Serikali imetafuna mfupa mgumu ambao umepigiwa kelele na wananchi kwa muda mrefu, kwa kupeleka bungeni miswada wa marekebisho ya sheria kuwapa Watanzania haki ya kufaidi madini yao.
Sheria zinazopendekezwa kurekebishwa ni; Sheria ya Madini, Sura ya 123(The Mining Act, Cap.123), Sheria ya Petroli, Sura ya 392 (The Petroleum Act, Cap. 392), Sheria ya Kodi ya Mapato, Sura ya 332 (The Income Tax Act, Cap. 332), Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, Sura ya 148 (The Value Added Tax Act Cap. 148), Sheria ya Bima, Sura ya 394 (The Insurance Act, Cap. 394) pamoja na Sheria ya Usimamizi wa Kodi, Sura ya 438.
Muswada huo wa marekebisho ya sheria mbalimbali (Miscellaneous Amendment, 2017) , uliopelekwa sambamba na miswada mingine miwili; Sheria ya Mamlaka ya Nchi Kumiliki Maliasili wa Mwaka 2017 na Muswada wa Sheria ya Mapitio na Majadiliano Kuhusu Masharti Hasi katika Mikataba Inayohusu Maliasili za Nchi, kwa pamoja inaandika historia mpya.
Serikali imepeleka miswada hiyo ya sheria mipya na kuliongezea Bunge siku hadi Julai 5, 2017 badala ya kumalizika Juni 30, kwa nia ya kuhakikisha sheria hizo zilizopelekwa chini ya hati ya dharura zinapita.
Uamuzi wa Serikali umeegemea maazimio ya Umoja wa Mataifa Na. 523(VI) la Januari 12, 1952 na Azimio Na 626(VII) la Disemba 21, mwaka 1952 yanayoipa kila nchi huku haki ya kumiliki rasilimali za taifa lake milele.
Katika kutunga sheria hizo mpya, Serikali pia imerejea Azimio Na 1314 (XIII) la Desemba 12, 1958; Na. 1515(XV) la Desemba 15, 1960; Na. 1803(XVII) la Desemba 14, 1962; Na. 2158(XXI) la Disemba 6, 1966; Na XXV la Desemba 11, 1970 na Azimio Na 32 la Desemba 12, 1974.

Serikali inataka hatua yoyote itakayochukuliwa kuhusu uwekezaji wa rasilimali za taifa inatambua na kuzingatia haki ya Jamhuri ya Muungano kama taifa huru na lenye mamlaka kusimamia na kutumia rasilimali zake kwa masilahi ya taifa.
Kwa pamoja miswada hii inalenga kuimarisha mifumo ya udhibiti, uwajibikaji, umiliki, usimamizi wa maliasili na kupanua wigo wa makusanyo ya kodi katika sekta ya uziduaji; gasi, madini na petroli.
Akizungumza kuhusu miswada hiyo, Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi, ambaye kitaaluma ni Mwansheria, amesema lengo la muswada huo ni kubadilisha vifungu vya Sheria kwa kufuta baadhi ya vifungu vya Sheria vinavyokandamiza haki ya Watanzania kumiliki na kufaidi rasilimali za taifa na kuviandika upya kwa nia ya kuipa Serikali wigo mpana wa kuisimamia sekta ya madini.
“Mabadiliko yanayokusudiwa yatatambua na kuweka umiliki wa madini, petroli na gesi asilia kwa wananchi chini ya usimamizi wa Rais kwa niaba ya wananchi tofauti na ilivyokuwa hapo awali… mabadiliko yanaipa serikali umiliki na mamlaka ya mazao yote yanayopatikana katika uchimbaji, uchakataji na uchenjuaji wa madini, ikiwa ni pamoja na makinikia.
“Serikali itakuwa na haki na dhamana juu ya makinikia na kuweka utaratibu wa kuyahifadhi sehemu maalumu migodini, kutambua na kuweka chini ya uangalizi wa Serikali maeneo yote ya uchimbaji wa madini, ikiwa ni pamoja na ulinzi mahsusi wa maeneo yote ya uchimbaji wa madini,” amesema Prof Kabudi.
Waziri huyo amesema kupitia miswada hiyo, utaanzishwa utaratibu wa Serikali kufanya ukaguzi na udhibiti wa uzalishaji wa madini, huku Serikali ikipewa uwezo wa kisheria, kudhibiti na kutambua viwango vya madini yote yanayotolewa kwenye maeneo ya migodi.

