Baadhi ya madereva wa magari ya viongozi wa serikali wanatajwa kuwa katika orodha ya madereva wanaongoza katika makosa mbalimbali ya uvunjaji wa sheria za barabarani Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Prescanne Business Enterprises Limited, Adelardo Marcel, amesema kwamba, madereva hao wamekuwa wakivunja sheria hizo makusudi kutokana na kuendesha magari ya viongozi mbalimbali nchini.
Adelardo aliyasema hayo wakati akitoa taarifa yake maalum ya tathmini ya utenda wa kazi wa kipindi cha mwezi mmoja iliyofanywa katika Manispaa ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
Kampuni ya Prescanne Business Enterprises Limited ya Jijini Dar es Salaam imepewa jukumu na mamlaka ya Jiji, kudhibiti matumizi mabaya ya barabara za Kinondoni kwa magari makubwa, ikiwamo uegeshaji kinyume na taratibu kwa magari ya aina yote.
Kampuni hiyo pia inawajibika kudhibiti uwapo wa gereji katika sehemu zisizoruhusiwa kisheria, maarufu kama gereji bubu, teksi na pikipiki za miguu mitatu ambazo zinafanya biashara kinyume na taratibu ikiwamo kutolipa kodi za jiji kwa mujibu wa sheria.
Kampuni ya Prescanne imepatiwa zabuni namba LGA /018/2015/2016/HS/13, inawajibika kuwatoza faini wahusika wote wanaokwenda kinyume na taratibu hizo, kwa kuzingatia uzito wa kosa na aina ya chombo chake kwa upande wa vyombo vya usafirishaji.
Katika taarifa yake maalum ya utendaji wa kazi ya kuanzia Oktoba 10 hadi Novemba 26, 2016, magari yaliyokamatwa kwa kosa la uegeshaji usio sahihi ni 76. Kati ya idadi hiyo 55 yalitozwa faini na 21 yaliachiwa kwa kupewa onyo kwa maandishi, ikiwa ni pamoja idadi kubwa ya magari ya vigogo mbalimbali wa serikali.
Aidha taarifa hiyo inataja maneo sugu katika Manispaa ya Kinondoni yenye tatizo la maegesho holela kuwa ni Kigogo, Mabibo, Manzese, Kawe na Tegeta.
Adelardo anasema kuwa kampuni hiyo ina utaratibu wa kutoa taarifa ya utendaji kila mara ili kupima uwezo wa uwajibikaji wa kampuni ikiwa ni pamoja na kuboresha utendaji.
“Kwa sasa ripoti yetu imezungumzia zaidi uegeshaji holela, ingawa tumegusia kwa kiasi kuhusu mambo mengine, wakati mwingine tutazungumzia taarifa ya jambo jingine, kwasababu tuna kazi nyingi chini ya zabuni tuliyopewa na Jiji la Dar es Salaam.
“Uwapo wa changamoto za hapa na pale unatufanya kuibua mikakati ya aina mbalimbali kwa ajili ya kuhakikisha kuwa kazi inafanyika bila kuwapo na bughudha katika pande zote tatu; kwa maana ya yule aliyevunja sheria, sisi watendaji, lakini pia kujenga picha nzuri ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam waliotupatia zabuni hiyo,” anafafanua Marcel.
Tofauti na ilivyokuwa katika miaka ya nyuma, Marcel anaelezea kuwa, mfumo uliopo sasa unampa nafasi hata aliyetenda kosa kujutia kile alichokifanya, na pia ulipaji wa faini kwa sasa umeboreshwa zaidi.
“Kwa sasa mtu anapokutwa amevunja sheria anapewa elimu kwanza. Wakati mwingine anaona dhahiri kuwa amekosea na hivyo anapoambiwa kulipa faini, hakuna ubishi. Lakini pia, siku hizi malipo yanafanyika benki, sisi tunapokea ile karatasi ya malipo na kumuandikia mlipaji stakabadhi ya Halmashauri ya Jiji.
“Kuvuta gari au bajaj ya mtu ni hatua ya mwisho kabisa na hasa pale ambapo hatoonesha ushirikiano ikiwamo kushindwa kulipa faini yake kwa wakati huo,” anasema Mkurugenzi huyo.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, bado wanakumbana na changamoto ya baadhi ya watu kutotii sheria, huku baadhi yao wakisingizia kuwa na uhusiano na baadhi ya viongozi wa ngazi za juu nchini.