Na Mwandishi Wetu

Kikosi cha Usalama Barabarani kimewakamata madereva 16,324 kwa makosa mbalimbali ya usalama barabarani na kuwafungia leseni madereva 14 katika kipindi cha Sikukuu ya Krismasi.

Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, William Mkonda pia aliwaelekeza wakuu wa usalama barabarani kote nchini kufanya operesheni kali usiku na mchana na kuwachukulia hatua madereva wanaofanya makosa hatarishi barabarani.

Mkonda alisema hayo juzi wakati akitoa taarifa kuhusu mfululizo wa ajali zilizotokea hivi karibuni na kusabaisha vifo vya watu zaidi ya 50 kwa kipindi cha mwezi mmoja.


“Kwa kipindi cha siku mbili (Krismasi na siku iliyofuata) madereva 14 walifungiwa leseni zao kwa makosa ya ulevi na mwendokasi na madereva 16,324 wamekamatwa kwa makosa mbalimbali ya usalama barabarani na kuandikiwa faini,” alisema.

Alitoa agizo kwa wakuu wa usalama barabarani kutofumbia macho madereva wanaokiuka sheria za usalama barabarani.

“Wakuu wa usalama barabarani wa mikoa na wakuu wa usalama barabarani wa wilaya na askari wote wa usalama barabarani kuendelea kufanya operesheni kali za usiku na mchana bila kumwonea mtu muhali dereva yeyote,” alisema.

Kamanda Mkonda pia, aliagiza kukamatwa kwa madereva wote wanaofanya makosa hatarishi barabarani pamoja na kuchukuliwa hatua za kisheria.

“Kwa dereva yeyote atakayekamatwa kwa makosa haya kwanza atalala mahabusu, tutamfungulia mashitaka na kuwapeleka mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria,” alisema.

Aliongeza: “Tutaendelea kuwafungia leseni zao wanaofanya makosa hatarishi… Jeshi la Polisi tutaendelea kuwa wakali kwa madereva wote watakaoendelea kupuuza na kutojali na kuvunja kwa makusudi sheria za usalama barabarani”.

Awali akitoa tathmini ya mwenendo wa ajali zilizotokea ndani ya wiki moja tangu Desemba 24, Mkonda alivitaja visababishi vikuu vya ajali hizo kuwa ni uzembe, kutokutii sheria za barabarani, mwendokasi, madereva kupenda kupita magari mengine sehemu isiyostahili na kuupuza sheria za barabarani.

Aidha, Jeshi la Polisi kikosi cha usalama barabarani kitaendelea kutoa elimu kwa watumiaji wa barabara ili kujenga uelewa na kupaza sauti pale dereva anapokiuka sheria za usalama barabarani.