Sheria zabana wawekezaji
Miswada ya sheria iliyopelekwa chini ya hati ya dharura ikipitishwa, hakika inabadili mfumo na mchezo wote katika sekta ya madini.
Wakati zamani ilikuwa Waziri (mwenye dhamana na madini) anakutana na mwekezaji nje ya nchi anatia saini mkataba wa madini kwa niaba ya nchi, hivi sasa si hivyo tena na enzi hizo zimekwisha.
“Kwa mujibu wa aya (c) na (i) za Ibara ya 9 ya Katiba [ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania], itakuwa ni kinyume cha sheria kuingia makubaliano au mkataba wowote katika uziduaji, uvunaji au umilikishaji na matumizi ya utajiri na maliasili, isipokuwa ambapo masilahi ya Watanzania na Jamhuri ya Muungano yametiliwa maanani na kuridhiwa na Bunge la Taifa,” inasema sehemu ya 6 ya Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Nchi Kumiliki Maliasili wa Mwaka 2017.
Kifungu cha 9 cha Muswada wa Sheria hii ambayo kuna kila dalili kuwa itapita, kinataka kila mwekezaji kujenga mitambo ya kusafisha madini hapa nchini au kueleza mpango wa jinsi gani atasafisha madini hapa nchini, huku kikipiga marufuku kuuza nje ya nchi madini ghafi.
Pia wawekezaji chini ya kifungu cha 10 wanapoteza uhuru wa kuhifadhi fedha zitokanazo na biashara ya madini hapa nchini kwenye akaunti za benki za kigeni nje ya nchi. Fedha zote zitakazotokana na uuzaji wa madini nje ya nchi zinapaswa kuhifadhiwa katika benki za ndani hapa nchini, isipokuwa tu mwekezaji ataruhusiwa kupeleka nje ya nchi sehemu ya gawio au faida aliyopewa kutokana na gawio.
Kama kuna jambo jema sheria hii italeta, basi ni kuipa heshima Katiba ya Tanzania na mahakama za ndani kwa kusimamia dhana ya ukuu wa sheria. Kifungu cha 11 cha Sheria ya Mamlaka ya Nchi Kumiliki Maliasili wa Mwaka 2017, kinataka mkataba wowote utakaoingiwa kutamka bayana kuwa mgogoro wowote utakaotokea katika muda wa utekelezaji wa mkataba utatatuliwa kwa kutumia mahakama za Tanzania na si za kimataifa.
Kabla ya ujio wa sheria hii, mikataba karibu yote ilikuwa haitambui sheria za ndani, badala yake ilikuwa inataka kila mwekezaji anapokuwa na tatizo la kimkataba kupeleka kesi yake nje ya nchi hali iliyokuwa inaliingiza hasara kubwa taifa kuendesha kesi, lakini pia kuifanya mikataba ya uzalishaji (PSA) kuwa na nguvu kubwa za kisheria na kuwa juu ya Katiba na Sheria za nchi.
Muswada wa Sheria ya Mapitio na Majadiliano Kuhusu Masharti Hasi katika Mikataba Inayohusu Maliasili za Nchi, 2017 katika kifungu cha pili unalipa Bunge mamlaka ya kupitia mikataba iliyosainiwa kabla ya sheria hiyo kuanza kufanya kazi na yote itakayosainiwa baada ya sheria hiyo kupitishwa.
Vifungu vya 4 na 5, vinaitaka Serikali kulifahamisha Bunge kuwa imeingia mkataba na taasisi au kampuni yoyote ndani ya siku sita, na iwapo Bunge litakuwa na maelekezo mahususi kwa njia ya Azimio, ambapo Serikali nayo ndani ya siku 30 baada ya Azimio la Bunge inapaswa kumjulisha mwekezaji masharti yasiyokubalika kwa nia ya kurejea kwenye majadiliano.
Mwekezaji asipowahisha au akagoma kuendelea na majadiliano kwa zaidi ya siku 90, masharti yaliyokuwa yamelalamikiwa na Bunge ndani ya Azimio, yanakuwa yamejifuta kwenye mkataba huo na hivyo Serikali kuwa na mkataba wenye masharti yasiyo hasi kwa nchi.

