Na Isri Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limetoa ripoti ya hali ya kiusalama barabarani katika kipindi cha sikukuu za Krismas na Mwaka Mpya.

Akizungumza na wanahabari leo Januari 2, 2025, Kamanda wa Kanda Maalum Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema Jeshi la Polisi lilifanyakazi ya ufuatiliaji tabia za madereva ili kuzuia na kudhibiti ajali za barabarani, ambapo waliwatuhumu madereva 179.

Baada ya kufanyiwa vipimo madereva 30 waligundulika kutumia kiwango kikubwa cha ulevi cha milligramu 80, huku wakiendesha vyombo vya moto.

Madereva 22 wamekamatwa Wilaya ya Kinondoni, 6 Wilaya ya Ilala na wawili Wilaya ya Temeke.

Kamanda Muliro amesema baada ya kuthibitisha hatua za haraka za kisheria za kuwaweka mahabusu zilichukuliwa hadi kilevi kilipopungua mwilini na kufungiwa leseni zao kwa miezi 6.

“Kwa ujumla katika Kanda Maalum ya Dar es Salaam hakukuwa na ajali zilizopelekea vifo au madhara mengine makubwa katika kipindi chote cha sikukuu za Krismas na Mwaka Mpya” amesema Kamanda Muliro.