Taarifa hii ni ya Chama cha Madereva wa Serikali Tanzania, inayohusu tamko la Serikali
la kurejeshwa kazini kwa watumishi wa darasa la saba lililotolewa na Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), George Mkuchika, bungeni Dodoma.
Chama cha madereva kimeipokea taarifa hiyo kwa mshituko mkubwa. Chama na wanachama
tulitegemea kuwa watumishi ambao ni madereva wa darasa la saba walioajiriwa baada ya Mei
2004 mpaka sasa ndiyo warejeshwe kazini na ambao walisema ukweli wakati wa zoezi la
uhakiki wa vyeti ambao walijaza taarifa sahihi kwenye mfumo wa Vitambulisho vya Taifa (NIDA)
nao warejeshwe kazini kufuatia maelekezo ya Mheshimiwa Rais wakati akizungumza na
watumishi wa Bandari ya Dar es Salaam, Septemba 26, 2016.
Rais alisema kuwa uhakiki wa vyeti ni Serikali kujiridhisha kuwa, “je, huyo mtumishi anayelipwa
mshahara wa masters je, ana masters? Kwanini usiseme ukweli ‘mimi’ nimemaliza darasa la
saba, basi kama ulifoji nafuu ujisalimishe useme kwa kweli nilidanganya nilimaliza form
four nikapata division zero kwa hiyo naomba mnipeleke position ya saizi yangu”. Pia
akawauliza, “Na hilo mnalichukia?” Watumishi wakasema, “Hapana”.
Hivyo, akasisitiza kuwa anaowatafuta ni watumishi wakubwa wenye vyeti lundo. Hivyo, chama
kilitekeleza maelekezo hayo ya Mheshimiwa Rais kwa kushirikiana na viongozi wa chama wa
matawi, wilaya, wizara na mikoa. Sisi kama chama Taifa tulitoa maelekezo kwa wanachama
wote (madereva) kuwa utakapofika wakati wa uhakiki watoe taarifa ya kweli.
Napenda kusema kuwa asilimia 99 ya madereva walitoa taarifa ya kweli isipokuwa asilimia 1
waliendelea kudanganya kwa kutoa taarifa ya uongo – wakaondolewa kazini. Hata hivyo,
madereva waliosema ukweli nao wameondolewa kazini.
Hivyo, watumishi anaozungumzia Mheshimiwa Waziri wengi wao wapo kazini isipokuwa
walioondolewa kimakosa ni kutokana na chuki binafsi ya baadhi ya maafisa utumishi wasioitakia
mema Serikali ya Mheshimiwa Rais Magufuli, maana kila siku wanafanya njia mbalimbali ili
Serikali ionekane haifai na sisi madereva tunasema hawatafanikiwa; tupo imara.
MAOMBI YA CHAMA KWA SERIKALI
1. Tunaomba Serikali iwarejeshe kazini madereva wote walioajiriwa baada ya Mei 2004
pamoja na kuwajeresha kazini madereva wote waliosema ukweli wakati wa uhakiki wa vyeti
kutokana na kauli ya Mheshimiwa Rais John Magufuli wakati akihutubia watumishi wa Bandari.
2. Kwa kuwa muundo wa utumishi wa kada ya madereva unamtambua dereva wa Serikali
kama kibarua yaani dereva wa Serikali anaajiriwa kwa masharti ya kada isiyo na taaluma
(operational service), sasa basi tunaomba Serikali kuharakisha utekelezaji wa muundo mpya wa
madereva ambao utamtambua dereva kama kada ya taaluma ili waweze kuthibitishwa kazini
pamoja na kupata pensheni kama watumishi wa kada nyingine.
Kwani madereva walio wengi hawajathibitishwa kazini na wanapostaafu hawalipwi pensheni
kutokana na muundo ulivyo sasa.
3. Tunalishukuru Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutetea wanyonge, pia
tunaliomba Bunge kuwa liishauri Serikali kutunga sheria ya kuwatambua wananchi wa darasa la
saba ambao wamejiendeleza kwa kusoma taaluma mbalimbali na wao wawe miongoni mwa
wananchi watakaoweza kuajiriwa na Serikali kwa kada ndogo ndogo kama vile madereva,
wahudumu, walinzi na kadhalika.
Mheshimiwa Rais anajenga reli kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza na maeneo mengine, sasa
basi reli inapopita sehemu kubwa ni vijijini, sasa ingefaa wananchi wa darasa la saba reli
inapopita waweze kupata hata ajira ya kufyeka majani pamoja na kufanya usafi kwenye
mabehewa. Hii italeta falsafa nzuri ya kuwasaidia wanyonge.
Ikumbukwe kwamba madereva wa darasa la saba walioondolewa walikuwa na uzoefu mkubwa
wa kazi pamoja na ujuzi. Madereva walioajiriwa hivi sasa wengi wao hawana uzoefu wa
kutosha na baadhi yao wamesababisha ajali nyingi mfano TBA-Mamlaka ya Majengo Mwanza,
RAS-Mwanza. Hivyo wanahitaji maelekezo kwa ajili ya kuwapatia uzoefu, sasa tukiwaondoa
madereva wote hakuna atakayewapa maelekezo.
Hata hivyo, kabla ya kutunga Sheria ya Ajira mwaka 2004 ambayo inahitaji mtumishi wa umma
kuwa na elimu ya kidato cha nne ilipaswa kubadiliswa miundo ya utumishi kwanza ya kada ya
madereva, walinzi na wahudumu ili na wao wawe kwenye ajira ya masharti ya kudumu yaani
(permanent and pensionable) ndipo sheria hiyo itumike.
Saidi Yusuph Kapande,
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Madereva wa Serikali – Taifa
0757-410016/0787 410016/0712 645555