Zitto azungumza
Akizungumza na JAMHURI, Kiongozi wa Chama Cha ACT-Wazalendo, ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, amesema kwa takribani miaka 10 sasa kumekuwa na harakati za wananchi na wanasiasa wa vyama vya upinzani kupitia Bunge kudai mabadiliko kwenye Sheria zinazosimamia maliasili za nchi.
Zitto amesema, juhudi za kuleta mabadiliko ya sheria za madini zilikuwa kubwa zaidi na kuanza kushika kasi baada ya sakata la mkataba wa mgodi wa Buzwagi la mwaka 2007, hivyo mwezi huu mjadala unatimiza miaka 10.
“Mjadala huo ulisababisha kutangazwa kwa Azimio la Songea la Septemba, 2007 na kisha kuundwa kwa Kamati ya Jaji Mark Bomani, miezi miwili baadaye, kamati hiyo ilikabidhiwa jukumu la kuipitia mikataba yote ya kuvuna rasilimali madini, kisheria na kisera.
“Taarifa ya Kamati ya Jaji Bomani iliwezesha kutungwa kwa sheria mpya ya Madini ya mwaka 2010, kutokana na sera ya Madini ya mwaka 2009. Tangu mwaka 2010 kumekuwa na mabadiliko ya sheria mbalimbali za masuala ya fedha zilizojaribu kurekebisha hali ya nchi yetu kutofaidika na sekta ya madini,” amesema Zitto.
Anasema takwimu rasmi za Serikali zinaonesha kuwa kati ya mwaka 2000 – 2016, Tanzania imeuza nje ya nchi madini yenye thamani ya Shilingi trilioni 50, Taifa lilipata mapato ya Shilingi trilioni 3, kiwango ambacho kiko chini ya asilimia 10 ya mauzo yote ya madini. Sekta ya madini imekuwa ikichangia asilimia 40 ya mauzo yote ya nje ya nchi, huku ikichangia asilimia 4 tu ya pato la taifa.
Zitto ameliambia JAMHURI, chama chake cha ACT-Wazalendo, kimetoa mapendekezo kadhaa kwenye muswada wa sheria ya ‘The Natural Wealth and Resources (Permanent sovereignty) Act, 2017.’
Kifungu cha 4 (3) kiongezwe maneno ‘Natural wealth and resources shall be extracted in such a manner that the right (mineral right) is held by the state through a designated public entity and that the model shall be a production sharing agreement’.
Zitto amesema, madhumuni ya marekebisho hayo ni kuwezesha uwepo wa Shirika la Umma ambalo ndio litakuwa na hati ya umiliki (mineral right) badala ya hati hiyo kuitoa kwa Kampuni za uwekezaji.
“Shirika hilo la Umma litaingia mikataba ya kugawana mapato na wenye mitaji watakaowekeza kwenye kuvuna utajiri wetu. Mfumo huo utaendelea kutambua madini kuwa mali ya Taifa, na mchimbaji/mwekezaji kuwa mkandarasi kwenye uvunaji,” amesema kiongozi huyo wa chama.

