiwa, jambo linalomlazimu aombe ushauri kutoka ngazi za juu za uongozi wa nchi.
Msekwa anatajwa kuwa kwa kutumia nafasi yake kama Mwenyekiti wa Bodi, aliweza kuifanya bodi hiyo ifanye kazi za Menejimenti ya NCAA. Kazi hizo ni pamoja na kupanga safari, hasa za nje ya nchi.
Chanzo cha habari kimesema, “Mambo mengine yanatia aibu, bodi ilijitwalia kazi za menejimenti kwa asilimia zaidi ya 90. Hata kwenye ununuzi wa vifaa kazi zilifanywa na bodi.”
Mambo mengine yaliyobainika ni pamoja na mmoja wa viongozi wa NCAA kujitwalia zabuni ya kazi mbalimbali, hasa za ukarabati za barabara ndani ya Mamlaka.
Kazi za menejimenti zilihodhiwa na Kamati iliyoundwa na Msekwa na kuongozwa na yeye mwenyewe. Kamati hiyo ilishughulikia nyaraka za malipo, maduhuli na mambo mengi ambayo kawa kawaida yanapaswa kufanywa na menejimenti.
Msekwa anaandamwa zaidi na uamuzi wake wa kuruhusu ujenzi wa hoteli hata kwenye maeneo ambayo ni mahsusi kwa uhifadhi, yakiwamo mapito (ushoroba) wa faru.
Dosari nyingine iliyojitokeza ni ya kutojulikana waliko faru watatu kwa muda wa miaka saba sasa. Faru hao hawaonekani, lakini Timu ilipoiuliza menejimenti ilijibiwa kuwa hawaonekani, lakini nyayo zao zinaonekana mara kwa mara!
“Fikiria, faru hawaonekani kwa miaka saba, lakini eti nyayo zao zinaonekana, hii inaingia akilini kweli? Hapa utaona kuwa faru hao walishauawa, na menejimenti haijaripoti popote,” kimesema chanzo kilichoisoma ripoti hiyo.
‘Madudu’ mengine yaliyoibuliwa yanahusu Kampuni ya Utalii ya Masek Tented Lodge, ambayo kwa miezi minne imebainika kuiingizia Serikali hasara ya Sh zaidi ya milioni 160 kwa msaada wa watumishi wa Mamlaka.
Wakati kampuni hiyo ikiwa inajaza wageni 40, kwenye taarifa za NCAA inaonekana kuwa wageni waliokuwa wakiingia kwa kipindi hicho ni kati ya asilimia 28 hadi asilimia 63.
Wakubwa waanza kumwandama Kagasheki
Baadhi ya watuhumiwa kwenye ufisadi huu wameshabaini kilichomo kwenye ripoti ya Timu iliyoundwa na Waziri Kagasheki.
Hatua imewafanya baadhi yao wawatumie wanasiasa kutaka kuyumbisha mambo. Miongoni mwa wanasiasa wanaotajwatajwa, ingawa mwenyewe amekuwa akikana, ni Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa (Chadema).
Msigwa alianza kumwandama Balozi Kagasheki wiki chache baada ya waziri huyo kukabidhiwa wizara hiyo. Hata hivyo, ilikuja kubainika kuwa Msigwa alikuwa akitumiwa na mfanyabiashara Nyaga Mawalla kufanikisha kile alichopigania, hasa ugawaji vitalu vya uwindaji wa kitalii. Mawalla alifariki dunia mapema mwaka huu.
Msigwa anatajwa kuwa karibu na mfanyabiashara huyo, kiasi cha kutumia maandiko yake na kuyawasilisha bungeni kama kauli rasmi ya Kambi ya Upinzani Bungeni kwa Wizara ya Maliasili na Utalii.
Mwingine anayetajwa ni Mbunge wa Kahama na Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli.
Ingawa Kagasheki na Lembeli wanatajwa kama marafiki, kwa siku za karibuni urafiki huo umekuwa ukidorora kwa kile ambacho chanzo cha habari kinasema ni uamuzi wa Lembeli wa
kutumiwa ‘kumuumiza’ Kagasheki.