DAR ES SALAAM
NA AZIZA NANGWA
Uuzaji wa mazao ya asili nje ya nchi umepungua kwa kiasi kikubwa katika miezi ya hivi karibuni kutokana na kuibuka kwa maambukizi ya virusi vya corona, Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, amethibitisha.
Akizungumza na JAMHURI mwishoni mwa wiki, Hasunga amesema ugonjwa huo umevuruga mifumo ya biashara na Tanzania ni moja ya nchi zilizoathirika.
JAMHURI lilimtafuta Hasunga kufuatia kuweko kwa tani 3,000 za korosho mkoani Pwani ambazo hazijapata mnunuzi kutoka nje ya nchi.
Kwa ujumla, kuibuka kwa ugonjwa huo kumesababisha kudoda kwa korosho mkoani Pwani na kusababisha mapato yake kushuka kwa asilimia 78 kutoka Sh bilioni 60 katika msimu uliotangulia hadi Sh bilioni 15 msimu uliomalizika.
Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika Mkoa wa Pwani, Rajabu Ng’onoma, amesema katika msimu huu wamepata hasara kubwa katika ukusanyaji wa mapato ikilinganishwa na misimu iliyopita kutokana na changamoto kadhaa, ikiwamo kuibuka kwa corona.
Ng’onoma ameeleza kuwa zao la korosho kwa kiasi soko lake lipo katika nchi za Asia, hasa India na Vietnam, ambazo kwa sasa zimesimamisha kupokea bidhaa kutoka mataifa mengi kutokana na kuibuka kwa korona.
“Bado tuna tani 3,000 za korosho katika maghala. Tangu zimenunuliwa mwaka jana bado hazijapata wateja. Hali hii imewaathiri sana wakulima pamoja na chama chetu kwa sababu tulitarajia kupata fedha kutokana na mauzo ya korosho hizo,” anasema.
Akizungumzia mipango ya baadaye, amesema wameshaanza utaratibu wa kuwasajili wakulima wote kama njia ya kuondoa migogoro kati ya benki na chama, kwani wakulima wasio waaminifu walikuwa wakipeleka maombi benki zaidi ya mbili wakitaka wapatiwe mkopo, jambo ambalo linawaongezea mzigo.
Waziri Hasunga amesema kuibuka kwa corona nchini China mwishoni mwa mwaka jana hakujaathiri korosho tu bali mazao mengine ambayo husafirishwa nje.
Amesisitiza kuhusu usajili wa wakulima kama njia ya kuwatambua ili iwe rahisi kwa serikali kuwapatia msaada na huduma wanazozihitaji kwa wakati.
Amesema serikali itaanza zoezi la uhakiki wa wakulima wote wakiwemo wadau wa kilimo, mashirika na NGOs zote nchini zinazojishughulisha na kilimo ili kuhakikisha wanakuwa na takwimu sahihi za idadi ya wakulima, wanamiliki kiasi gani cha ardhi ili iwe rahisi kupata soko la kuuza mazao yao.
Amedai hatua hiyo itasaidia zaidi kupata hali ya usalama wa chakula kwani kutakuwepo na takwimu sahihi za matarajio ya uzalishaji wa chakula kwa msimu, hivyo kuondoa upungufu wa chakula na mazao mengine ya kilimo.