Katika kifungu cha 5 (3) cha muswada huo, chama hicho kimependekeza kiandikwe upya kwa kuongeza maneno kwamba “ni lazima kupata kwanza kibali cha wananchi wa eneo husika kabla ya kupewa leseni ya kutafuta na kuchimba madini kwenye eneo hilo (principle of free prior informed consent).”
Malengo ya kuongeza kipengele hicho ni kuwapa nguvu wananchi watakaoathirika na uvunaji wawe na sauti kuanzia hatua ya awali kabisa. Kibali cha wananchi kitawezesha pia wenye mitaji kuingia makubaliano ya kimaendeleo na wananchi kabla ya kuanza kuvuna utajiri. Sababu kubwa ya kifungu hicho ni kuondoa migogoro kati ya wenye mitaji (wawekezaji) na wananchi wanaozunguka migodi.
Mapendekezo mengine ni kuwapo mabadiliko kwenye kifungu cha 12 Maneno “May be” yaondolewe na badala yake maneno “Shall be” yaongezwe. Hiyo italipa Bunge mamlaka zaidi kwani kitafsiri ya kisheria neno “may” halimlazimishi mtu au chombo kufanya jambo husika lakini neno “shall” linamlazimisha mtu au chombo kufanya jambo hilo.
Chama hicho kinapendekeza mabadiliko kwenye kifungu cha 14, kiongezwe kwamba “mabadiliko yeyote ya sheria hiyo yatafanywa iwapo tu kutakuwa na kura ya maoni (referendum) ambayo asilimia 75 ya watu wenye umri wa kupiga kura wataunga mkono”.
Uwepo wa kifungu hicho ni kuufanya muswada kuwa wa wananchi na kuzuia uwezekano wowote wa Serikali yeyote kubadilisha sheria hiyo kirahisi bila kupata ridhaa ya wananchi wenyewe.
Katika muswada wa pili wa ‘The Natural Wealth and Resources Contracts (Review and Renegotiation of unconscionable terms) Act, 2017’. Zitto amesema chama chake kinapongeza hatua hiyo kubwa ya kuhakikisha mikataba yote ya rasilimali za nchi itakuwa inawasilishwa Bungeni kwa ajili ya kuidhinishwa.
Katika kipengele cha kuidhinishwa bungeni, Mbunge huyo ameliambia JAMHURI, mabadiliko yeyote ya sheria hiyo, yatakuwa yamepitishwa iwapo theluthi mbili ya wabunge wataunga mkono, malengo ya kufanya hivyo ni kuweka ulinzi wa kutosha kwenye sheria hiyo isichezewe na chama chochote cha siasa kitakachoingia madarakani.
Amesema katika kulipatia Bunge, mamlaka ya kupitia mikataba husika pamoja na kuingia katika kuitazama upya mikataba hiyo (renegotiation) basi Kifungu cha 4 (1) neno “May” libadilishwe na badala yake liingizwe neno “Shall”.

Wabunge watoa ya moyoni
Akichangia katika mjadala huo, Mjumbe wa Kamati Maalum ya Sheria, Mbunge wa Bukene, Suleiman Zedi, amehoji iwapo miswada hiyo imekuja na majibu ya kuwazuia, wawekezaji katika makampuni ya uchimbaji madini kufanya uthamini wa madini kama mali yao na kutumia utafiti huo kuomba mikopo.
Pia amehoji kuhusu sera ya madini kuzungumzia “Free Market Economy (Soko Huria)” ambapo miswada hii inayopendekezwa inalenga katika “Public Command Economy (Uchumi Hodhi)”
Taska Mbogo, Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Arusha, amehoji iwapo miswada hiyo imegusa taratibu za utafiti wa madini na makampuni ya madini kufungua bima hapa nchini. Amesema Tanzania haipo katika orodha la watunza dhahabu duniani na kwamba Benki Kuu haina mamlaka ya kutunza kiwango kikubwa cha dhahabu, jambo ambalo si sahihi. Tanzania ni ya tatu duniani kwa kuzalisha dhahabu kwa wingi baada ya Afrika Kusini na Ghana. Zipo taarifa kuwa Sierra Leone imechukua nafasi ya tatu kwa wingi wa dhahabu, ila hazijathibitishwa.

Akijibu hoja hizo Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi amesema taarifa zote zinazohusu madini chini ya miswada hiyo itakuwa mali ya serikali.
“Kutaanzishwa hifadhi ya dhahabu pale Benki Kuu kwasababu thamani ya madini hupanda na kushuka. Hapa inamaana kuwa dhahabu ikishuka bei katika soko la dunia serikali iwe na haki ya kununua na kuuza pale bei inapopanda,” amesema Profesa Kabudi.
Amesema miswada hiyo inawataka wawekezaji kupata bima ya migodi hapa nchini na inazuia makampuni kufanya uthamini wa madini kama mali yao.
Prof. Florens Luoga, kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, amesema Serikali, kupitia miswada hiyo, ambayo ikipitishwa na Bunge na kusainiwa na Rais John Magufuli, itakuwa na haki ya kumiliki hisa za kuanzia asilimia 16 na kuendelea kutoka kwa makampuni za madini hapa nchini.

