Ushirikiano Tanzania, Indonesia waimarishwa
Madini ya Kimkakati kupewa kipaumbele
Balozi wa Indonesia nchini Tanzania Mhe. Tri Yogo Jatmiko amesisitiza kushirikiana na Tanzania katika kutangaza Mwelekeo Mpya wa Wizara wa VISION 2030: Madini ni Maisha na Utajiri ili kutangaza fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo katika Sekta ya Madini Nchini.
Balozi Jatmiko amesema hayo leo Septemba 20, 2023 jijini Dodoma mara baada ya mazungumzo mafupi na Katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali katika kikao kilicholenga kujenga mahusiano baina ya nchi hizo mbili katika shughuli za uchimbaji madini
“Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilimbali mbalimbali za madini ambazo ni muhimu na zinahitajika duniani. Kupitia Dira hiyo Sekta ya Madini inakwenda kutangaza nchini Indonesia na kueleza wawekezaji fursa mbalimbali zilizopo,” amesema Mhe. Jatmiko.
Ameongeza kuwa, kutokana na mahitaji makubwa ya matumizi ya nishati hiyo hususan magari ya umeme katika nchi hiyo, Serikali ya Indonesia itaweka vipaumbele katika matumizi ya madini mkakati kutoka nchini Tanzania ili waweze kukidhi mahitaji yao katika matumizi mbalimbali ya vifaa vya umeme.
Katika hatua nyingine, amempongeza Waziri wa Madini Mhe. Antony Mavunde kwa kuteuliwa na kuapishwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Waziri wa Madini. Amesema nchi hiyo itatoa ushirikiano wa kutosha nchini ili kuvutia uwekezaji katika Sekta ya Madini.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali amesisitiza nchi hiyo kutoa ushirikiano katika kuwajengea uwezo wataalam mbalimbali wa wizara na taasisi katika maeneo ambayo yatahitajika ikiwemo mafunzo ya Uongezaji Thamani Madini na mafunzo maalum kwa wakufunzi wachache ambao watakuwa walimu katika kutoa mafunzo maeneo muhimu.
Pia, ameeleza fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo katika Sekta ya Madini ikiwemo ushirikiano katika uchimbaji wa madini ya dhahabu na madini ya kimkakati. ‘’Tunahitaji ushirikiano katika maeneo ya uchimbaji wa madini hayo kupitia Shirika la Madini la Taifa STAMICO na sisi Serikali tutatoa ushirikiano ili uchimbaji wa madini hayo ufanyike hapa nchini,” amesema Mahimbali.
Vile vile, amewakaribisha kushiriki katika Jukwaa la Kimataifa la Uwekezaji katika Sekta ya Madini linalotarajiwa kufanyika Oktoba 25 na 26 mwaka huu. Amesema jukwaa hilo litatangaza fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo nchini.
Kikao hicho kifupi kimehudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo, Kamishna wa Madini Dkt. AbdulRahman Mwanga pamoja na wataalam mbalimbali wa Wizara.