Na Mwamvua Mwinyi,JamhuriMedia,Bagamoyo
Baraza la Madiwani Halmashauri ya Bagamoyo,mkoani Pwani limepiga marufuku ongezeko la malipo ya gari la wagonjwa kwa wateja wanaopata rufaa hospital ya Wilaya ya Bagamoyo kwenda Hospital ya Muhimbili ama Muhas -Mloganzila kwa gharama ya sh.85,000 badala ya 50,000 .
Kufuatia hali hiyo baraza limemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bagamoyo, Mganga Mkuu wa wilaya kufanya ufuatiliaji na kutenda haki ,na endapo akigundulika anayekwenda kinyume na maamuzi ya vikao achukuliwe hatua.
Akitoa msimamo wa baraza hilo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bagamoyo, Mohammed Usinga alieleza , ufuatiliaji ufanyike katika utendaji huduma za afya katika hospital hiyo ili kupunguza malalamiko kutoka kwa Wananchi.
Aliongeza kueleza ,wagonjwa wanatozwa kinyume na vikao vya kisheria vilivyokaa ambapo gharama ya uchangiaji kwa wagonjwa ilipitishwa kuwa 50,000 ili kugharimia mafuta ya gari.
“Haikubaliki kuona wananchi wananyanyasika na kufikia hatua ya kuchelewa katika hospital za rufaa na kusababisha madhara makubwa ya kuzidiwa kwa mgonjwa ama kifo, kisa mizozano ya kulipishwa gharama kubwa”.
Alieleza ,awali wananchi walitakiwa kuchangia 30,000 ,baada ya gharama za mafuta kupanda vikao vikajadili na kukubaliana 50,000 Lakini cha kushangaza hospital inatoza wananchi 85,000 ikiwa ni kinyume na maamuzi ya vikao.
Vilevile Usinga, amesikitishwa na gharama kubwa ya huduma ya upasuaji, wagonjwa kulipishwa 150,000 gharama ambayo ni kubwa .
“Kinachofanyika hospital yetu ya wilaya haifanyi haki, 150,000 ni kubwa ,mgonjwa akihoji anaambiwa ni fedha za dawa na huduma na risiti za malipo hawapewi, suala hili lifuatiliwe ili kurejesha Imani kwa Serikali na Chama Cha Mapinduzi ambacho kinasimamia sekta zote na utekelezaji wake”amefafanua Usinga.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bagamoyo, Shauro Selenda amekiri kwa ongezeko la malipo ya uchangiaji wa mafuta na kusema Bei ya gharama ya mafuta imepanda na kusababisha changamoto hiyo.
“Bei ya mafuta imetoka sh.2,000 Hadi sh3,000 na zaidi ya hapo ,kwa mchango wa Halmashauri upo pale pale Lakini ongezeko linakuwepo kwa gharama zinazozidi”ameeleza Selenda.
Usinga alikana kwa ufafanuzi huo na kueleza,endapo ingekuwa ni ongezeko la mafuta wananchi wangechangia 50,000 na fedha ya ziada iliyoongezeka Lakini sio gharama yote ya 85,000 inayotakiwa kwa rufaa kutoka hospital ya Bagamoyo hadi Muhas.
Alielekeza kama Kuna changamoto, mapendekezo yapelekwe katika vikao vya kisheria ili ijadiliwe na kufanyiwa marekebisho badala ya kufanya Maamuzi kiholela.
Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, Muharami Mkenge,alisema hali ya utoaji huduma za afya hospital ya wilaya ni mbaya, utendaji kazi hauendi vizuri.
“Nikiwahi kufika usiku pale nikiwa na gari ambalo halijulikani, nikakuta wagonjwa Lakini madaktari sijui walikuwa wapi ,nikaulizia huduma za uzazi unakuta mzazi analipia dawa na huduma haziridhishi mganga Mkuu fuatilia”amesisitiza Mkenge.
Hoja na malalamiko hayo yaliibuliwa na diwani viti maalum, Sinasudi Rashidi Honelo ,ambae alitaka ufafanuzi na kuona namna ya kusaidia wananchi wanapokuwa wagonjwa na kupewa rufaa huku wakigharamia fedha yote bila kuona Halmashauri, hospital ikishiriki kwenye uchangiaji.