Amesema misamaha ya kodi kulingana na uzalishaji haitazidi miaka miwili, huku kampuni ya uchimbaji itakayosema haijatengeneza faida zaidi ya muda huo italazimika kulipa kodi.
Prof. Kabudi ameongeza kuwa miswada hiyo imefanya mapitio ya madaraka ya Waziri na Kamishina wa Madini kwa lengo la kupunguza baadhi ya majukumu na madaraka yao.
“Muswada unalenga kuunda na kuainisha kazi za Kamisheni ya Madini, kuanzishwa kwa hifadhi ya dhahabu na vito chini ya Benki Kuu, kuanzisha maeneo maalumu ya masoko ya dhahabu na vito, pamoja na kuanzisha mfumo mahsusi wa kukusanya na kuhifadhi taarifa zote za shughuli za madini.
Amesema muswada huo umeweka misingi ya Bunge kupitia, kujadili na kuridhia mikataba ya utafutaji na uendelezaji wa mafuta na gesi asilia. Mabadiliko hayo yanalenga kuhamasisha uanzishwaji wa viwanda vya kuongeza thamani madini hapa nchini.
Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni na Mbunge wa Hai (CHADEMA), Freeman Mbowe amesema kuna hatari kubwa Bunge kupitisha sheria zinazohusu sekta ya madini haraka, hivyo hazitatoa ufumbuzi wowote.
Akizungumza na JAMHURI, Mbowe amesema hakukuwa na uharaka wowote wa kuitisha mikataba hiyo kwa dharura wakati kuna mkutano mwingine wa bunge mwezi Novemba, mwaka huu, kwani uamuzi wa haraka hauleti umakini wowote.
Amesema pamoja na nia njema ya Serikali kuchunguza mikataba hiyo “tunapaswa kuchukua tahadhari kwani biashara ya gesi, mafuta na madini inahitaji umakini zaidi badala ya jazba ambazo hazitufikishi kokote.
“Napenda kurudia kusema serikali ina nia njema sana, lakini ubabe utatupeleka pabaya kama ilivyo kwa Zimbabwe ambao walifanya ubabe ambao umesababisha nchi hiyo kuporomoka kiuchumi,” amesema Mbowe na kuongeza:
“Wabunge wanaotunga sheria hizo sio wafanyabiashara wala wachimbaji wa madini na wengi wao hawafahamu biashara kubwa za kimataifa na kinachofanyika ni kutafuta sifa tu ndio maana Serikali hii inaendeshwa bila mipango yoyote.
“Maamuzi yanayofanyika Dodoma, hakuna mbunge yeyote wa CCM anayeweza kuelewa masuala ya biashara za kimataifa na kinachofanyika ni kutafuta sifa tu kwa wananchi ambao wengi wao uelewa wao ni mdogo,” amesema Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa CHADEMA.

Amesema kinachofanyika ni kutafuta sifa kwa watu kwa kuanzisha tukio na kabla halijapatiwa ufumbuzi linazimwa kwa kuanzisha tukio jingine; “Limetoka la makinikia likazimwa na IPTL, nalo litazimwa na tukio jingine na tawala zote za kibabe ndivyo zinavyoendeshwa sehemu mbalimbali na hatari zaidi ni kukosa mipango.
“Sekta ya madini inachangia asilimia ndogo sana katika pato la taifa na wala haimsaidii chochote mwananchi wa kawaida na watu wanatafuta sifa tu. mambo ya msingi na muhimu kwa wananchi kama kuinua sekta ya kilimo hayazungumzwi kabisa,” amesema.
Amesema sheria hizo zinazotungwa hazimwezeshi mwekezaji kuwa na uhakika na uwekezaji wake hapa nchini katika sekta za gesi, mafuta na madini. “Pia Watanzania tunapaswa kuelewa kwamba rasilimali hizi hazipo Tanzania pekee, lakini hata Kenya kuna dhahabu au Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), pia Msumbiji na Uganda kuna mafuta na gesi.
“Kwa kawaida kabla ya kupitisha sheria na mikataba tulipaswa kuwatumia wataalamu wetu kufanya utafiti wa kina hata kwa nchi kumi za jirani ambao ni washindani wetu kujua wao sheria na mikataba yao ikoje?
“Hakuna miradi yoyote iliyoasisiwa na serikali hii bali yote ilikuwa ya serikali ya awamu ya nne. Inahitajika mipango madhubuti, kwa hata suala la viwanda, ujenzi wa barabara za juu yote hayo yalikuwa yamefanyiwa mchakato wakati wa Jakaya Kikwete,” amesema Mbowe.

Taarifa ya Benki Kuu
Wakati Mbowe akisema madini hayana mchango mkubwa kwa taifa, Taarifa ya Mapitio ya Uchumi ya Mwezi inayotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaonyesha kinyume na kauli hiyo.
Kwa miaka mitano kuanzia mwaka 2013 – 2017 inaonyesha kuwa madini yamechangia zaidi ya asilimia 40 ya mauzo ya nje kama ifuatavyo: Mwaka 2013 kwa kipindi cha mwaka kinachoishia Aprili, Tanzania iliuza nje ya nchi bidhaa na huduma zenye thamani ya dola milioni 355.4, ambazo kati ya hizo dola milioni 126.5, sawa na asilimia 35.6 zilizotokana na madini.
Mwaka 2014 kwa kipindi kama hicho, Tanzania iliuza nje ya nchi mali na huduma zenye thamani ya dola milioni 315.5, kati ya hizo madini yalichangia dola milioni 95.8 (30.3%) na mwaka 2015 dola milioni 376.6, kati ya hizo madini yamezalisha dola milioni 115.4 (36.5%), mwaka 2016 dola milioni 505.1, kati ya hizo madini yalichangia 105.6 (20.9% na mwaka 2017 hadi Aprili, mwaka huu Tanzania imeuza dola milioni 338.2, ambapo kati ya hizo dola milioni 126.7 (37.4) zimetokana na madini.
Rais Magufuli mwezi Machi, mwaka huu aliamua kuzuia makontena yanayosafirisha mchanga kwenda nje ya nchi kuzuiwa na akaelekeza makontena hayo 277 yafanyiwe uchunguzi kote yaliko nchini. Uchunguzi huo uliofanywa na Kamati mbili alizoziunda umebaini kuwa nchi imepoteza mapato zaidi ya Sh trilioni 108 tangu nchi hii ilipoanza kusafirisha mchanga nje ya nchi, hali iliyomfanya aamuru sheria zibadilishwe chini ya hati ya dharura kulinda rasilimali za nchi.
Rais Magufuli amesema mara kadhaa kuwa Tanzania si nchi maskini kama inavyotajwa na baadhi ya watu bali kinachohitajika ni moyo wa uadilifu, uzalendo na usumamizi wa sheria kwa manufaa na masilahi mapana ya Watanzania na Tanzania kwa ujumla.

Bunge laongeza muda
Bunge limeongeza siku za Mkutano wa Saba hadi tarehe 05 Julai 2017, ili kupitia Miswada hiyo mitatu ya sheria inayohusu marekebisho ya Sheria za Madini na ulinzi wa rasilimali za Taifa.
Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema Kamati ya Uongozi ilikutana Juni 28, 2017 Jioni kufanya marekebisho ya Ratiba ya Mkutano wa Saba Bunge ambao ulitarajiwa kuisha Juni 30, 2017 na kukubaliana kuongeza siku tatu za kazi hadi Julai 5, 2017 kuliwezesha Bunge kupitia Miswada hiyo.
Spika alilieleza Bunge kuwa ameunda Kamati ya pamoja itakayopitia Miswada miwili ambayo tayari imeshasomwa kwa mara ya kwanza Bungeni. Miswada hiyo ni; Muswada wa Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu Masharti Hasi katika Mikataba ya Maliasili za Nchi wa Mwaka 2017 [The Natural Wealth and Resources Contracts (Review and Re-Negotiation of Unconscionable Terms)] Bill, 2017]; (iii) Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Nchi kuhusiana na Umiliki wa Maliasili wa Mwaka 2017 [The Natural Wealth and Resources (Permanent Sovereignty)] Bill, 2017].
Spika amesema Kamati ya pamoja itakayochambua miswada hiyo itaongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, Dotto Biteko na itajumuisha Wajumbe wa Kamati nne za Bunge ambazo ni Kamati ya Nishati na Madini, Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Kamati ya Katiba na Sheria na Kamati ya Sheria Ndogo.
Kwa upande mwingine, Spika amesema Kamati ya Katiba na Sheria chini ya Uenyekiti wa Mohamed Omary Mchengerwa, itauchambua Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2017 [The Written Laws (Miscellaneous Amendments) Bill, 2017].
Mjadala wa sheria hizi ulitarajiwa kuendelea jana na leo mjini Dodoma.

Habari hii imeandikwa na Mkinga Mkinga aliyeko Dodoma, Francis Kajubi na Clement Magembe, walioko Dar es Salaam.